Vikundi vya wanawake wajasiriamali vyapewa msaada wa Sh4 milioni Musoma

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Agnes Marwa (wapili kulia) akiwa na baadhi ya wakina mama baada ya kuwakabidhi msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo viti vya kukodisha kwaajili ya kuboresha vikundi vyao vya kijasiriamali vinavyoundwa na wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Musoma. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Vikundi vya ufugaji kuku, upambaji na ufundi cherehani vimepewa msaada wa vyerehani, viti vya kukodisha na vifaranga vya kuku vyenye thamani ya Sh4 milioni ili kuboresha biashara zao na kujiinua kiuchumi.

Musoma. Vikundi vitatu vya wanawake wajasiriamali mkoani Mara vimepewa msaada wa vyerehani, viti vya kukodisha na vifaranga vya kuku vyenye thamani ya Sh4 milioni ili kuboresha shuguli zao.

Akikabidhi msaada huo kwa wajasiriamali hao leo Jumanne Aprili 11, 2023 Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Agnes Marwa amesema utasaidia wanawake hao kuweza kujiimarisha kiuchumi na kimaendeleo.

Amesema baada ya kuwasisitiza kuanzisha vikundi, sasa ni muda wa kuwawezesha ili waweze kuwa na mitaji ya kutosha na kuzalisha kulingana na uhitahiji kwenye  soko na mwisho wa siku wawe na uchumi imara.

 “Mara nyingi tunawakumbuka hawa wanawake nyakati za kampeni tu sasa tuseme basi, wanawake wanatakiwa kuwa na uchumi imara na hii itawezekana kupitia njia mbalimbali ikiwemo vikundi vya kijasiriamali, kinachotakiwa ni kuwawezesha, 

“Hakuna sababu ya kusubiri hadi wakati wa uchaguzi ndipo tuwape hela ni lazima tuwawezeshe hawa wakinamama wawe na vyanzo imara vya mapato hata wakati wa uchaguzi ukifika wanakuwa imara na wenye uwezo wa kuchagua viongozi bora na sio wale wanaotokana na hela,” amesema Agnes

Mwenyekiti wa kikundi cha wafuga kuku, Anifa Webi alimshukuru mbunge huyo akidai msaada huo utaondoa  baadhi ya changamoto zinazowakabili katika vikundi vyao ikiwemo ya mtaji.

“Tayari tumeanzisha vikundi lakini kuna mapungufu kadhaa ikiwemo mitaji sasa huu msaada tuliopata ni shemeu ya mtaji na tunaahidi  kuwa hii ni chachu ya kufanya vizuri zaidi,” amesema 

Mwenyekiti wa kikundi cha washonaji,  Kazege Ochola amesema kupitia msada huo kikundi chake kinakwenda kupanua uzalishaji wake hali ambayo itaongeza kipato cha kikundi.

“Tunataka kutoa huduma ya ushonaji ndani na nje ya Musoma na huu msaada ni mojawapo ya kichocheo cha kufikia malengo yetu, niwaombe wanasiasa wengine waige mfano huu ambao unalenga kumuinua mwanamke,” amesema 

Katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT) Angel Simwanza amesema umoja huo umeamua kuanzisha vikundi vya wanawake ili waweze kuwezeshwa kiuchumi kutokana na changamoto mbalimbali walizonazo.

“Bila uchumi imara hakuna siasa kwahiyo uwepo wa vikundi hivi utapelekea chama chetu kufanya vizuri kwenye siasa kwasababu hivi vikundi vinakuja na suluhisho la mitaji kwa wajasiriamali wadogo,” amesema