Sh18 bilioni zitakavyoleta neema kwa wauza dagaa

Wachuuzi wa dagaa wakilazimika kuingia majini kuifuata mitumbwi kwenye Ziwa Victoria, mwalo wa Mswahili kutokana na ubovu wa miundombinu wa eneo hilo. Picha na Anania Kajuni

Mwanza. Kilio cha muda mrefu cha wadau wa sekta ya uvuvi kuhusu ubovu wa miundombinu katika mialo kimesikika baada ya Serikali kutenga zaidi ya Sh18 bilioni kutekeleza miradi ya ujenzi na maboresho ya masoko ya samaki nchini.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema hatua hiyo ni miongoni mwa jitihada za Serikali kuboresha na kuimarisha sekta ya uvuvi kufikia lengo la kuongeza tija na mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa.

Akizungumza na wadau wa uvuvi wakati wa ziara yake mkoani Mwanza mwishoni mwa wiki iliyopita, Ulega alisema kila mwaka wa bajeti, Serikali itatenga fedha kulingana na mahitaji na uwezo wa kibajeti.

Ahadi hiyo ya Serikali ni neema kwa wavuvi na wafanyabiashara wa mazao ya samaki katika mialo kadhaa ya Ziwa Victoria ambayo haina gati kwa ajili ya boti za uvuvi kutia nanga.

Kukosekana kwa magati katika mialo hiyo huwafanya wavuvi kutia nanga katika kina kirefu cha maji, hivyo kuwalazimisha wafanyabiashara, wachuuzi na wateja wanaohitaji samaki kuingia majini kufuata bidhaa hiyo.

Kwa Jiji la Mwanza, uwekezaji huo utawanufaisha wavuvi na wachuuzi, wengi wao wakiwa wanawake katika mialo ya Igombe, Mkuyuni, Kayenze, Bwiru na Luchelele.

Mmoja wa wachuuzi wa dagaa katika mwalo wa Mkuyuni, Zuwena Rashid anasema uwekezaji huo si tu utaboresha miundombinu ya biashara, pia utamaliza tatizo la wao kulazimika kuingia ndani ya maji kufuata bidhaa kutoka kwenye boti za uvuvi kutokana na kushindwa kufika ufukweni kwa kukosekana gati.

“Anayeingia majini hununua bidhaa kati ya Sh10,000 hadi 15,000 lakini anayesubiri nchi kavu hulazimika kununua dagaa kwa bei ya ulanguzi kutoka kwa walioingia majini kati ya Sh15,000 hadi Sh20,000 kwa sado,” anasema.


Maambukizi ya magonjwa

Mwamvua Salehe, mchuuzi wa dagaa mwalo wa Mswahili anasema kitendo cha kuingia majini kufuata bidhaa kinawaweka katika hatari ya kiafya kwa kupata maradhi ya kuambukiza ikiwemo kichocho na fangasi.

 Kauli hiyo iliungwa mkono na Josephina Nduta na Hadija Jamed wanayoiomba Serikali iharakishe utekelezaji wa mradi wa kujenga gati katika mwalo wa Mswahili, ili kuwezesha boti za uvuvi kutia nanga eneo ambalo hawatalazimika kuingia majini.

Naye Monica Paula anasema kulowana na nguo kushika miili, hivyo kuchoresha maumbile yao ni udhalilishaji wa utu na heshima. “Naomba Serikali ituondolee adha hii kwa kujenga gati,’’ anasema.

Adha nyingine wanayoipata wachuuzi wa dagaa ni maneno ya karaha na ugomvi katika vyombo vya usafiri kati yao na abiria wengine.

“Wakati mwingine ugomvi hutokea ndani ya daladala kati ya wachuuzi wa dagaa na abiria pindi wanapogusana kwa sababu ya kulowa na kuwa na shombo la dagaa," anasema Monica.

Njia za daladala zenye mivutano ya mara kwa mara kati ya abiria na wachuuzi hao ni Nyashishi-Kisesa kupitia Natta, Buzuruga, Nyakato, Igoma na Kishiri.

Sauda Jabir, mmoja wa abiria aliyezungumza na Mwananchi ndani ya daladala ya Nyashishi-Kishiri anashauri wachuuzi wa dagaa kubadilisha nguo wanapotoka majini kabla ya kupanda daladala kuondoa kero hiyo.

“Utafutaji hauna kanuni, kila mmoja anapata riziki kwa njia na shughuli yake, lakini si sawa kuwa kero kwa wengine. Kina mama hawa wawe wanabadilisha nguo zilizolowa kabla ya kupanda daladala,” anashauri Sauda.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Hussein Zunda akisema abiria ndani ya daladala huketi au husimama kwa kugusana, hivyo kitendo cha wachuuzi wa dagaa kuwapaka shombo abiria wengine ni kero.


Wavuvi waruka kiunzi

Wakati wachuuzi wakiwarushia lawama wavuvi kwa kuegesha mitumbwi kwenye kina kirefu cha maji, mvuvi Musa Hamidu anayefanya shughuli zake mwalo wa Mswahili anasema wanalazimika kuegesha boti kwenye kina kirefu kuepuka kukwama kwenye mchanga kwa sababu eneo hilo halina gati.


Wadau wa uvuvi

Katibu wa Chama cha Wavuvi Tanzania, Jephta Machandaro anataja mialo mingi ya uvuvi kutokuwa na magati ya kushushia mizigo kuwa miongoni mwa changamoto wanazokumbana nazo wavuvi na wafanyabiashara wa bidhaa za samaki, licha ya halmashauri kutoza ushuru katika maeneo hayo.

“Hakuna gati kwa zaidi ya asilimia 90 ya mialo yote ya uvuvi nchini. Wafanyabiashara, wachuuzi na wakati mwingine wateja wa kitoweo hulazimika kuingia hadi hatua 10 ndani ya maji kufuata bidhaa,’’ anasema Machandaro.

Anasema kwa jiji la Mwanza inayoundwa na Wilaya za Nyamagana na Ilemela, ni mialo ya Kirumba na Kayenze ndio pekee yenye magati.

“Mialo ya Luchelele, Mswahili, Bwiru, Kayenze ndogo, Igombe, Mihama, Kibandani, Kabangaja, TX na Swea, kwa kutaja kwa uchache haina gati, hali inayowalazimisha wachuuzi kuingia majini kufuata bidhaa,’’ anasema Machandaro

Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Maeneo ya Fukwe (BMU) mwalo wa Mkuyuni, Robert Charles anasema uongozi wa BMU kwa kushirikiana na wadau umeanza jitihada za kuhakikisha gati inajengwa kwenye mwalo huo.

Nyongeza na Kelvin Michael