Tanzania inavyoathirika na vita Mashariki ya Kati
Muktasari:
- Waziri Kitila amesema vita ya Iran imeathiri upatikanaji wa baadhi ya bidhaa muhimu zikiwemo mafuta, mbolea, malighafi za viwandani na bidhaa za chakula katika baadhi ya masoko duniani.
Dar es Salaam. Serikali imeeleza namna Tanzania ilivyoathirika na vita inayoendelea Mashariki ya Kati baina ya Iran na Marekani inayoshirikiana na Israel huku ikiahidi kuchukua hatua za kisera kulinda uthabiti wa uchumi wa Taifa.
Hayo yamebainishwa leo Juni 11, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo wakati akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/27.
Profesa Kitila amesema vita ya Iran imeathiri minyororo ya usambazaji wa bidhaa na huduma duniani kwa kuongeza gharama za usafirishaji wa mizigo na muda wa usafirishaji. Pia, baadhi ya kampuni za usafirishaji zimebadilisha njia za usafirishaji ili kuepuka maeneo yenye migogoro hali iliyoongeza gharama za biashara ya kimataifa.
Amesema hali hiyo imeathiri upatikanaji wa baadhi ya bidhaa muhimu zikiwemo mafuta, mbolea, malighafi za viwandani na bidhaa za chakula katika baadhi ya masoko duniani.
Kwa Tanzania, amesema athari za vita hiyo zinajitokeza katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi, hususan katika sekta za nishati, uchukuzi, viwanda, biashara na kilimo.
Kwa upande wa mbolea, amesema Tanzania huagiza asilimia 30 hadi 40 ya mbolea (Urea na DAP) kutoka nchi za Ghuba (hususan Qatar). Amesema vita inayoendelea inatarajiwa kusababisha ongezeko la bei ya mbolea hali ambayo itasababisha kuongezeka kwa bei katika soko la ndani na hivyo kuathiri shughuli za kilimo kwa msimu ujao wa mwaka 2026/27.
kwa upande wa mafuta, amesema Tanzania huagiza kwa asilimia 100 bidhaa za petroli zilizosafishwa kutoka nje ya nchi (sawa na asilimia 13 ya thamani ya bidhaa zote zinazoagizwa nchini).
Ameongeza kuwa sehemu kubwa ya mafuta hayo (asilimia 60 hadi 70) huagizwa kutoka nchi za Ghuba (husuani Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, na Kuwait), India na Singapore.
“Pamoja na athari zingine, kuongezeka kwa bei za mafuta kumeongeza gharama za uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa na huduma.
“Aidha, suala hili linaweza kuiathiri sekta ya utalii inayochangia takribani dola za Marekani milioni 4,410.6 na kutoa ajira takribani milioni 1.5 kupitia ongezeko la bei ya tiketi za ndege na kuahirishwa kwa safari za ndege,” amesema.
Waziri huyo amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na migogoro ya kidunia.
Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuendelea kuimarisha usimamizi wa sera za fedha na bajeti ili kudhibiti mfumuko wa bei; kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala; kuimarisha uhifadhi wa akiba ya mafuta; pamoja na kuendelea kutafuta masoko mbadala ya bidhaa zinazouzwa nje.
Vilevile, amesema Serikali inaendelea kuhamasisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa muhimu ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje hususani mbolea na baadhi ya malighafi za viwandani.
Profesa Kitila amesisitiza kwamba jitihada zinaendelea kufanyika katika kuimarisha sekta za usafirishaji, biashara na uwekezaji ili kuongeza ustahimilivu wa uchumi wa Taifa dhidi ya mishtuko ya kiuchumi ya kimataifa.
“Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uchumi wa dunia na athari za migogoro ya kimataifa ili kuhakikisha kuwa hatua za kisera zinazochukuliwa zinaendelea kulinda uthabiti wa uchumi wa Taifa, ustawi wa wananchi na mazingira ya biashara na uwekezaji nchini,” amesema.