Tanzania yauza tani 20,000 za nyama nje
Dar es Salaam. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Tanzania imeuza nje ya nchi tani 20,000 za nyama kwa kipindi cha mwaka mmoja, huku Saudi Arabia ikitajwa kinara kwa kuagiza nyama kwa wingi.
Kiwango hicho kiliuzwa kuanzia Desemba mwaka 2022 hadi Desemba 2023, kwani kuanzia Desemba 2022 hadi Juni 2023 waliunza tani 14,000, wakati tani 6,500 ziliuzwa kati ya Julai 2023 hadi Desemba 2023.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi baada ya kutembelea mnada wa Pugu Stasheni kusikiliza kero za wafanyabiashara, Ulega alisema jumla ya Sh200 bilioni (dola milioni 90) zilipatikana kutokana na biashara ya nyama na mifugo.
Alisema kwa sasa wameanza kuuza ng’ombe kwa mfumo wa makasha na hali hiyo imerahisisha na kuondoa kero kwa wafanyabiashara tofauti na ilivyokuwa zamani wakiuza kwa kilo.
“Mwaka 2023 takwimu zinasema wafanyabiashara wa mifugo na ufugaji wamefanya kazi nzuri, jumla ya ng’ombe milioni 2.2 waliuziana wenyewe kwa wenyewe.
“Biashara ya kuuziana mbuzi na kondoo milioni 2.1 imefanyika na biashara hii imeweka jumla Sh1.74 trilioni. Hii inaonyesha unyeti na ukubwa wa biashara hii,” alisema.
Kwa upande wao wafanyabiashara wa mnada wa Pugu walieleza magumu wanayopitia kwa Serikali katika kutekeleza shughuli zao, ikiwemo kukosekana kwa huduma za msingi kama maji na barabara inayofikika eneo hilo.
Walisema mnada huo unategemewa na unahudumia wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam na unaingiza ng’ombe 1,300 kwa siku na wanachangia kodi kubwa kwa Serikali, jambo linalowashangaza kuona huduma za msingi hazizingatiwi.