Sababu kudorora viwanda vya nguo nchini

Muktasari:

Tanzania inazalisha wastani watani 700,000 za pamba kila mwaka. Hata hivyo, ni asilimia 30 tu hutumika nchini, huku asilimia 70 zikiuzwa nje ya nchi, hali inayovinyima malighafi za kutosha viwanda vya ndani.

Tanzania inazalisha wastani watani 700,000 za pamba kila mwaka. Hata hivyo, ni asilimia 30 tu hutumika nchini, huku asilimia 70 zikiuzwa nje ya nchi, hali inayovinyima malighafi za kutosha viwanda vya ndani.

Kutokana na hali hiyo, idadi ya viwanda imekuwa ikipungua nchini kutoka 34 vilivyokuwapo miaka ya 1960 mpaka vinane tu vilivyopo sasa, licha ya idadi ya watu kuongezeka hivyo mahitaji ya nguo. Licha ya kilimo cha malighafi hayo muhimu, Tanzania imeendelea kuagiza kiasi kikubwa cha nguo kutoka nje ya nchi, kwani hata viwanda vichache vilivyopo ambavyo vinaajiri takriban wafanyakazi 18,000 vinazalisha kwa kati ya asilimia 40 hadi 60, hivyo kutokidhi mahitaji yaliyopo.

Mwandishi wetu Elias Msuya amezungumza kwa kina na Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Viwanda vya Nguo Tanzania (Tegamat), Adam Zuku masuala kadhaa kuhusu sekta hiyo. Fuatilia:

Swali: Tanzania inazalisha pamba kwa wingi, mnayatumiaje malighafi haya kukuza uzalishaji wa nguo nchini?

Jibu: Kweli Tanzania ni mzalishaji mkubwa wa pamba barani Afrika na pamba hiyo ni bora sana, viwanda vya nguo tunaipendelea zaidi.

Tumekuwa tukitumia pamba hiyo kuendeleza viwanda kwa kadiri ya uwezo wetu kuzalisha kanga na vitenge na mavazi mengineyo kwa soko la ndani hata nje.

Pamoja na Tanzania kuzalisha pamba kwa wingi, ni asilimia 30 tu ndio huuzwa kwa viwanda vya ndani na hiyo ndio tunayotumia kwenye viwanda vyetu.
Kwa hiyo bado hatupati malighafi za kutosha kwa uzalishaji.

Swali: Kama pamba yetu ni nzuri kwa nini msiinunue kwa wingi badala ya asilimia 30 mnayonunua sasa?

Jibu: Tangu zamani nchi yetu imekuwa na uhaba wa fedha za kigeni, kwa hiyo Serikali wakati wote inaangalia namna ya kuzipata fedha hizo za kigeni.

Pamba ni miongoni mwa mazao ya biashara yanayoiingizia Serikali fedha hizo, hivyo ni suala lililo nje ya uwezo wa wamiliki wa viwanda pekee kwa sababu sokoni hatupo peke yetu.

Ili ununue pamba inabidi uwe na fedha ambazo viwanda vingi havina za kutosha. Changamoto iliyopo ni kwamba ukienda kukopa benki nao wanakuuliza namna utakavyolipa deni hilo kwa sababu benki nao wanaangalia mwenendo wa soko la nguo nchini.

Ukienda viwandani, utakuta vitenge vingi tu vimejaa stoo vikisubiri wateja, lakini sokoni waliko kumejaa vitenge na nguo nyingine zinazoweza kutengenezwa nchini zilizoagizwa kutoka nje ya nchi.

Swali: Kwa mazingira yaliyopo unadhani kuna haja ya kuongeza uzalishaji wa pamba ili viwanda vya ndani navyo viwe na uhakika wa malighafi?

Jibu: Ni muhimu kufahamu kwamba sisi tunazalisha pamba nyingi kuliko Uganda na tuna viwanda vingi kuwazidi lakini wao, wamewavutia wawekezaji kwa kuwapunguzia gharama za uzalishaji.

Kwanza Serikali inawahakikishia wenye viwanda kupata pamba ya kutosha katika kila msimu wa mavuno. Serikali pia inaelewana na benki za biashara kuwakopesha wenye viwanda hivyo kwa kuwapa dhamana tofauti na sisi tunaojitegemea kwa kila kitu. Uganda pamba inakuwa chini ya uangalizi wa benki.

Mwenye kiwanda anapewa pamba ya mwezi mmoja, anazalisha, ikiisha anapewa nyingine wakati hapa Tanzania unatakiwa ununue pamba ya jumla katika msimu wa mavuno utakayoitumia mwaka mzima, nani anao huo uwezo?

Jambo la pili, Serikali nchini Uganda hazitozi Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) bidhaa za nguo tofauti na hapa kwetu, sisi tunatozwa.

Kwa Uganda, haishii kwenye kupewa pamba tu, kuna mambo mengi ambayo wamiliki wa viwanda vya nguo wanafanyiwa na Serikali yao tofauti na sisi. Hilo linafanyika pia hata kwenye nchi nyingine jirani ambazo zimetupita kwenye sekta hiyo.

Sisi hapa tunalipia umeme kati ya senti 10 na 12 za Marekani, lakini Uganda wawekezaji wanatozwa senti nne tu kwa kilowati moja. Huwezi kushindana na mtu mwenye mazingira hayo. Tukiboreshewa na sisi, tutazalisha zaidi, hivyo kutumia pamba nyingi zaidi inayolimwa nchini.

