TMRC yatoa mikopo ya nyumba ya Sh500 bilioni

Muktasari:

  • Kampuni ya Mikopo ya Nyumba Tanzania (TMRC), imetoa mikopo ya nyumba yenye thamani ya Sh500 bilioni kutoka Sh6 bilioni kipindi inaanza kutoa mikopo hiyo mwaka 2010.

Dar es Salaam. Kampuni ya Mikopo ya Nyumba Tanzania (TMRC), imetoa mikopo ya nyumba yenye thamani ya Sh500 bilioni kutoka Sh6 bilioni kipindi inaanza kutoa mikopo hiyo mwaka 2010.

Hayo yamesema na Mkurugenzi Mtendaji wa TMRC, Oscar Mgaya, wakati wa hafla kumpokea mwekezaji mpya wa hisa, ambao ni benki ya Mwanga Hakika (MHB).

TMRC inajihusisha na utoaji wa mikopo ya nyumba ya muda mrefu kwa mabenki na taasisi za fedha, kwa kuzikopesha kwa ajili ya kutoa mikopo ya nyumba kwa wateja wao mmojammoja.

Mgaya amesema fedha hizo zimetolewa ndani ya kipindi cha 2010 kwa mabenki kukopesha kwa wateja wao na mpaka sasa kuna taasisi za fedha 31 kutoka tatu walizoanza nazo na kueleza kuwa wanaendelea kukuza soko hilo.

“Kuwepo kwa idadi hii kubwa ya benki imesaidia kushusha riba katika mikopo hiyo ambayo inaanzia asilimia 13 mpaka 18 na kufanya kuwa soko la ushindani ambalo mwisho wa siku linamnufaisha mteja,”alisema Mkurugenzi huyo.

Kuhusu kujiunga kwa benki ya MHB, Mgaya alisema inaongeza mwanahisa na mwanachama wa 18 kwa TMRC, ambayo imeweza kuwekeza kiasi cha Sh500 milioni.

Pamoja na malengo mengine alisema wanafikiria kuongeza muda wa kulipa marejesho muda mrefu, ili kumrahisishia mteja kwani mingi ilikuwa ni miaka mitano lakini wao kwa sasa wanafanya miaka 15 hadi 25.

Kwa upande wake, Mkuu wa kitengo cha wateja wa kati na wadogo, wa benki ya  ya Mwanga, Hamis Chimwaga , alisema kujiunga kwao TMRC, wanapata manufaa  makubwa mawili mojawapo ikiwa kupata ujuzi wa kwenda kutoa mikopo ya makazi, na jingine kunufaika na mkopo ambao TMRC inatoa kwa benki.

Aidha alisema wapo tayari kuwahudumia waateja wao ikiwemo kuingia makubalinao na wajenzi wa nyumba kumjengea mteja nyumba vile anavyotaka kutoka kwenye msingi hadi kumaliza.