Prime
Undani soko la nyama choma la Kumbilamoto Dar

Muktasari:
- Mei 25, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa alizindua soko la kisasa la nyama choma la Kumbilamoto lililopo Vingunguti jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Je, umewahi kusikia kuhusu soko la nyama choma la Kumbilamoto? Mie nimesikia habari zake kwa watu kadhaa, nikaweka mpango wa kuandaa mtoko wa kwenda kula nyama choma, mwishoni mwa wiki.
Jana Jumapili Julai 6, 2025 siku ya mapumziko, natoka 'home' kwenda kula nyama choma-Vingunguti.
Ndio, Vingunguti. Machinjioni. Nyama za kila aina zinapatikana, kuanzia maini, bandama, ashua za mbuzi na ng'ombe, utumbo, kichwa, na steki za kawaida.
Hapa tumekutana watu wa hali mbalimbali, kuanzia walala hoi na wenye vipato vya kati, wote tunataka kuonja ladha ya nyama choma katika soko hili linalomilikiwa na halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Huna haja ya kuhofia kipato chako, hapa nyama inaanzia 'buku' na kuendelea, kama una kipato cha kutosha, basi unachoma 'mguu wa mbuzi'.
Ukiacha masoko maarufu kwa nyama choma, kuanzia pale Pugu mnadani, Mkata (Handeni), Kwa Morombo jijini Arusha, Mnadani, jijini Dodoma, soko hili pia linaingia katika ramani kwenye suala la nyama choma hasa kwa kujengewa miundombinu mizuri na kulifanya kuwa rasmi ukilinganisha na mengine.
"Braza, kaka pale, huyu mama atakuletea nyama," ananiambia mchoma nyama. Mara anadakia na mama lishe: "Kaka, ugali dona au sembe?" Basi, nilipomjibu, nikaongozwa hadi sehemu ya kukaa.
Wakati nikisubiri "mguu wa mbuzi" uive, nimetembea kuangalia miundombinu ya soko hili la nyama choma, nimeona lina choo cha kisasa, ukifika unakaribishwa na maandishi: "Haja ndogo Sh200, haja kubwa Sh300, kuoga Sh700."
Eneo hili lina fremu 36 ambazo zimekwenda urefu wa kama mita 100. Wamepangishwa wafanyabiashara tofautitofauti hasa mawakala wa miamala ya simu, vioski vya pombe na mama ntilie.
Mbele vya fremu hizo kuna nafasi kubwa inayotumiwa na wafanyabiashara wa vinywaji kama eneo la kukaa wateja wanaokunywa. Kila mmoja amepanga viti vyake na ana wateja wake.

