TCAA, Uhamiaji waingia makubaliano kubadilishana taarifa kidijitali
Muktasari:
- Taasisi hizo mbili zimeingia makubaliano hayo ya kutekeleza majukumu yao kidijitali ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi na wageni kwa weledi na haraka zaidi. Pia kusaidia ukusanyaji takwimu za wageni wanaoingia nchini.
Dodoma. Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na Idara ya Uhamiaji wametiliana saini makubaliano ya mpango wa kubadilishana taarifa kwa njia ya kidijitali kwa lengo la kuboresha utendaji.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama, kuongeza ufanisi wa huduma na kusaidia ukusanyaji wa takwimu sahihi hususan katika sekta ya utalii.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo Mei 27, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Salim Msangi na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala, katika makao makuu ya Idara ya Uhamiaji jijini Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Msangi amesema, “mpango huu umekuja katika wakati muafaka ambapo dunia inazidi kukumbatia teknolojia ya kisasa.”
“Utaongeza ufanisi wa operesheni zetu, kuimarisha usalama wa anga na kusaidia udhibiti bora wa wageni wanaoingia na kutoka nchini kupitia viwanja vya ndege,”amesema Msangi.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali Makakala ameeleza kuwa Idara ya Uhamiaji itaendelea kushirikiana kwa karibu na TCAA kuhakikisha taarifa za abiria na safari za anga zinawasilishwa kwa wakati na kwa usahihi.
“Huu ni mwendelezo wa ushirikiano mzuri ambao tayari upo kati ya taasisi zetu. Tunaamini ushirikiano huu wa kidijitali utatuwezesha kuhudumia wananchi na wageni kwa weledi na haraka zaidi,”amesema.
Makubaliano haya pia yanatajwa kuwa chachu ya kuboresha ukusanyaji wa takwimu za wageni wanaoingia nchini, jambo litakalosaidia katika kupanga mikakati bora ya kukuza sekta ya utalii na uchumi wa nchi kwa ujumla.
“Hatua hii ni utekelezaji wa maelekezo ya mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliyesisitiza umuhimu wa taasisi za umma kushirikiana kwa karibu kupitia mifumo inayosomana ili kuongeza tija, kupunguza urasimu na kuboresha huduma kwa wananchi,”amesema Dk Makakala.