Tanzania ilivyong’ara Afrika mpango wa Mission 300
Muktasari:
- Serikali ya Tanzania inalenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme kwa wananchi hadi asilimia 75 ifikapo mwaka 2030, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia unafikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.
Dar es Salaam. Tanzania imeongoza miongoni mwa nchi za Afrika zinazonufaika na mpango wa Mission 300 baada ya watu milioni 7.5 kuunganishwa na huduma ya umeme kupitia mpango huo.
Hatua hiyo inatajwa kuwa kichocheo cha kuongeza kasi ya upatikanaji wa nishati nchini.
Mission 300 ni mpango wa pamoja unaotekelezwa na Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa lengo la kufikisha umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika ifikapo mwaka 2030.
Taarifa iliyotolewa na Benki ya Dunia na AfDB Juni 16, 2026 inaeleza kuwa hadi sasa zaidi ya watu milioni 50 katika nchi 40 za Afrika wameunganishwa na umeme kupitia mpango huo, ikiwa ni hatua kubwa kufikia lengo lililowekwa.
Kwa Tanzania, mafanikio hayo yanatajwa na AfDB kuwa yameifanya nchi hiyo kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu walionufaika na Mission 300, huku kasi ya usambazaji wa umeme ikiongezeka mara tano ikilinganishwa na kipindi kabla ya kuanza kwa mpango huo.
Ukuaji huo umechangiwa na ongezeko la uwekezaji katika sekta ya nishati, maboresho ya sera pamoja na utekelezaji wa haraka wa miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Akizungumzia hatua hiyo, mchambuzi wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude amesema upatikanaji wa umeme ni moja ya nguzo kuu za maendeleo kwa kuwa huongeza tija katika uzalishaji, huwezesha ukuaji wa viwanda na huchochea uwekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi.
Amesema takwimu hizo zinaonyesha Tanzania imeanza kunufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika miundombinu ya nishati katika miaka ya karibuni.
Kwa mtazamo wa maendeleo jumuishi, amesema ongezeko la upatikanaji wa umeme hususan maeneo ya vijijini huleta mapinduzi katika sekta za elimu, afya na biashara ndogo ndogo.
Wakati wananchi wanapopata umeme, gharama za uzalishaji hupungua, huduma za kijamii huboreka na fursa mpya za ajira huongezeka.
"Hii ni hatua inayoweza kusaidia kupunguza pengo la maendeleo kati ya maeneo ya mijini na vijijini na hivyo kuimarisha ustawi wa wananchi kwa ujumla," amesema.
"Aidha, nafasi ya Tanzania kuwa kinara wa mpango huo barani Afrika inaongeza imani ya taasisi za fedha za kimataifa na wawekezaji binafsi katika mazingira ya uwekezaji nchini," amesema.
Mkude amesema endapo kasi hiyo itaendelea sambamba na mageuzi ya sekta ya nishati, Tanzania inaweza kufikia lengo la kuongeza upatikanaji wa umeme kwa asilimia 75 ya wananchi ifikapo mwaka 2030, jambo litakalochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa viwanda na kufikia malengo ya maendeleo endelevu.
"Umeme si huduma ya kawaida pekee, bali ni mtaji wa maendeleo. Kila kaya au biashara inayounganishwa na umeme huongeza uwezo wa taifa kuzalisha, kuajiri na kukuza uchumi wake kwa kiwango kikubwa zaidi," amesema Mkude.
Januari 2025, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika uzinduzi wa mpango wa kitaifa wa nishati akiwa kwenye Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika jijini Dar es Salaam, alisema Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kuunganisha umeme kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Alisema utegemezi wa kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ni zaidi ya asilimia 90, hivyo katika kukabiliana na hali hiyo Tanzania imeweka Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kupandisha kiwango cha matumizi ya nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.
Mkuu huyo wa nchi alisema umeme uliokuwa unazalishwa nchini wakati huo ulikuwa megawati 3,831, huku megawati zaidi ya 2,000 zikitarajiwa kuzalishwa kupitia vyanzo mbalimbali ifikapo mwaka 2030 na kufanya uunganishaji wa umeme kufikia asilimia 72.
