TRA kukusanya kodi kwa wamachinga wote Kariakoo

Muktasari:

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza kuwasajili wafanyabiashara wadogo ‘wamachinga’ waliopo katika Soko Kuu la Biashara Kariakoo


Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza kuwasajili wafanyabiashara wadogo ‘wamachinga’ waliopo katika Soko Kuu la Biashara Kariakoo

Akizungumza na wanahabari leo Jumatatu Desemba 12, 2022 Meneja wa Mkoa wa Kikodi wa TRA, Alex Katundu amesema tayari machinga 5273 wameshasajiliwa ili kuingizwa kwenye mfumo wa malipo ya kodi wa makadirio.

“Usajili huu unafanyika kwa kila machinga aliyepo Kariakoo kwa sababu tulibaini baadhi ya wafanyabiashara wengine sio waaminifu, haonekani akifanya biashara ila mizigo yake anaisambaza kwa machinga ili akwepe kodi.

“Lakini tunawasajili baada ya kujiridhisha kwamba wote wanaingiza mapato zaidi ya Sh4milioni kwa mwaka, kuna mapato mengi yanapotea hivyo wataanza kulipa kodi” amesema Katundu.

Usajili huo ulioanza Februari mwaka huu, unafanyika ikiwa ni utekelezaji wa tangazo la Kamishna wa TRA la Julai mosi mwaka huu, linaloagiza kila machinga kusajiliwa eneo hilo.

Katundu amesema baada ya kusajiliwa wote watakabidhiwa mashine za EFDs kwa ajili ya kushiriki kwenye ulipaji wa kodi ya makadirio.

Kwa sasa machinga wote wataingizwa kwenye makadirio ya kiwango sifuri kabla ya Januari mwakani kuanza kuingizwa wote kwenye mfumo wa makadirio ya mapato yao halisi ya mwaka.

Pamoja na uamuzi huo, Katundu pia amezindua mkakati mwingine wa uhamasishaji wa matumizi ya EFDs katika mabango kumi wakati huu wa Sikukuu za mwisho wa mwaka.

Kikanuni, usipotoa risiti utatozwa faini kati ya Sh3milioni hadi 3.5milioni na usipodai risiti utatozwa faini kati ya Sh30,000 hadi Sh1.5milioni