Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaweka jicho sakata la mafuta, Kamati yataka ruzuku

Muktasari:

  • Kamati ya Nishati na Madini imetoa ushuri huo bungeni jijini Dodoma kupitia maoni yake kuhusu hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, iliyosomwa na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikisema inafuatilia kwa karibu mwenendo wa upatikanaji wa mafuta duniani na kuwa itachukua hatua kulingana na hali itakavyokuwa, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, imeshauri itolewe ruzuku kutoka kwenye bajeti.

Hatua hiyo, Kamati imesema ilenge kupunguza makali ya bei za petroli na dizeli ambazo kwa mwezi Aprili, mwaka huu zimeongezeka kwa zaidi ya Sh900 kwa lita na kusababisha baadhi ya huduma zikiwemo nauli za usafiri wa umma kupaa.

Hata hivyo, wakati Kamati ya Bunge ikishauri hilo, Tanzania bado inatajwa kuwa na bei ya chini ya nishati hiyo ikilinganishwa na baadhi ya nchi jirani, ambazo watumiaji wamekuwa wakiugulia maumivu zaidi.

Wabunge wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2026/27, leo, Aprili 22, 2026, bungeni jijini Dodoma.

Bei za mafuta zimepanda duniani kutokana na mivutano ya kisiasa Mashariki ya Kati hasa athari za kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz unaopitisha zaidi ya asilimia 20 ya mafuta yote duniani.

Kamati ya Nishati na Madini imetoa ushuri huo bungeni jijini Dodoma kupitia maoni yake kuhusu hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, iliyosomwa na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi.

Katika hotuba hiyo, Waziri Ndejembi alisema: “Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa upatikanaji wa mafuta duniani na itaendelea kuchukua hatua za kimkakati ili kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta, ili kutoathiri utekelezaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii nchini,” alisema.

Katika ufafanuzi wake, alisema pamoja na ufuatiliaji katika soko la dunia, Serikali imeliwezesha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuagiza mafuta yanayotosheleza matumizi ya miezi mitatu ya Mei, Juni na Julai mwaka huu.

Ndejembi alisema Tanzania inategemea asilimia 59 ya mafuta kutoka Mashariki ya Kati akizitaja nchi za Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Bahrain, Oman na Kuwait huku asilimia 41 ikiagiza kutoka India.

“Utegemezi huu unaifanya Tanzania kuwa katika nafasi nyeti wakati wa misukosuko ya kimataifa, hasa pale changamoto zinapohusu maeneo muhimu ya usafirishaji kama Hormuz,” alisema.

Katika hotuba hiyo, alisema licha ya wastani wa bei ya mafuta ghafi kushuka kwa asilimia 14 na kufikia dola 66 kwa pipa kati ya Julai 2025 na Machi 2026, hali ilibadilika Machi mwaka huu, baada ya bei kupanda hadi dola 102 kwa pipa.

Alisema ongezeko hilo lilisukuma pia bei za mafuta yaliyosafishwa kupanda. Kati ya Februari na Machi 2026, bei ya petroli iliongezeka kwa asilimia 69.12, dizeli asilimia 104.30 na mafuta ya taa na ya ndege asilimia 115.83.

Ndejembi, alisema pamoja na changamoto hizo, Serikali itaendelea kutumia hatua za kimkakati kulingana na maendeleo ya hali hiyo, huku ikiendelea kufuatilia mwenendo wa soko la dunia.

“Tunafanya hivi ili kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kijamii haziathiriwe na mishtuko ya mafuta,” alisema.

Alisema Tanzania ilipokea lita bilioni 5.84 za mafuta katika kipindi husika. Kati ya hizo, lita bilioni 1.63 za petroli, bilioni 3.94 za dizeli na milioni 260 za mafuta ya taa na ndege, huku sehemu ya mafuta hayo ikihudumia pia nchi jirani.


Ushauri wa Kamati

Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Nishati na Madini, mwenyekiti wa kamati hiyo, Subira Mgalu alipendekeza Serikali iangalie uwezekano wa kufanya uhamisho wa fedha kati ya mafungu ya matumizi ya kawaida na kuzielekeza katika ruzuku ya mafuta, ili kusaidia kudhibiti kupanda kwa bei.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, akizungumza wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2026/27, leo Aprili 22, 2026, bungeni jijini Dodoma.

“Utoaji wa ruzuku ya muda kwa mafuta unaweza kutoa ahueni kwa wananchi katika kipindi cha miezi mitatu huku Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya athari za mwenendo wa vita unaoendelea kwenye soko la mafuta duniani,” alisema.

