Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yaorodhesha hatifungani katika Soko la Hisa la London

Muktasari:

  • Hatifungani hiyo yenye thamani ya Sh262 bilioni itaiwezesha Benki ya NMB kupata fedha za muda mrefu kwa Shilingi ya Tanzania ili kuongeza utoaji wa mikopo kwa biashara ndogo sana, ndogo na za kati (MSMEs), biashara zinazoongozwa na wanawake, wakulima na wajasiriamali kote nchini.

Dar es Salaam. Tanzania imefanikiwa kuorodhesha hatifungani yake ya kwanza ya kimataifa iliyotolewa kwa Shilingi ya Tanzania na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) katika Soko la Hisa la London (LSE).

Hii inakuwa mara ya kwanza kwa hatifungani ya aina hiyo kuorodheshwa kwa Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki.

Hatifungani hiyo yenye thamani ya Sh262 bilioni itaiwezesha Benki ya NMB kupata fedha za muda mrefu kwa Shilingi ya Tanzania ili kuongeza utoaji wa mikopo kwa biashara ndogo sana, ndogo na za kati (MSMEs), biashara zinazoongozwa na wanawake, wakulima na wajasiriamali kote nchini.

Mkurugenzi Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, amesema kuorodheshwa kwa hatifungani ya Shilingi ya Tanzania katika Soko la Hisa la London (LSE) ni hatua ya kihistoria kwa sekta ya fedha nchini.

Amesema hatua hiyo inaashiria mafanikio muhimu kwa sekta ya fedha Tanzania kwa kufungua njia mpya ya uwekezaji wa kimataifa, huku ikiongeza upatikanaji wa fedha za muda mrefu kwa Shilingi ya Tanzania kwa ajili ya sekta binafsi.

“Tofauti na mikopo ya fedha za kigeni, ufadhili huu wa Shilingi ya Tanzania utaziwezesha biashara kuwekeza na kukua bila kukabiliwa na hatari ya mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni, hivyo kuimarisha ustahimilivu wa kifedha na kuchochea maendeleo endelevu ya uchumi,” amesema.

Kuorodheshwa kwa hatifungani hiyo kunakuja wakati Tanzania inaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inaweka mkazo katika ukuaji unaoongozwa na sekta binafsi, maendeleo ya viwanda, ubunifu na mageuzi endelevu ya uchumi.

“Upatikanaji wa mtaji wa muda mrefu kupitia nyenzo bunifu za masoko ya mitaji utakuwa muhimu katika kufanikisha malengo hayo ya Taifa,” amesema.

LSE ni miongoni mwa masoko makubwa ya mitaji duniani, ambalo limejijengea hadhi kama moja ya vituo vinavyoongoza kwa uorodheshaji wa hatifungani za sarafu za ndani katika masoko ya kimataifa.

“Kuorodheshwa kwa hatifungani hii kunaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoibukia kiuchumi zilizofanikiwa kupata mtaji wa kimataifa kupitia hatifungani za sarafu zao wenyewe, hatua inayoongeza hadhi ya nchi katika masoko ya fedha duniani,” amesema.

Hatua hii inatajwa kuwa muhimu katika kuiweka Tanzania kwenye ramani ya masoko ya mitaji ya kimataifa, ikiakisi kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa kimataifa katika misingi ya uchumi wa nchi, uimara wa taasisi zake za kifedha na matarajio yake ya ukuaji wa muda mrefu.

Pia, hatua hiyo inaimarisha nafasi ya NMB kama taasisi ya kifedha yenye uwezo wa kuvutia mtaji wa kimataifa kwa ajili ya kuunga mkono vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.

Naye Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema upatikanaji wa mtaji wa muda mrefu kwa Shilingi ya Tanzania kutoka soko la kimataifa ni ishara thabiti ya imani ya wawekezaji wa kimataifa katika uchumi wa Tanzania na ajenda ya mageuzi ya Serikali.

Amesema kwa kuunganisha mtaji wa kimataifa na biashara za ndani kupitia ufadhili wa muda mrefu katika Shilingi ya Tanzania, hatua hiyo inachochea ujasiriamali, uundaji wa ajira na ukuaji wa sekta binafsi.

“Sekta hizi ni nguzo muhimu katika kufanikisha azma ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kuifanya Tanzania kuwa uchumi wa dola trilioni moja wenye ushindani,” amesema.