SBC yalipa kodi ya Sh1 trilioni, yatanua uwekezaji
Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Vinywaji ya SBC Tanzania, Ziad El Khalil, akizungumza na Mkurugenzi wa Kituo cha Vijana Wenye Ulemavu na Watoto Tanzania (Mihayo Tanzania), Linda Ngido, wakati wa maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo. SBC Tanzania iliadhimisha kwa kutoa msaada wa kibinadamu kwa kituo hicho kilichopo Mazimbu, Manispaa ya Morogoro. Picha na Juma Mtanda.
Muktasari:
- Kampuni ya SBC Tanzania yasema imelipa zaidi ya Sh1 trilioni kodi katika kipindi cha miaka 25 ya shughuli zake nchini huku ikitoa ajira zaidi ya 100,000 huku ikitangaza kuongeza mtambo mpya katika kiwanda chake cha Arusha na kujenga kiwanda kipya Dodoma ili kuongeza uzalishaji.
Morogoro. Kampuni ya SBC Tanzania imesema imelipa zaidi ya Sh1 trilioni kama kodi kwa Serikali ndani ya kipindi cha miaka 25 ya shughuli zake nchini, huku ikitangaza mpango wa kupanua uwekezaji kwa kuongeza mtambo mpya katika kiwanda chake cha Arusha na kujenga kiwanda kipya mkoani Dodoma.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza uwezo wa uzalishaji, kufungua ajira mpya na kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Akizungumza leo Jumamosi Julai 25, 2026, katika maadhimisho ya miaka 25 ya kampuni hiyo yaliyofanyika mkoani Morogoro, Mkurugenzi Mtendaji wa SBC Tanzania, Himanshu Shekhar, amesema mafanikio ya kampuni yametokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali, ushirikiano wa wadau pamoja na kujituma kwa wafanyakazi.
Amesema katika kipindi hicho kampuni imechangia zaidi ya Sh1 trilioni kupitia kodi zinazokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), fedha ambazo zimeendelea kusaidia Serikali kugharamia huduma za kijamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
"Tunajivunia kuwa sehemu ya maendeleo ya Tanzania kupitia ulipaji wa kodi, uwekezaji na utoaji wa ajira. Mafanikio haya yametokana na ushirikiano mzuri tulioujenga na Serikali, wafanyakazi na wadau wetu mbalimbali," amesema Shekhar.
Ameongeza kuwa tangu kuanza shughuli zake nchini, SBC imewekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni 100 katika shughuli za uzalishaji na upanuzi wa biashara, huku ikiendelea kuweka mikakati ya kuongeza uwekezaji katika miaka ijayo.
Kwa mujibu wa Shekhar, hatua inayofuata ni kuongeza mtambo mpya katika kiwanda cha Arusha ili kuongeza uzalishaji, sambamba na ujenzi wa kiwanda kipya mkoani Dodoma kitakachopanua shughuli za kampuni na kuongeza fursa za ajira.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Vinywaji ya SBC Tanzania, Ziad El Khalil, akimlisha kipande cha keki mmoja wa watoto wa Kituo cha Vijana Wenye Ulemavu na Watoto Tanzania (Mihayo Tanzania), wakati wa maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo. Picha na Juma Mtanda.
Amesema kwa sasa kampuni ina wafanyakazi wa kudumu zaidi ya 1,200 na wafanyakazi wa msimu zaidi ya 15,000, huku shughuli zake zikichangia zaidi ya ajira 100,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kupitia uzalishaji, usafirishaji, usambazaji wa bidhaa na huduma nyingine zinazotokana na uwekezaji wake.
Mbali na shughuli za biashara, SBC imeendelea kutekeleza miradi ya uwajibikaji kwa jamii, ambapo katika maadhimisho hayo iliahidi kutoa bajaji kwa Kituo cha Vijana Wenye Ulemavu na Watoto Tanzania (Mihayo Tanzania) ili kuboresha huduma za usafiri kwa watoto na vijana wanaolelewa katika kituo hicho.
Mkurugenzi wa Mihayo Tanzania, Linda Ngido, amesema kituo hicho kinahudumia jumla ya wanufaika 91, wakiwemo watoto wenye ulemavu wa akili, vijana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Amesema watoto 45 kati ya hao wanasoma katika shule za Serikali za elimu maalumu, huku vijana 31 wenye umri wa kati ya miaka 20 na 52 wakipatiwa mafunzo ya kilimo cha bustani, ufundi wa sanaa na useremala ili kuwawezesha kujitegemea.
Ngido alisema changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa usafiri wa kuwahudumia walengwa wanaoishi maeneo ya Mazimbu na Mkundi pamoja na uhaba wa vyumba vya kulala, akibainisha kuwa msaada wa bajaji utarahisisha utoaji wa huduma na kupunguza gharama za uendeshaji.
"Tunatoa elimu jumuishi, huduma za afya, mafunzo ya ufundi na stadi za maisha kwa watoto yatima na vijana wenye ulemavu wa akili ili waweze kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii," amesema.
Kwa upande wake, Meneja Mauzo wa SBC Tanzania Kanda ya Morogoro na Dodoma, Kassim Zarafi, amesema maadhimisho ya miaka 25 ya kampuni hiyo hayakulenga kusherehekea mafanikio pekee, bali pia kurejesha sehemu ya mafanikio hayo kwa jamii kupitia shughuli za kijamii.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) tawi la SBC Morogoro, Noah Boneka, amesema ukuaji wa kampuni umeenda sambamba na kuboreshwa kwa maslahi ya wafanyakazi kupitia mikataba ya hali bora kazini.
Amesema hatua hiyo imechangia kuinua ustawi wa wafanyakazi na familia zao, kuongeza ajira kwa Watanzania na kuonyesha jinsi uwekezaji wa sekta binafsi unavyoweza kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na kuboresha maisha ya wananchi kupitia ajira pamoja na miradi ya maendeleo ya kijamii.