CRDB: Dhamana ya mkopo si lazima iwe nyumba

Meneja Mwandamizi wa Biashara wa Benki ya CRDB, Agness  Kisinini akizungumza katika kongamano la wajasiriamali wadogo na wakati lililoandaliwa na =Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa udhamini wa Ashton, Benki ya CRDB, Kampuni ya Usafirishaji DHL, Benki ya Stanbic, Benki ya NMB, Clouds Media na Ukumbi wa mikutano wa Dome.

Muktasari:

  • Wakati wafanyabiashara wengi wakilia kukosa dhamana ili waweze kupata mikopo katika Taasisi za kifedha, Benki ya CRDB imesema dhamana ni suala mtambuka.

Dar es Salaam. Meneja Mwandamizi wa Biashara wa Benki ya CRDB, Agness  Kisinini amesema dhamana ni suala mtambuka katika utoaji mikopo na si kwa wafanyabishara wadogo tu bali watu wote.

Amesema si lazima dhamana iwe nyumba jambo la msingi ni mkopaji kuzungumza na maofisa wa benki wanaoshughulika kwenye eneo hilo kuangalia kama anazo sifa za kukopesheka ikiwemo dhamana inatosha kufikia kiasi cha fedha anachotaka kuchukua.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Aprili 27, 2023 katika kongamano la Wafanyabiashara wachanga, wadogo na Kati (MSMEs), lililoandaliwa na Mwananchi Communications Limited na kukutanisha wadau ili kujadili nini kifanyike kuwawezesha kufanya biashara zao kwa ufanisi.

Amesema ugumu wa dhamana hutokana na msukumo wa wafanyabiashara wengi ambapo akili zao huwa katika kukuza biashara na wengine huwa na biashara zinazofanya vizuri lakini kwenye dhamana anakuwa hajaweka nguvu.

"CRDB tumelitambua hilo na kuangalia dhamana upande wa wanawake na wateja wa kawaida. Kwa upande wa wanawake tumekuja na Malkia akaunti ambayo itamsaidia mwanamke kufikia malengo yake” amesema.

Amesema akaunti hiyo humuwezesha mtu kuweka kidogokidogo na baada ya muda anafikia anachotaka na hiyo inamsaidia kutengeneza dhamana katika mfumo wa fedha taslimu.

Kisinini amesema dhamana si lazima iwe nyumba bali zipo za aina nyingi ikiwemo fedha inayoweza kumfanya mtu apate mikopo kwa haraka na riba ya chini kwa sababu tayari anayo fedha pesa inayopunguza hasara kwa benki.

"Mtu anapotoza riba anaangalia na hasara anayoweza kupata, kuwa huyu mtu asipofanya vizuri na asipolipa tukauza hii dhamana tutauza haraka au itatusumbua? Sasa kwa upande wa fedha haina hasara ndiyo maana riba yake inakuwa chini," amesema Agness.

Amesema kwa upande wa CRDB, wateja wadogo ni wale ambao mzunguko wao kwa mwaka unaanzia Sh100,000 hadi Sh250 milioni.

"Katika utoaji mkopo huyu anaweza kupata hadi Sh50 milioni na zaidi ya mikopo wametengenezewa akaunti ambazo wakizitumia vizuri zinaweza kuwasaidia kupata mitaji kwa sababu wakiwa na nidhamu ya kuweka fedha baada ya muda anapata mtaji  na kufanya wanachotaka kupita akaunti ya hodari," amesema Agness.

Amesema akaunti hiyo imeondoa makato yote isipokuwa ya kiserikali jambo linaloweza kuwafanya kuweka fedha hadi mwaka mmoja bila kukatwa.

"Inaweza kuwa kama kibubu kinachomsaidia kutunza fedha zake zisizokatwa na uhakika kwa sababu kama tupo kwenye kundi tunaweka mmoja mmoja mwenzangu anaweza kutumia ile fedha na kuna siku naihitaji nikaikosa lakini kwa kupitia akaunti hii nina uhakika na kile ninachokifanya,”amesema.

Kongamano hilo limedhaminiwa na Ashton, Benki ya CRDB, Kampuni ya Usafirishaji DHL, Benki ya Stanbic, Benki ya NMB, Clouds Media na Ukumbi wa mikutano wa Dome.