TEF yatoa kongole uwekezaji kiwanda cha nyama

Morogoro. Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF limepongeza uwekezaji mkubwa uliofanywa na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kujenga Kiwanda cha Nyama cha Nguru Hills ambacho kina uwezo wa kuchinja ng'ombe 100 kwa siku.

 Pongezi hizo zimetolewa leo na mwenyekiti wa jukwaa hilo Deodatus Balile baada ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ambao ni wanachama wa TEF kutembelea kiwanda hicho cha Nguru hills kuangalia utendaji kazi wa kiwanda ambacho kilizinduliwa mwaka jana.

Balile alisema alisema kuwa kutokana na uwekezaji huo wao kama wahariri wameridhishwa na kwamba mbali ya kutoa soko la mifugo kwa wafugaji wanaozunguka kiwanda hicho lakini pia kimeweza kuzalisha ajira.

Hivyo Balile ameshauri uongozi wa PSSSF kutunza uwekezaji huo kwa maslahi mapana ya nchi na kuwasihi wafanyakazi kuwa waaminifu na waadilifu katika kazi zao.

"Mara kadhaa tumekuwa tukishuhudia uwekezaji kama huu katika maeneo mbalimbali lakini baada ya muda mfupi unaanza kulegalega kutokana na kukosekana kwa uaminifu na utunzaji na hivyo kubaki historia, tusikubali kuharibu uwekezaji huu, wafanyakazi msiwe na tabia ya udokozi na wizi," amesema Balile.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi Meneja uendeshaji wa kiwanda hicho Eric Cormack amesema kuwa uzalishaji wa kiwanda hicho kwa sasa umefikia asilimia 12. Hata hivyo baada ya oda ya kupeleka nyama nchi za Uarabuni uzalishaji huo utaongezeka hadi kufikia asilimia 60. 

Amesema kuwa tangu kilipozinduliwa mwezi Desemba mwaka jana hadi sasa tayari kimezalisha na kuuza nyama tani zaidi ya 150 zenye thamani ya Sh1.59 Bilioni hasa kwenye soko la ndani, huku kiasi kikubwa cha nyama mbuzi ikiuzwa nchini Qatar wakati michuano ya Kombe la Dunia.

Akieleza utaratibu wa kiwanda kiwanda hicho katika kununua mifugo, meneja huyo amesema kuwa ng'ombe anatakiwa awe na umri usiopungua miaka mitano na kuwa na uzito usiopungua kilo 215 ili baada ya kunenepeshwa aweze kufikia kilo 390.

Kwa upande wake Meneja Uwekezaji PSSSF, Helman Goodluck amesema mfuko huo katika uwekezaji wake hasa mwenye viwanda umesaidia upatikanaji wa ajira.