Ifahamike kuwa kupitia Mission 300, Serikali, taasisi za maendeleo na wawekezaji binafsi wameunganishwa katika mpango mmoja unaolenga kuongeza upatikanaji wa umeme kwa kaya, biashara na taasisi mbalimbali.
Taarifa ya AfDB inaeleza kuwa tofauti na mipango ya awali ambayo mara nyingi ilikuwa ikitekelezwa kwa njia tofauti na taasisi mbalimbali, Mission 300 imeleta uratibu wa pamoja unaosaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme.
Hadi sasa, Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika zimeelekeza karibu dola bilioni 15 (Sh trilioni 39.4) katika miradi inayohusiana na Mission 300, huku zikivutia takribani dola bilioni 4.5 (Sh trilioni 11.8) za ufadhili wa pamoja kutoka kwa washirika wengine.
Aidha, washirika mbalimbali wa maendeleo wameahidi zaidi ya Dola 7 bilioni (Sh18.4 trilioni) kusaidia sekta ya nishati Afrika.
Mbali na kuongeza miundombinu ya umeme, mpango huo pia unalenga kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya nishati kwa kupunguza changamoto zinazowakabili wawekezaji binafsi.
Kwa kutumia mifumo ya ufadhili ikiwemo ruzuku, dhamana na mikopo yenye masharti nafuu, Mission 300 inalenga kuwasaidia watoa huduma kufikisha umeme katika maeneo ambayo awali yalikuwa na gharama kubwa au changamoto za kufikika.
Katika nchi kama Nigeria, zaidi ya watu milioni 4.5 wameunganishwa na umeme kupitia miradi inayoongozwa na sekta binafsi, hali inayoonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wawekezaji katika kupanua huduma hiyo.
Kwa upande wa Kenya, watu milioni mbili wameunganishwa na umeme kupitia miradi mitatu ya Mission 300, huku Rwanda ikifikia watu milioni 2.4 kupitia miradi minne.
Nchi nyingine za Afrika Mashariki zilizonufaika na mpango huo ni Uganda iliyounganisha watu milioni 2.5, Burundi watu 265,000, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) watu 281,000 na Somalia watu 71,000. Sudan Kusini ndiyo nchi pekee ambayo bado haijarekodi mafanikio licha ya kupata ufadhili wa mradi mmoja.
Mwanzoni mwa utekelezaji wa Mission 300, zaidi ya taasisi 10 za kifedha, zikiwamo AfDB na Benki ya Dunia, ziliahidi kutoa dola za Marekani bilioni 50 kwa ajili ya kufadhili miradi ya nishati barani Afrika hadi mwaka 2030.
Hadi sasa, miradi inayotekelezwa katika nchi 23 imevutia uwekezaji wa Dola za Marekani 1.4 bilioni (Sh 3.7 trilioni) kutoka kwa wafadhili 10, huku Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) ikiongoza kwa kutoa Dola 347 milioni (Sh 912 bilioni), ikifuatiwa na AfDB iliyotoa Dola 161 milioni (Sh 423 bilioni).
Kwa sasa, nchi 30 zimeandaa mipango yao ya kitaifa ya nishati (National Energy Compacts) inayolenga kuimarisha mifumo ya nishati, kuongeza uzalishaji wa umeme wa gharama nafuu, kukuza matumizi ya nishati jadidifu na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi.
Akizungumzia hatua hiyo, Ajay Banga amesema kufikiwa kwa watu milioni 50 ni mafanikio makubwa, lakini jambo muhimu zaidi ni kasi ya utekelezaji na ushirikiano unaowezesha nchi kuunganisha watu wengi zaidi kwa muda mfupi.
“Umeme si suala la nishati pekee bali ni msingi wa kuongeza ajira, kukuza biashara, kuboresha huduma za afya, elimu na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi,” amesema.
Kwa upande wake, Sidi Ould Tah amesema hatua hiyo inapaswa kuwa mwanzo wa kuongeza kasi zaidi ili kuhakikisha Afrika inafikia lengo la kufikisha umeme kwa watu milioni 300 ifikapo mwaka 2030.