Ulanga: Urasimu uondolewe urasimishaji biashara

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL) John Ulanga akizungumza wakati wa Kongamano la Wafanyabiashara Wadogo na Wakati katika ukumbi wa Super Dome, Masaki  jijini Dar es salaam

Muktasari:

  • Watanzania wametakiwa kujadiliana namna bora ya kuondoa urasimu katika kurasimisha biashara ili kuwawezesha wafanyabiashara wachanga, wadogo na kati kukua

Dar es Salaam. Mwakilishi wa Mwenyekiti wa bodi ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), John Ulanga amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wachanga, wadogo na kati ni urasimu wanaokutana nao wapotaka kurasimisha biashara zao.

Ametoa kauli hiyo leo, Alhamisi Aprili 27, 2023 katika kongamano la wafanyabiashara wachanga, wadogo na kati lililoandaliwa na MCL ambalo limekutanisha wadau mbalimbali ili kujadili nini kifanyike ili kuwawezesha kufanya biashara zao kwa ufanisi.

Akizungumza katika kongamano hilo Ulanga amesema changamoto kubwa ambayo wafanyabiashara wamekuwa wakiitaja ni mtaji bila kujali utapatikana kwa njia gani ikiwemo mikopo.

"Changamoto nyingine ni namna ya kufikia masoko, pia ujuzi si tu wa kutengeneza biashara wanazosimamia bali ujuzi wa kuongoza biashara,"

Amesema changamoto nyingine inaweza kuwa ya kisera, kikanuni kitaratibu au sheria inayoweza kusababisha urasimu hasa mtu anapotaka kutoka sekta isiyokuwa rasmi na kuwa sekta rasmi.

"Unapotaka kurasimisha unakutana na urasimu ili uweze kurasimisha ni mjadala ambao leo tutauzungumza," amesema Ulanga.

Amesema kampuni ya Mwananchi kwa kutambua umuhimu wa kampuni ndogondogo imekuwa ikiwapa nafasi huku akitolea mfano wa ‘Top 100 Midsized Enterprises’ iliyokuwa ikitambua kampuni zilizopo katika ngazi ya kati kwa sababu ya mchango mkubwa zinapokutanishwa na kampuni kubwa au ndogo.

"Ilipotokea Uviko-19 tukatetereka kwahiyo huu ni mwanzo pia wa kuanza kufikiri namna ya kurudisha kitu kinachofanana na Top 100," amesema Ulanga.

Hilo linafanyika kutokana na kutambua mchango wa kampuni ndogo na changa ambapo alieleza kuwa zaidi ya theluthi moja ya pato la Taifa linachangiwa na biashara ndogondogo ambazo zaidi ya asilimia 54 hadi 60 zinamilikiwa au kuongozwa na kinamama.

"Hivyo tunapozungumzia usawa wa kijinsia katika biashara haukwepeki,  pia asilimia 40 hadi 50 ya ajira zinatokana na biashara hizo," amesema Ulanga.

Amesema kama ilivyo moto wa Kampuni ya Mwananchi ni 'kuliwezeshaTaifa' ameeleza kuwa ni lazima kufanya kazi zinazoiwezesha Taifa.

Amesema ni vyema mjadala huo ukajikita katika kutoa suluhisho badala ya kulalamika ili kujua nini cha kufanya kwa pamoja kitakachowezesha kukuza biashara ndogo, changa na kati kwa kufanya taratibu kuwa rahisi ikiwemo za wafanyabiashara kupata mitaji.

"Hii itahusisha kwa kuwakutanisha wanaohitaji mitaji na wanaotoa mitaji.," amesema Ulanga.

Ametolea mfano kuwa kuna mfanyabiashara akipewa Sh50,000 ni mtaji wa biashara lakini wengine hutengeneza nywele ambazo hubadilisha baada ya wiki mbili au mwezi.

"Kuna mtu aliwahi kuniambia kuwa mtaji wa biashara yake ulikuwa Sh50,000 na sasa yuko katika mamilioni. Lakini huyo anayetumia Sh50,000 kusuka ukimuuliza kwanini anafanya hivyo atasema ni bora nitumie kwenye nywele zangu kuliko kumpa mtu hela atapotea na hela zangu," amesema Ulanga.

Amesema hivyo ni vyema kujenga uaminifu ili kuwakutanisha wenye mitaji na wanaohitaji huku akieleza kuwa mjadala huo ni muhimu na mzuri na utalifanya Taifa kujua nini kifanyike ili kuhakikisha kuwa mchango wa bishara changa, ndogo na kati unatambulika na kulifanya Taifa kwenda katika  kipato cha kati.

Kongamano hilo limedhaminiwa na Ashton, benki ya CRDB, Kampuni ya Usafirishaji DHL, Benki ya Stanbic, Benki ya NMB, Clouds Media na Ukumbi wa Mikutano wa Dome