Mbali na ruzuku, Kamati imeitaka Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kuharakisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa matenki ya kuhifadhi mafuta kimkakati, hatua itakayosaidia nchi kuwa na akiba ya uhakika na kupunguza athari za misukosuko ya soko la dunia.

Katika taarifa hiyo, Subira amesema kamati ilipokea maelezo ya Serikali kuhusu hatua zilizochukuliwa kutafuta suluhu ya upatikanaji wa mafuta nchini kwa bei himilivu, ikiwamo kuipa TPDC jukumu la kuagiza mafuta kwa kipindi cha dharura.

Subira alisema uamuzi huo umechukuliwa kwa mujibu wa sheria, ambapo vifungu vya sheria na kanuni za uagizaji wa mafuta kwa pamoja vimetoa mamlaka kwa Waziri anayesimamia nishati kuweka utaratibu mbadala wa kununua mafuta nje ya mfumo wa kawaida katika kipindi cha dharura.

“Kamati pia iliridhishwa na mchakato wa ushindanishaji wa makampuni 11 uliofanywa na PBPA na TPDC na hatimaye kupatikana mzabuni mwenye bei nafuu atakayetekeleza jukumu hilo kwa muda wa miezi mitatu,” amesema.


Unafuu bei Tanzania

Ingawa kupanda kwa bei ya mafuta ni janga linaloyakabili mataifa yote duniani, angalau Tanzania imetajwa kuwa na unafuu wa bei ya nishati hiyo, ukilinganisha na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kuanzia Aprili mwaka huu, bei ya lita moja ya Petroli kwa Dar es Salaam ni Sh3,820 kwa lita, dizeli Sh3,650 na mafuta ya taa ni Sh3,400 kwa lita. Bei hiyo ni nafuu zaidi ukilinganisha na Rwanda ambako bei ya lita moja ya Petroli kwa Aprili imefika RWF 2,303 (sawa na Sh4,600), dizeli RWF 2,200 (Sh4,400) na mafuta ya taa RWF 2,050 (Sh 4,100).

Kwa upande wa Kenya taarifa ya Aprili 15 hadi Mei 14, mwaka huu, inaonyesha bei ya lita moja ya petroli ni KSh206.97 (sawa na Sh3, 830), dizeli ni KSh193.13 (Sh3,573) na mafuta ya taa KSh163.71 (Sh3,029).

Unafuu huo wa bei kwa Tanzania ukilinganisha na baadhi ya nchi Afrika Mashariki, unahusishwa na masuala ya sera, miundombinu na mifumo ya usimamizi wa nishati, kama inavyofafanuliwa na wachambuzi na wanazuoni wa uchumi.

Akizungumzia hilo, mchambuzi wa uchumi, Dk Baraka Mfinanga alieleza sababu ni nafasi ya kijiografia ya Tanzania, inayoifanya kuwa lango kuu la mafuta kwa nchi nyingi za Afrika.

“Bandari ya Dar es Salaam ni lango kuu la mafuta kwa nchi nyingi za Afrika. Hii inapunguza gharama za usafirishaji kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na nchi zisizo na bandari kama Rwanda,” alisema.

Ameongeza mbali na uwepo wa bandari, Tanzania pia imewekeza katika miundombinu ya uhifadhi wa mafuta, hali inayopunguza utegemezi wa uagizaji wa haraka wa mafuta wakati bei za dunia zinapopanda ghafla.

Aidha, mwanazuoni huyo, amesema anaiona nafasi ya Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa mafuta kwa nchi jirani kama Uganda na Rwanda inaongeza ufanisi wa soko.

Kwa upande wake, Mtafiti wa Sera za Uchumi, Neema Kalinga ameeleza mfumo wa kodi nchini Tanzania una mchango mkubwa katika kudhibiti bei.

“Ingawa kuna tozo mbalimbali, Serikali imekuwa ikifanya marekebisho ya mara kwa mara ili kuhakikisha bei hazipandi kupita kiasi. Hii ni tofauti na baadhi ya nchi ambazo kodi zake ni kubwa na hazibadiliki kirahisi,” alisema.

Naye, mchambuzi wa masuala ya biashara na usafirishaji, Hassan Mwakyusa amehusisha hali hiyo na suala la ushindani wa soko.

“Kadiri washindani wanavyoongezeka, ndivyo inavyokuwa vigumu kwa bei kupanda kiholela. Hii imekuwa tofauti kidogo na baadhi ya nchi jirani ambazo soko lina watu wachache,” alisema.