Sh1.4 trilioni zitakavyobadilisha hali ya umeme nchini ifikapo 2030

Dar es Salaam. Katika harakati za kujenga uchumi wa viwanda na kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa Watanzania wote, uwekezaji katika vyanzo mbadala vya umeme unazidi kuwa jambo lisiloepukika.
Kwa Taifa linalokua kwa kasi kama Tanzania, kutegemea vyanzo vya jadi kama maji na mafuta pekee si salama tena hasa kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kupanda kwa gharama za mafuta duniani.
Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za uzalishaji wa nishati mbadala kama jua, upepo, jotoardhi na biogesi ambazo bado hazijatumika kikamilifu.
Uwekezaji katika maeneo haya sio tu kwamba unaleta umeme safi na wa kudumu, bali pia unachochea maendeleo ya kiuchumi, kuboresha huduma za kijamii vijijini na kupunguza utegemezi wa nje. Ni njia ya kuimarisha mustakabali wa nishati wa nchi kwa njia endelevu na jumuishi.
Katika kutambua umuhimu huo, zaidi ya Sh1.48 trilioni zimepangwa kutumika hadi mwaka 2030 katika kuendeleza miradi miwili mikubwa ya umeme wa jotoardhi katika maeneo ya Ngozi Crater na Kiejo-Mbaka, mkoani Mbeya.
Uendelezaji wa miradi hiyo utafanywa na Kampuni ya Maendeleo ya Umeme Jotoardhi Tanzania (TGDC), ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Akizungumza katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa TGDC, Shakiru Kajugus anasema mradi wa Ngozi Crater unatarajiwa kuzalisha megawati 70 huku ule wa Kiejo-Mbaka ukitarajiwa kuzalisha megawati 60.
“Kwa pamoja, miradi hii miwili itachangia megawati 130 kwenye gridi ya taifa ifikapo mwaka 2030. Huu ni mchango muhimu katika juhudi za kuongeza vyanzo vya nishati mbadala na ya uhakika nchini,” anasema Kajugus.
Kwa mujibu wa TGDC, Tanzania ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 5,000 kutoka kwenye vyanzo vya jotoardhi, lakini kwa sasa lengo ni kufanikisha megawati 130 kama hatua ya awali.
Umeme huo utachangia pia katika jitihada za Afrika za kuhakikisha watu milioni 300 ambao bado hawajafikiwa na huduma hiyo wanafikiwa. Mradi wa Ngozi, ambao ulianza mwaka 2015, uko hatua za mwisho za utekelezaji na unatarajiwa kuanza kwa kuchimbwa visima vitatu vya jotoardhi ndani ya mwezi huu.
Visima hivyo vitachimbwa kwa urefu wa mita 1,500 ili kufikia kina chenye joto la nyuzi joto 250.
“Tunatarajia zoezi la uchimbaji litadumu kwa miezi sita. Maandalizi yote yamekamilika na tunawakaribisha wananchi kutembelea banda letu hapa Sabasaba kwa ajili ya kupata elimu zaidi kuhusu miradi hii,” alisema Kajugus.
Mbali na Ngozi na Kiejo-Mbaka, maeneo mengine yaliyopewa kipaumbele na TGDC kwa ajili ya maendeleo ya jotoardhi ni Songwe, Lohoi (Pwani) na Natron (Arusha).
Kwa ujumla, TGDC imetambua zaidi ya maeneo 50 yenye chemichemi za moto katika mikoa 16 yenye uwezekano wa kuzalisha nishati hiyo.
Kajugus anasema miradi ya jotoardhi si tu kwamba inaweza kutoa umeme wa uhakika kwa gharama nafuu bali pia ina faida kubwa kiuchumi na kijamii.
Anasema matumizi ya jotoardhi katika sekta mbalimbali yatasaidia kuongeza mapato ya serikali, kutoa ajira na kuleta maendeleo ya haraka kwenye jamii.
Katika kufanikisha miradi hiyo, TGDC inashirikiana kwa karibu na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kutoa msaada wa kitaalamu, kujenga uwezo na kusaidia upatikanaji wa fedha.
“JICA imekuwa mdau wetu mkubwa. Kwa sasa tuna wahandisi wawili walioko nchini Japan wakisomea Shahada ya Uzamili katika masuala ya jotoardhi,” anasema Kajugus.
Historia ya maendeleo ya nishati ya jotoardhi nchini Tanzania ilianza miaka ya 1970 ambapo tafiti mbalimbali za kisayansi zilifanywa kwenye Ukanda wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki.
Kati ya mwaka 1976 hadi 1979, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweden (SIDA) liliwezesha uchunguzi wa awali wa maeneo yenye jotoardhi yakihusisha ushirikiano wa wataalamu kutoka makampuni ya SWECO na Virkir-Orkint kutoka Sweden na Iceland.
Katika tafiti hizo, jumla ya chemchemi 50 za maji moto kutoka kaskazini mwa Tanzania hadi Mbeya zilifanyiwa uchunguzi na kubainishwa kuwa zina viwango tofauti vya joto vinavyoweza kufaa kwa uzalishaji wa nishati.
Hali ya umeme nchini
Wakati wa Bunge la Bajeti Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko aliliambia Bunge kuwa hadi Aprili, 2025, uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa ulikuwa Mega Watt (MW) 4,031.71.
Katika kiasi hicho, MW 2,716.27 (asilimia 67.4) ni umeme unaotokana na maji; MW 1,198.82 (asilimia 29.7) gesi asilia, MW 101.12 (asilimia 2.5) mafuta, MW 5 (asilimia 0.1) jua na MW 10.5 (asilimia 0.3) tungamotoka.
Katika hilo, Mchambuzi wa Uchumi na Biashara, Oscar Mkude anasema jotoardhi ni chanzo muhimu cha umeme sawa na umeme wa maji.
Anasema kwa sasa Tanzania inatarajia kutumia vyanzo vya nishati mbadala kama vile jua na upepo siku za hivi karibuni lakini vyanzo hivi vina muda havifanyi uzalishaji mzuri nyakati za mawingu au jioni kwa Umeme Jua, na nyakati ambapo upepo hauvumi kwa kasi kwa upande wa umeme upepo. “Hivyo, unapokuwa na sehemu ya uhakika kama jotoardhi au umeme wa maji inasaidia kufanya grid isitetereke na kuhakikisha upatikanaji wa umeme muda wote,” anasema.
Hata hivyo anatoa angalizo kuwa ni vyema chanzo hiki cha nishati ambacho ni kipya nchini kuangaliwa kwa umakini.
“Tunapaswa kukiendea kwa umakini wa juu na kushirikiana na wenzetu wenye uzoefu nacho ili kuepuka kufanya makosa na kuingia hasara,” anasema.