Wafanyabiashara hapa wanategemeana. Ukinunua nyama choma, wapo wanawake wanaouza ugali, wanakudaka ili nao wauze, kisha utakwenda kukaa ili kupata huduma uliyoagiza.
Wanaouza nyama choma hawana sehemu za kukaa, wala wahudumu, bali wanaouza vinywaji na mama ntilie ndiyo wana viti vya kukaa wateja. Kwa hiyo, ukija kula nyama, aidha ule juu kwa juu ikiwa motoni, au ukae kwenye viti ununue na kinywaji au chakula kwa aliyeweka viti vyake.
Pia, ukiletewa nyama choma na wanaouza ugali, ukakaa kwa muuza vinywaji, nao watataka ununue kwao ili wakuhudumie ukiwa umekaa hapo utakapo. Kwa hiyo, kila biashara inamtegemea mwingine na wote wanajuana.
Mbele ya soko kuna barabara, na pembezoni kuna vijana wanaochoma nyama na upande mwingine ni eneo dogo la maegesho ya magari.
Basi, nikarudi kukaa. Nikaanza kupiga stori na Mama Debo aliyejitambulisha kwa jina la Sophia Dominic, muuzaji wa vinywaji aliyenihudumia.
Anasema soko hili linafanya kazi kwa saa 24 na muda wote wateja wapo na usiku watu ni wengi kuliko mchana. Hivyo, wafanyabiashara wamejiwekea utaratibu wa kupokezana, mmoja akienda kupumzika, anamuacha mtu kwenye biashara yake.
"Leo nimeingia asubuhi, nitaondoka saa usiku. Leo sikeshi, napumzika, nitakesha kesho," anasema mwanamke huyo.
Anasema soko hili linawasaidia kwa sababu mazingira ni mazuri na wanapata wateja wa uhakika kwa sababu watu wengi wanapenda kwenda kula nyama choma na kunywa pombe.
Said Mrisho ni kijana anayechoma nyama, anasema wateja wao wakubwa ni watu wa chini, ndiyo maana wanauza nyama kwa bei ya chini ili wapate wateja muda wote.
"Hapa wateja wetu wengi ni wa kawaida, ndiyo maana unaona nyama za buku buku, lakini ukitaka ubavu wa mbuzi au mguu, unapata kwa oda," amesema kijana huyo.
Upande mmoja wa soko hili umefungwa feni na zinafanya kazi muda wote. Upande wa pili hauna feni zilizofungwa, lakini watu wanaendelea na starehe zao huku wengine wakiendelea na biashara zao.
Bodaboda na bajaji pia hawako nyuma, wanategemea wateja wanaotoka katika soko hilo. Wanasema biashara imechangamka baada ya kujengwa kwa soko hilo.
"Pale sokoni hatuna sehemu ya kupaki boda, kwa hiyo tunakaa huku mbali kidogo. Wanajua wanapotupata, kwa hiyo wakitoka kula nyama wanatembea kudogo kuja hapa, kisha tunawapeleka wanakokwenda," amesema Patrick Mengo, mwendesha bodaboda.
Kwa upande wake, mama ntilie anayeuza chakula katika soko hili, Fausta Mwasa anasema kwa siku anauza kati ya Sh90,000 hadi Sh150,000. Anasema amekuwa akilipa ushuru wa halmashauri pamoja na tozo nyingine kama usafi.
"Wateja wangu wakubwa ni wenye fremu katika eneo hili. Pia, wanaokuja kuchoma nyama wamekuwa wakinunua ugali kwangu. Kwa hiyo, nikikesha hapa, napata hela ya kutosha kulingana na biashara yangu," anasema.

Nimezungumza na aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, anasema wazo la kubuni soko hilo alilipata nchini Namibia ambako alikwenda na kuona soko la nyama choma, hivyo akabeba wazo na kulileta hapa nchini.
"Wazo hili nililipata nchini Namibia nilipokwenda, wenzetu ni nchi ya tatu kwa kuzalisha mifugo mingi, Tanzania ni ya pili. Kwa hiyo, nikaona Soko la Nyamachoma, ndipo nikaja na wazo lile, nikakaa na mkurugenzi na wataalamu wa jiji, nikawaeleza, tukachora mchoro ule. Mheshimiwa Rais Samia akatupatia Sh729 milioni za ujenzi," anasema.
Kuhusu Manufaa ya ujenzi wa soko hilo, Kumbilamoto anasema: ”Kwanza, tumetengeneza ajira rasmi kwa watu 296 ambao ni wajasiriamali, pili mradi huo umependezesha mji na kuvutia wageni kuja Vingunguti.
"Umeongeza mzunguko wa pesa na kuzalisha ajiri mpya hususan bodaboda. Pia, umeongeza chanzo cha mapato cha halmashauri, tunatarajia kwa mwaka kukusanya Sh160 milioni," anasema Kumbilamoto ambaye pia ni alikuwa diwani wa Vingunguti.
Anasema kabla ya ujenzi wa soko hilo, hali ilikuwa mbaya na eneo hilo lilikuwa chafu. Anawaalika wananchi wengine kutembelea eneo hilo kujionea mandhari nzuri.
Soko lenyewe
Soko hilo lilizinduliwa Mei 25, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ambalo limegharimu Sh727 milioni.
Alisema soko hilo litakwenda kuwapatia ajira wananchi wengi huku akisisitiza kuendelea kulitunza ili lisiharibike kwenye kipindi kifupi.
Mchengerwa alisema kukamilika kwa soko hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akifafanua Serikali ya awamu ya sita tayari imekamilisha miradi mingi kama ilivyoahidi.
Wakati huohuo, Mchengerwa amezitaka halmashauri zote nchini kutimiza malengo zilizojiwekea ya ukusanyaji mapato ili ziweze kutekeleza miradi ya maendeleo huku akizitaka kuendelea kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo yenye tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Waziri huyo alizitaka halmashauri na mikoa yote nchini kuwapa kipaumbele makandarasi wazawa huku akitoa wito kuwachukulia hatua wanaofanya vibaya kwenye kazi wanazopewa.