Swali: Kwa mwenendo wa uzalishaji uliopo viwandani, hali ya biashara ikoje sokoni?

Jibu: Tangu miaka ya 1960 viwanda vya nguo vimekuwa mchanzo kikubwa cha kodi serikalini na ajira kwa raia vikiajiri zaidi ya wafanyakazi 75,000.

Viwanda vya nguo, kama ilivyo kwa vingine nchini vimekuwa vikidorora kutokana na kukosekana kwa umeme kunakochangiwa na kushuka kwa kina cha maji kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme, yakiwamo ya Kidatu na Mtera tangu mwanzoni miaka ya 1990 mpaka sasa.

Kutokana na changamoto hiyo iliyoanza mwanzoni mwa miaka ya 1990, Serikali iliruhusu uingizaji nguo kutoka nje, hasa India na China.

Mpaka mwaka 2000 tulikuwa na viwanda 33, lakini vimekuwa vikipungua kadiri muda unavyoenda. Mwaka 2015 tulikuwa na viwanda 17, ila sasa vimebaki viwanda vinane na vingine viwili vilivyopo ndani ya Eneo la Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) ambavyo huzalisha mahsusi kwa ajili ya kuuza katika soko la nje.

Kwa ujumla viwanda hivi kwa sasa vinafanya kazi kwa uzalishaji wa kati ya asilimia 40 mpaka asilimia 60 kutokana na kukosa masoko kunakosababishwa na ushindani wa nguo zinazoingizwa kutoka nje. Ushindani uliopo hauko sawa kati ya waingizaji hao na wazalishaji.

Kupungua kwa viwanda hivi kunachangiwa na kuingiliwa kwa soko, huku nguo nyingi zikiingizwa kwa magendo kutoka kwa wafanyabiashara wanaolenga kupata faida kubwa.

Siku hizi utaona viwanda vina maduka yao wakati zamani hakukuwa na haja ya kufanya hivyo kwa sababu wafanyabiashara walikuwa wanakuja moja kwa moja kiwandani, lakini sasa hivi hali ni tofauti, hawaji kwetu kwa sababu wanaingiza kwa bei ya chini kutoka nje ya nchi.

Wafanyabiashara wanapenda bidhaa kutoka nje kutokana na faida kubwa wanayoipata ama kwa kutolipa ushuru na kodi stahiki au kuziingiza kwa magendo, hivyo kutumia gharama kidogo.

Sio kwamba hatutaki nguo za nje ziingie nchini, hapana. Tunachosema tuwe na soko halali. Kwa gharama halisi, kitenge cha China pale Kariakoo kinatakiwa kiuzwe Sh58,000 kwa jora moja (mita 10) siyo wanavyouza Sh35,000. Kwa bei hiyo, kuna udanganyifu unafanyika. Tunaweza kuboresha ubora hata mara tatu ya ule wa China kukiwa na soko lenye usawa. Hatushindwi kufanya hivyo.

Swali: Wafanyabiashara wanaoingiza vitenge kutoka nje ya nchi wanalalamika kutozwa kodi kubwa inayolenga kulinda viwanda vya ndani, nanyi bado mnalalamika?

Jibu: Tanzania ikiwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inatoza ushuru wa forodha kwa mujibu wa East African Customs Management Act 2005 (Sheria ya Forodha ya EAC ya mwaka 2005) ili kuhakikisha viwanda haviathiriki na bidhaa nafuu kutoka nchi zilizoendelea zaidi kwa viwanda na teknolojia kuliko sisi.

Hivyo bidhaa kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki hutozwa ushuru huo wa forodha. Uganda kwa mfano, wanatoza nguo zote dola tatu za Marekani kwa kilo au asilimia 35, kiasi chochote kitakachokuwa kikubwa.

Kwa mantiki hii ushuru wa forodha kwa mita moja ya wax kitenge cha uzito wa gram 190 itakuwa Sh1,304, ukiongeza tozo ya asilimia 50 itakuwa Sh2,609 kwa mita. Kwa maana nyingine Uganda wanatoza ushuru kwa zaidi ya Sh2,288 wakati sisi tunatoza Sh1,830 tu.

Gharama ya pamba sasa hivi ni Sh5,538 kwa kilo moja. Pamba iliyomo kwenye kitenge ni gramu 190 (kilo 0.19) ambayo gharama yake ni Sh1,052 sasa inawezekanaje kitenge kiuzwe Sh823.85 kama wanavyotaka wafanyabiashara? Nchi zote wanachama Jumuiya ya Afrika Mashariki tunatoza kodi sawa kwa mujibu wa sheria.

Swali: Pamoja na kununua pamba kutoka kwa wakulima, kuna taarifa pia mnanunua vitambaa kama malighafi na mnachapisha kuwa vitenge kwa gharama nafuu. Lina ukweli gani hili?

Swali: Ni kweli tunaingiza vitambaa wakati mwingine, lakini vinalipiwa kodi zote zinazostahili.

Kwa sababu sheria iliyopo inafafanua kwamba ukileta kitu kilichokamilika kama kitenge kina kodi yake, ukileta kitambaa ambacho hakijawa kitenge pia na chenyewe kina kodi yake. Kwa hiyo tunaleta vitambaa na tunalipa kodi kwa mujibu wa sheria.

Kitambaa chenyewe (grey) ni senti dola 45 (kabla ya kodi). Tunaingiza vitambaa kwa sababu wakati mwingine pamba inauzwa hivyo sisi tunakosa. Wakati mwingine tunaingiza pamba kutoka nje pia.