Ndege yazama Bahari ya Hindi, 14 watafutwa

Muktasari:
Baada ya kupotea kwenye rada mawasiliano nayo yalikatika, hivyo wamiliki wakaanza kuitafuta maharini ambako mabaki kadhaa ya ndege yamepatikana.
Dar es Salaam. Watu 14 wakiwemo marubani wawili wanaodaiwa ni raia wa Tanzania hawajulikani walipo baada ya ndege ya Kampuni ya Fly Zanzibar kudondoka katika Bahari ya Hindi.
Ndege hiyo aina ya Cessna Caravan 5HMZA ilikuwa inatoka makao makuu ya Kisiwa cha Moroni kuelekea mji wa Fomboni uliopo Kisiwa cha Moheli, vyote vikiwa ni sehemu ya Comoro.
Marubani waliopotea katika ajali hiyo ni Adili Sultani na Ashraf Abdallah Juma ambao amekuwa marubani wa ndege hiyo kwa wiki moja, chini ya Kampuni ya Airline AB Aviation ya Comoro, tangu ilipoingia mkataba wa kuikodi kutoka Fly Zanzibar.
Jana katika mitandao ya kijamii zilikuwa zikisambaa picha zinazodaiwa mabaki ya ndege hiyo yaliyokuwa yanakusanywa katika Bahari ya Hindi.
Emmanuel Buhohela, mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema “taarifa hizo tumeziona katika mitandao pia, kwa sasa tunaendelea kufuatilia kwa karibu na balozi wetu kule Comoro, tutatoa taarifa baadaye.”
Captain Mazrui Mohammed, mmiliki wa Kampuni ya Fly Zanzibar Limited aliliambia Mwananchi jana kuwa, mabadiliko ya hali ya hewa ndiyo yalisababisha ajali ya ndege hiyo juzi saa 6:40 mchana.
Alisema juhudi za kuwatafuta abiria na marubani hao zinaendelea hadi jana, huku Serikali ya Comoro ikifuatilia kwa karibu.
“Ni kweli ajali imetokea, ndege ilipoteza mawasiliano kama saa sita na nusu mchana katika kisiwa cha Moheli. Kilichosababisha ni hali ya hewa ilibadilika, maeneo ya kule hali ya hewa inaweza kubadilika wakati wowote, hakuna hata mmoja aliyepatikana. Ndege imezama yote baharini.
“Tuliangalia track system yetu (mfumo wa kufuatilia ndege angani), tukaona imekata katikati kabla ya kutua uwanja wa ndege, tukapiga simu hawapokei ndio tukapata wasiwasi. Tukaanza kuitafuta baadaye kama saa 11 hivi kuna baadhi ya vitu vimeonekana kuelea juu, mabaki ya ndege na mabegi ya abiria.”
Alisema Kampuni ya Fly Zanzibar inamiliki ndege sita, ikiwamo hiyo aliyokuwa imeikodishwa nchini Comoro.
“Lakini ndege hiyo pekee tulikuwa tumeikodisha na ilikuwa chini ya Kampuni ya AB Aviation ya huko Comoro,” alisema.
Kwa mujibu wa Mazrui, kampuni yake huendesha shughuli za usafirishaji wa abiria kutoka Uwanja wa Ndege ya Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA) kwenda nchi za Afrika Mashariki.
Uraia wa abiria
Wakati Mazrui akieleza kutofahamu uraia wa abiria wengine 12, isipokuwa marubani wawili aliodai ni Watanzania, Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) limenukuu taarifa za Serikali ya Comoro ikisema abiria 12 walikuwa ni raia wa nchi hiyo na wawili ni wa Tanzania.
Kuhusu hatua za kiuchunguzi wa ndege hiyo iliyosajiliwa Tanzania na kupata ajali Comoro, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari aliomba atafutwe baadaye akidai yupo katika mkutano.
“Nipo kwenye mkutano kuna ajali imetokea, tafadhari,” alisema bila kueleza ni ajali gani.
Kwa mujibu wa AFP, AB Aviation ilisema ndege hiyo ndogo aina ya Cessna ilitoweka kwenye rada ikiwa takribani kilometa 2.5 kabla ya kufika ilipokuwa inaelekea, Fomboni, katika kisiwa cha Moheli.
“Shughuli za kuitafuta ndege na miili zimeshaanza katika maeneo ya pwani ya Djoiezi.
Ofisa mwandamizi wa polisi visiwani Comoro, Abdel-Kader Mohamed alisema wameshatoa boti tatu za mwendokasi kuelekea eneo ajali hiyo.
“Japokuwa bado hatujapata milli lakini matumaini yapo,” alisema.
“Sina matumaini kabisa, kuanzia kesho (leo) tunakwenda kuanza maombolezo ya msiba wa dada yangu,” Idi Boina (55) aliliambia Shirika la AFP mjini Moroni.
Kwa mujibu wa Shirika la utangazaji la Al-Jazeera, Tukio hilo limekumbusha na Novemba mwaka 2012, pale abiria 29 waliponusurika katika ajali ya ndege ya Brazil iliyoanguka dakika chache baada ya kuondoka Comoro.