Kongamano la wajasiriamali lavutia wengi

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL), Bakari Machumu akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Wafanyabiasharaa wadogo na wa kati jijini Dar es salaam

Dar es Salaam. Mamia ya wajasiriamali na wadau wa biashara changa, ndogo na kati wamekutana jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki kushiriki kongamano mahususi lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

Kongamano hilo limedhaminiwa na Benki ya CRDB, Kampuni ya usafirishaji ya DHL, Benki ya Stanbic, Benki ya NMB, Clouds Media, Kampuni na ukumbi wa mikutano wa The Dome.

Lengo la kongamano hilo ni kujadili namna ya kuwezesha biashara changa, za chini, ndogo na za kati kukua haraka.

Washiriki walianza kuwasili ukumbini saa mbili asubuhi na wakafanya taratibu za ukaguzi wa tiketi mlangoni na baadaye wasaidizi maalumu waliwaongoza hadi katika maeneo wanayopaswa kukaa.

Ndani ya ukumbi huo wa kisasa, kumewekwa meza za duara nyeupe ambazo wadau wa kongamano hilo waliketi kusikiliza taarifa mbalimbali huku wengine wakiangalia runinga kubwa zilizowekwa kila upande kuhakikisha aliyekaa mbali na meza kuu anaona vizuri.

Hali ya hewa ndani ya ukumbi huo wenye taa za rangi mbalimbali, paa jeupe na ukuta mweusi ilikuwa ya utulivu licha ya hali ya hewa Dar es Salaam kwa siku ya leo kuwa nyuzijoto 29.