Stendi ya Mwenge kuingiza Sh1.5 bilioni kwa mwezi

Mwonekano wa stendi mpya ya Mwenge. Picha na Nasra Abdallah

Muktasari:

  • Stendi hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2020, imegharimu Sh10 bilioni, fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Kinondoni.

Dar es Salaam. Wakati stendi mpya ya Mwenge ikitarajiwa kufunguliwa ndani ya mwezi huu, Manispaa ya Kinondoni imesema inatarajia kukusanya Sh1.5 bilioni kwa mwezi.

Stendi hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2020, imegharimu Sh10 bilioni, fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Kinondoni.

Akizungumza na Mwananchi leo Januari 8, 2024, Ofisa biashara wa Manispaa ya Kinondoni, Shedrack Mbonike, amesema katika uendeshaji wa mradi huo kuna utoaji huduma ya usafiri na ya pili ni ya ukodishaji fremu.

Katika fremu amesema wamezitengeneza kwa ajili ya wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo ambapo kodi yake inaanzia Sh299, 000 hadi Sh4 milioni kwa mwezi.

Kwa kutambua wafanyabiashara wadogo, amesema wamewajengea vibanda vyao vinavyiofika 38.

“Hata hivyo kwa idadi ya wafanyabiashara 15,000 walioondoka kupisha ujenzi, sio rahisi uwarudishe wote na kwa kuwa hela iliyotumika kujenga stendi ile ni ya Serikali, lazima irudi ndio maana tukaruhusu na wawekezaji wengine wakubwa kuja kupanga fremu hizo zikiwemo benki,” amefafanua Mbonike.

Kuhusu kuanza kufanya kazi kwa stendi hiyo, Mbonike amesema ni kabla ya kuisha mwezi huu Januari kwa kuwa kwa upande wao asilimia kubwa ya ujenzi imeisha na watu washakabidhiwa fremu zao.

Amesema kilichokuwa kinasubiriwa ni Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kupeleka magari kituoni hapo.

Awali wakizungumza na Mwananchi kituoni hapo leo, baadhi ya wafanyabiashara wamesema walikuwa wanaisubiri stendi hyo kwa hamu.

“Wakati stendi ilikuwa hapa, nilikuwa napata sio chini ya Sh60, 000 kwa siku, lakini tangu wameanza kuikarabati hii stendi, hakuna biashara zaidi ya kupata tu hela ya kula ambapo siku nyingine unaweza kupata Sh20, 000 ilimradi tu usikae nyumbani,” amesema Fides Thomas, mkazi wa Ubungo na mmiliki wa duka la vyakula.

Kwa upande wake Mrisho Bakari amesema hatua ilipofikia stendi hiyo kunawapa imani ya kupata walau fedha za kula japo hawajajua lini inafanya kazi.

“Kurudi stendi hapa kunatupa imani ya kufanya biashara, kwani wakati ipo kwenye ujenzi, tulikuwa tukikimbizwa mara kwa mara humu, sasa naona tunaenda kutulia na kufanya shughuli zetu kwa utulivu,” amesema Bakari.

Naye Neema Paulo, amesema kwa muda stendi ilikuwa haipo, hali ya biashara haikuwa nzuri, lakini kurejea kwake ni wazi kutakuwa na idadi kubwa ya watu wanaofika hapo kupata huduma mbalimbali na hivyo nao kusaidia kufanya biashara.

Sadick Amri, alisema licha ya stendi hiyo kurejea, lakini kilio chao kikubwa ni kutopata fremu ndani ya stendi hiyo kutokana na utaratibu uliotumika kuzipata kwa njia ya mnada.

“Wakati tunaondolewa hapa kwa ajili ya kufanyika ujenzi wa stendi, tuliahidiwa kwamba tungerudishwa, lakini imekuwa ndivyo sivyo, na sasa tumebaki kupigwa hela nyingi kwa fremu za watu binafsi kwa kulipa mamilioni ya hela.

“Kwani wakati fremu hizi za Serikali zikiwa zinakodidishwa kati ya Sh200,000 hadi Sh600,000 sisi huku tunalipa Sh1 milioni na mtu anailipa kwa mwaka iweje tushindwe kulipa hizi kama ambavyo mamlaka zimekuwa zikisema kuwa hatutaweza kulipa?” amehoji  Amri.

Ally Athuman ambaye mwananchi wa kawaida, alisema anaipongeza Serikali kwa ujenzi wa stendi hiyo ambayo ina muonekano mzuri lakini kubwa inaenda kuwarahisishia usafiri wakazi wa eneo hilo.

Hata hivyo, kwa upande wa wamiliki binafsi wa fremu zinazozunguka stendi hiyo wanaonekana nao kwenda kufaidika zaidi, ambapo kwa sasa ukodishaji wa fremu moja ni Sh1 milioni  kutoka Sh200,000 iliyokuwa ikitozwa huko nyuma na tayari nyingi zimejaa.