Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wafanyabiashara wapigia chapuo ushirikiano Kenya, Tanzania

Mfanyabiashara wa Tanzania, Rostam Aziz akizungumza wakati wa Kongamano la biashara kati ya Kenya na Tanzania lililofanyika  jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kitaifa ya Rais William Ruto

Muktasari:

  • Imeelezwa kuwa, majadiliano kati ya mataifa hayo yanapaswa kuhamia kutoka kwenye biashara ya kawaida na kuelekea ujenzi wa mfumo mmoja wa kibiashara

Dar es Salaam. Viongozi wa biashara kutoka Tanzania na Kenya wametaka kuimarishwa kwa ushirikiano wa kiuchumi, wakisema ni wakati wa nchi hizo kuacha kutegemea biashara ya kawaida  badala yake kujenga mfumo mmoja wenye uwezo wa kuvutia uwekezaji mkubwa.

Akizungumza katika Jukwaa la Uwekezaji la Tanzania na Kenya lililofanyika Mei 4, mfanyabiashara wa Tanzania, Rostam Aziz amesema mustakabali wa uchumi wa nchi hizo mbili unategemea zaidi ushirikiano unaoongozwa na sekta binafsi.

Rostam amesema majadiliano kati ya mataifa hayo yanapaswa kuhamia kutoka kwenye biashara ya kawaida na kuelekea ujenzi wa mfumo mmoja wa kibiashara wenye uwezo wa kushindana kikanda na kimataifa.

“Tunapaswa kuondoka kwenye biashara ya kawaida na kuelekea kitu kikubwa zaidi mfumo unaoweza kushindana na kukua ili kuvutia mtaji kwa masoko ya kikanda na kimataifa,” amesema.

Amesema mbinu hiyo itaziwezesha nchi hizo kufikia kiwango kinachohitajika kuvutia uwekezaji na kuharakisha mabadiliko ya kiuchumi.

Rostam ameeleza kuwa uchumi wa dunia kwa sasa unakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 100 trilioni, huku deni la dunia likifikia takribani Dola 300 trilioni, hali inayopunguza uwezo wa Serikali kukopa zaidi.

“Hii inaleta fursa lakini pia inalazimisha sekta binafsi kuchukua nafasi kubwa katika kuendesha maendeleo,” amesema.

Amesema Kenya tayari imefikia kiwango kikubwa cha ukopaji, huku Tanzania nayo ikikaribia hali kama hiyo, jambo linalofanya ushiriki wa sekta binafsi kuwa muhimu zaidi.

“Uchumi wetu ni mdogo takribani Dola bilioni 130 kwa Kenya na Dola bilioni 100 kwa Tanzania. Lakini tukijumuika, tunakuwa na mvuto mkubwa zaidi kwa wawekezaji,” amesema.

Rostam ametoa wito wa kuoanisha mifumo ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) ili kusaidia miradi mikubwa kupitia masoko ya mitaji kama vile hati fungani na uuzaji wa hisa kwa umma (IPOs).

“Njia hii itabadilisha miundombinu ya nchi zetu na kufungua uwezo wetu halisi wa kiuchumi,” amesema.

Amesema ushirikiano wa kina ndio ufunguo wa kufikia malengo ya muda mrefu, ikiwamo kujenga uchumi wa thamani ya trilioni kadhaa ifikapo mwaka 2050.

“Sioni namna tutafikia lengo hilo bila kufanya kazi pamoja kupitia mfumo mmoja wa kibiashara unaotoa ukubwa unaohitajika kuvutia mtaji,” amesema.

Akitoa maoni yanayofanana na hayo, Mtendaji Mkuu wa KCB Group, Paul Russo amesema kuvutia uwekezaji kunahitaji dhamira thabiti na kuhamia kutoka kutambua fursa hadi kuzitekeleza.

“Mara nyingi tunajikita kwenye fursa badala ya matokeo lazima kuwe na mtu wa kuongoza utekelezaji,” amesema.

Russo amesisitiza sekta binafsi hustawi katika mazingira yenye utabirika na uwazi, akibainisha kuwa kuondoa kutokuaminiana ni muhimu katika kufungua mtiririko wa uwekezaji.

“Kama tunataka kufikia kiwango kikubwa, hatuwezi kuzingatia nchi moja au soko moja pekee. Lazima tuwe jasiri kufungua mipaka,” amesema.

Ameongeza uwekezaji wa kuvuka mipaka kati ya Tanzania na Kenya umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni, akitaja KCB Group kama mfano wa jinsi upanuzi wa kikanda unavyoongeza uimara wa biashara.

“Kama KCB ingebaki katika soko moja, ingepata changamoto wakati wa misukosuko ya kiuchumi. Kuenea katika masoko mbalimbali kumekuwa muhimu kwa ukuaji na uthabiti,” amesema.

Russo pia amehimiza ushirikiano wa karibu zaidi kati ya Serikali na sekta binafsi, akisema pande zote ni washirika katika kukuza maendeleo ya uchumi.