Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu Profesa Manya, Waziri Tax kutochukua fomu za ubunge CCM

Muktasari:

  • Dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu za kuwania udiwani na ubunge ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), lilifunguliwa Juni 28 na kufungwa Julai 2, 2025. Profesa Shukurani Manya, Dk Stergomena Tax na Shamsi Vuai Nabodha hawakujitosa kwenye mbio hizo.

Shinyanga. Kurudi Chuo Kikuu kushika chaki na kubaki kuwa mwanachama mtiifu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ndiyo mipango waliyonayo wabunge wawili wa kuteuliwa, Profesa Shukurani Manya na Dk Stergomena Tax, ambao hawakuonekana kuchukua fomu za kuwania ubunge kama ilivyo kwa wengine.

Wawili hao, waliingia bungeni bila historia za kisiasa, Profesa Manya akitoka kuiongoza Tume ya Madini, baada ya kufundisha kitambo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Dk Tax, akitoka katika historia ya nafasi za utendaji na diplomasia.

Profesa Manya, ndiye aliyeanza kuteuliwa kuwa Mbunge na kisha Naibu Waziri wa Madini, enzi za Serikali ya awamu ya tano chini ya hayati John Magufuli, kisha Dk Tax akafuata, alipoteuliwa kuwa Mbunge na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Wawili hao, si sehemu ya makada wa CCM walioonekana katika orodha ya waliochukua fomu za kuutaka ubunge wa majimbo wala viti maalumu huku wenyewe wakifafanua sababu za kutofanya hivyo na mipango yao baada ya ubunge.


Profesa Manya

Profesa Manya aliukwaa ubunge Desemba 2020, baada ya kuteuliwa na Rais wa wakati huo, hayati John Magufuli na baadaye Desemba 11 mwaka huohuo kuapishwa na aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Uteuzi wa Profesa Manya kuwa mbunge uliambatana na uteuzi wa kushika wadhifa wa Naibu Waziri wa Madini, akichukua nafasi ya Francis Ndulane aliyekuwa ameteuliwa, lakini akishindwa kusoma kiapo kwa usahihi na hayati Magufuli, aliahidi angemteuwa mwingine.

Baada ya kuhudumu kwa miaka miwili kama Naibu Waziri wa Madini, mwaka 2022, Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan alimteua Stephen Kiruswa kushika wadhifa huo na Profesa Manya akabaki kuwa mbunge.

Licha ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kufungua pazia la uchukuaji na urejeshaji fomu hadi kulifunga Julai 2, 2025 Profesa Manya hajachukua fomu ya ubunge, kama anavyothibitisha, alipoulizwa na Mwananchi.

Kwa mujibu wa Profesa Manya, mwendo wake katika siasa ulihitimishwa Juni 27, 2025 na sasa amebaki kuwa raia kama wengine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Nilihitimisha mwendo wa siasa Juni 27, 2025 ndugu yangu. Sasa ni raia tu wa kawaida wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Asante," ameeleza.

Alipoulizwa sababu ya kufanya hivyo, Mwanazuoni huyo ambaye chimbuko lake ni ukufunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema miaka mitano ilimtosha kutumikia wadhifa huo.

Hata hivyo, amesema baada ya kuachana na siasa, mpango wake ni kurudi kushika chaki chuoni, ambayo ni kazi yake ya asili kabla ya uteuzi.

"Ndiyo kazi yangu originally (ya asili) kabla ya uteuzi," amejibu Profesa Manya alipoulizwa iwapo atarudi chuoni kushika chaki.


Dk Tax

Kama ilivyo kwa Profesa Manya, Dk Stergomena Tax naye Septemba 10, 2021 aliteuliwa kuwa mbunge kati ya nafasi 10 za Rais, ikiwa ni mwezi mmoja tangu alipomaliza muda wake katika nafasi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Uteuzi wake katika nafasi ya ubunge, uliambatana na kuteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, akimrithi hayati Elias Kwandikwa aliyefariki dunia Agosti 2, 2021.

Naye, mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu ndani ya CCM umepita na hakuchukua katika jimbo lolote na mwenyewe ameithibitishia Mwananchi.

Alipoulizwa kuhusu mpango wake baada ya kutochukua fomu, Dk Tax amesema amepanga abaki kuwa mwanachama mtiifu wa CCM.

"Nimepanga nibaki kuwa mwanachama mtiifu wa CCM na sio vinginevyo," amesema Dk Tax alipoulizwa na Mwananchi.


Kapteni Mkuchika

Kapteni George Mkuchika ni waziri mwingine ambaye hakuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya ubunge na mwenyewe alishaweka hadharani kuwa imetosha kutumikia nafasi hiyo, baada ya miaka 20 katika Jimbo la Newala mkoani Mtwara.

Mkuchika aliyewahi kuhudumu katika utumishi wa umma tangu enzi za Serikali ya awamu ya kwanza chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, nafasi yake ya mwisho ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, asiye na wizara maalumu.

Akitaja sababu za kutogombea tena ubunge, Machi 23, 2025 Mkuchika alisema uzee ni mojawapo na kwamba kabla ya kuwaambia wananchi wa jimboni mwake, alitoa taarifa kwa Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Newala.

Amesema maisha yake katika utumishi wa umma unatimiza miaka 52, kabla aliitumikia Tanu na CCM kwa miaka 10.

Baada ya ukuu wa utumishi wake ndani ya Tanu na CCM, alihamia kuwa Mkuu wa Wilaya, kisha Mkuu wa Mkoa na mwaka 2005 aligombea ubunge na kushinda jimbo la Newala.


Shamsi Nahodha

Waziri kiongozi mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha ni mwanasiasa mwingine ambaye licha ya mchakato wa uchukuaji fomu kufunguliwa, hakuchukua hadi dirisha lilipofungwa.

Hata hivyo, utumishi wake katika Bunge la 12, ulitokana na nafasi 10 za Rais, alipoteuliwa Machi mwaka 2022.

Alipoulizwa na Mwananchi, Nahodha amekiri kuwa hakuchukua fomu na hakuwa na mpango wa kuwania nafasi hiyo.

"Niliacha kugombea, kama unakumbuka hata nafasi hii niliyokuwa nayo niliteuliwa. Hivyo nilishaacha kugombea ndio maana sijachukua fomu," amesema.

Alipoulizwa mipango yake, amesema ni vigumu kuiweka hadharani kwa kuwa ni mambo yake binafsi yasiyostahili kuandikwa kwenye vyombo vya habari.

Ingawa hali iko hivyo, bado viongozi hao wana nafasi ya kurudi bungeni, kupitia nafasi 10 za Rais, kama walivyoingia katika Bunge la 12.