Machumu: MCL tumedhamiria kuleta utatuzi wa kibiashara

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL), Bakari Machumu akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Wafanyabiasharaa wadogo na wa kati jijini Dar es salaam

Muktasari:

  • Wakati kukiwa na malalamiko ya kuwapo kwa urasimu na vikwazo vya kukuza biashara, Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imesema imedhamiria kuleta utatuzi wa changamoto za kibiashara nchini.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu, amesema mjadala fikirishi wa changamoto za wafanyabiashara na wajasiriamali utasaidia kuleta ufumbuzi.

Amesema MCL wameamua kuandaa kongamano la wajasiriamali (MSMEs) ili kuwezesha biashara changa za chini, ndogo na za kati kukua na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa wajasiriamali wachanga, wadogo na wa kati (MSMEs) ni asilimia 90 ya wafanyabiashara na shughuli zao zinachangia asilimia 80 ya ajira zote hususani kwa vijana na wanawake.

Machumu ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Aprili 27, 2023 jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki alipokuwa akizungumza kwenye ufunguzi wa kongamano hilo ambapo wanashirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kutafuta ufumbuzi wa changamoto kwa wajasiriamali.

"Leo tumekuja tena ambapo tunalikutanisha Taifa pamoja, wadau mbalimbali tukae pamoja na kuangalia changamoto zetu ni zipi na kuwa na mjadala fikirishi lakini unaoleta ufumbuzi wa yale yanayotukabili.

"Nia yetu kama MCL ni kujipambanua kwenda mbele zaidi ya kuwa chombo cha habari na kuondoka katika kile kwamba, Serikali itafanya kila kitu badala yake tuchukue jukumu la kuleta utatuzi badala ya kuwa mabingwa wa kulalamika au kulielezea tatizo. Tusishindane kulielezea tatizo lakini tufanye jitihada za kutatua tatizo. Ndiyo dhima nzima ya kwanini tunafanya kongamano hili la leo," amesema Machumu.

Kongamano hili linaendelea katika ukumbi wa wa The Dome, uliopo Masaki jijini Dar es Salaam, limedhaminiwa na Benki ya CRDB, Kampuni ya usafirishaji ya DHL, Benki ya Stanbic, Benki ya NMB, Clouds Media, Kampuni ya matangazo ya Ashton na ukumbi wa mikutano wa The Dome.

MCL ni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, watoa huduma za usafirishaji na uchapishaji na waendesha makongamano, mijadala jadidifu na sekta ya tafiti kupitia Habari Hub.