TCAA yaingilia kati ndege iliyozama baharini

Muktasari:
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imesema itachukua hatua za kisheria endapo itabaini kuna makosa ya kibinadamu, yaliyosababisha ajali ya ndege nchini Comoro.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imesema itachukua hatua za kisheria endapo itabaini kuna makosa ya kibinadamu, yaliyosababisha ajali ya ndege nchini Comoro.
Siku tatu zilizopita, ndege ndogo aina ya Cessna Caravan 5HMZA ikiwa na abiria 14 wakiwamo marubani wawili wa Tanzania ilipotea katika rada kilometa 2.5 kabla ya kutua katika mji wa Fomboni, uliopo kisiwa cha Moheli ikitokea makao makuu ya kisiwa cha Moroni.
Ndege hiyo ilipata ajali ikiwa chini ya kampuni ya Airline AB Aviation ya Comoro, baada ya kuikodisha kutoka kampuni ya Fly Zanzibar na ilikuwa imeshatimiza takribani wiki moja tangu ianze kazi huko.
Juzi Mazrui Mohammed, mmiliki wa kampuni ya Fly Zanzibar Limited, alidai sababu za ajali ni mabadiliko ya hali ya hewa visiwani humo.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari akisema jana kuwa mamlaka kwa kushirikiana na mamlaka ya anga nchini Comoro inafanya uchunguzi.
“Ni kweli ndege ilisajiliwa Tanzania na ilikodishwa huko, sasa tunashirikiana kwa ukaribu na mamlaka ya usafiri wa anga ya huko kufanya uchunguzi, sisi tutatuma watalaamu wetu Comoro kutoa ushirikiano, itategemeana na ugumu wa kazi kabla ya kutoa ripoti ya uchunguzi wake,” alisema Johari.
“Ajali za ndege ni mara chache sana, sasa kama kuna makosa yalifanyika hatua zitachukuliwa kisheria. ”alifafanua alipoulizwa hatua gani zitachukuliwa endapo kuna makosa ya kibinadamu.
Wazalishaji wa ndege hizo, kampuni ya Textron Aviation kupitia tovuti yao wanasema ndege hiyo inatakiwa kubeba abiria kati ya 10 hadi 14. Pia inatakiwa kubeba mzigo usiozidi kilo 1,500.
Majonzi
Hali ya majonzi imeendelea kutawala, baada ya Mazrui kupitia taarifa ya habari ya ITV kudai ajali hiyo haijapoteza marubani tu ila sehemu ya familia yake.
“Huyu rubani mmoja mimi ni mwanafamilia wake, ni mtoto wetu na huyu mwingine tumeshawajulisha wazee wake wakasema kuna wanafamilia watatu watakwenda katika msafara,” alisema Mazrui juzi kabla ya kuelekea Comoro.