Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sanaa za maonesho na ubunifu fursa kwa wahitimu vyuoni

Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imeendelea kushuhudia ongezeko kubwa la vijana wanaohitimu kutoka vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za elimu. Hata hivyo, changamoto ya ukosefu wa ajira rasmi imeendelea kuwa tatizo kubwa linalowakabili wengi wao.

Kutokana na hali hiyo, kuna haja ya kuangalia sekta mbadala zenye uwezo wa kuzalisha ajira na kipato. Miongoni mwa sekta hizo ni sanaa za maonesho na ubunifu (Fine and Performing Arts), ambazo zimekuwa zikikua kwa kasi na kutoa fursa nyingi za kiuchumi.

Kwa muda mrefu, jamii nyingi zimekuwa zikichukulia sanaa kama shughuli za burudani pekee. Mtazamo huo umesababisha vijana wengi kushindwa kuona thamani ya taaluma za sanaa katika kujenga maisha yao. Hata hivyo, hali imebadilika sana katika dunia ya leo ambapo sanaa zimegeuka kuwa sekta muhimu ya uchumi wa ubunifu (creative economy) inayochangia ajira, mapato ya kodi na ukuaji wa uchumi wa taifa.

Sanaa za maonesho zinajumuisha muziki, uigizaji, ngoma, tamthilia, filamu na uwasilishaji wa matukio mbalimbali ya kitamaduni. Kwa upande mwingine, sanaa za ubunifu zinahusisha uchoraji, usanifu wa picha, uchongaji, utengenezaji wa bidhaa za mikono, upigaji picha na ubunifu wa kidijitali. Kila eneo kati ya haya lina uwezo mkubwa wa kuwapatia vijana ajira za kujiajiri na hata kuajiri wengine.

Mfano mzuri ni sekta ya muziki nchini Tanzania ambayo imezalisha mamia ya wasanii, watayarishaji wa muziki, wapigapicha za video, waongozaji wa kazi za sanaa na mameneja wa vipaji. Kupitia majukwaa ya kidijitali kama YouTube, TikTok na Instagram, vijana wanaweza kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi bila gharama kubwa.

Kadhalika, sekta ya filamu na maigizo imeendelea kukua na kutoa nafasi kwa waigizaji, waandishi wa miswada, wapiga picha, wahariri wa video na wataalamu wa sauti. Ukuaji wa televisheni za mtandaoni na majukwaa ya kidijitali umeongeza mahitaji ya maudhui ya ubunifu, hivyo kuongeza nafasi za ajira kwa vijana wenye vipaji na ujuzi wa sanaa.

Katika upande wa sanaa za ubunifu, vijana wanaweza kujihusisha na utengenezaji wa bidhaa za mikono, michoro ya kisasa, usanifu wa nembo na matangazo ya biashara. Biashara nyingi leo zinahitaji wabunifu wa picha (graphic designers) kwa ajili ya kutangaza bidhaa na huduma zao.

Pamoja na fursa hizi, bado kuna changamoto mbalimbali ikiwamo ukosefu wa mitaji, vifaa vya kisasa, mafunzo ya kibiashara na mifumo madhubuti ya kulinda hakimiliki. Serikali, taasisi za elimu na sekta binafsi zinapaswa kushirikiana kuimarisha mazingira ya ukuaji wa sekta ya sanaa kwa kuwekeza katika mafunzo, vituo vya ubunifu na upatikanaji wa masoko. Vyuo vikuu na vyuo vya ufundi pia vinapaswa kuendelea kuimarisha programu za sanaa na ubunifu ili kuwajengea vijana ujuzi unaoendana na mahitaji ya uchumi wa kidijitali. Aidha, wazazi na jamii kwa ujumla wanapaswa kuondokana na dhana kwamba taaluma za sanaa hazina mchango katika maendeleo ya maisha ya mtu mmoja mmoja na taifa.

Kwa kuzingatia mwelekeo wa dunia ya sasa, sanaa za maonesho na ubunifu zina nafasi kubwa ya kuwa chanzo muhimu cha ajira na maendeleo ya kiuchumi nchini Tanzania. Vijana wanapaswa kuona sekta hii kama fursa halisi ya kujenga mustakabali wao badala ya kusubiri ajira rasmi pekee.