TRA Tanga walivyovuka lengo la makusanyo, RC asema…
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian akizungumza na wafanyakazi wa TRA, wawakilishi wa taasisi za fedha na wafanyabiashara wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya tangu kuanzishwa kwa Mamalaka hiyo nchini. Picha na Mbonea Herman.
Muktasari:
- TRA imeongeza makusanyo ya kodi kutoka Sh531 bilioni mwaka 1996/1997 hadi Sh32 trilioni mwaka 2025/2026 kupitia matumizi ya teknolojia na maboresho ya usimamizi wa kodi.
Tanga. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga imeandika historia ya mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996, ambapo makusanyo ya kodi yameongezeka kutoka Sh531 bilioni hadi kufikia Sh32 trilioni katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Mafanikio hayo yameelezwa na Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castro John wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya mamlaka hiyo jana Jumamosi, Juni 27, 2026, akisema mageuzi ya mifumo ya ukusanyaji kodi, matumizi ya teknolojia na kuongezeka kwa ushirikiano na walipa kodi ndiyo yameifanya TRA kufikia mafanikio hayo.
Castro amesema miaka ya mwanzo ukusanyaji wa kodi ulitegemea mfumo wa mwongozo (manual), ambapo watumishi walipokea fedha taslimu kutoka kwa walipa kodi na kuzisafirisha kwenda benki, hali iliyokuwa na changamoto nyingi.
"Tulikuwa tunakusanya fedha na kuzibeba kwenye magari. Wakati mwingine tulilazimika kulaza gari lenye fedha kituo cha polisi kabla ya kuzipeleka benki. Leo hii mlipakodi anakadiriwa, anapatiwa namba ya malipo na analipa kwa simu au benki bila usumbufu," amesema.
Anasema matumizi ya teknolojia yameongeza uwazi, kupunguza mianya ya upotevu wa mapato na kurahisisha ulipaji wa kodi kwa wafanyabiashara na wananchi.
Aidha, amesema utoaji wa elimu kwa walipa kodi kupitia redio, mikutano ya ana kwa ana na ushirikiano na vyama vya wafanyabiashara umeongeza mwitikio wa ulipaji kodi kwa hiari.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian kulia akimkabidhi tunzo mmoja wa wafanyakazi wa mamlaka hiyo aliyeanza ajira mwaka 1996 wakati wa kuanzishwa wa TRA anayefuatia ni Meneja wa TRA Tanga CPA Cantro John. Picha na Mbonea Herman.
"Hapo zamani kulikuwa na uhasama kati ya TRA na wafanyabiashara, lakini sasa tunafanya kazi kwa ushirikiano. Tunazungumza, tunakubaliana na kusonga mbele pamoja. Hayo ndiyo yamechangia mafanikio tunayoyaona leo," amesema.
Castro amesema Serikali imeongeza watumishi zaidi ya 2,000 nchi nzima ili kuboresha utoaji wa huduma kwa walipa kodi na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga (RC), Balozi Batilda Burian, ameipongeza TRA kwa mafanikio hayo akisema mkoa umevuka malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 100 kutokana na ukuaji wa shughuli za uchumi, hususan Bandari ya Tanga na kituo cha mpaka cha Horohoro.
"Tanga ina fursa nyingi za kiuchumi. Tukiongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato na kupanua huduma za TRA, tunaweza kufikia nafasi za juu zaidi kitaifa. Pia wananchi waendelee kuacha magendo na kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa," amesema.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Tanga, Fredy Mmasy amesema ushirikiano uliopo kati ya wafanyabiashara na TRA umeongeza uelewano na kuimarisha ulipaji kodi kwa hiari.
"Zamani uhusiano wetu na TRA ulikuwa kama paka na chui, lakini sasa tunashirikiana vizuri. Hali hiyo imechangia mafanikio makubwa ya ukusanyaji wa mapato," anasema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, amesema ushirikiano kati ya TRA na Halmashauri umewezesha kurasimishwa kwa vikundi vya wajasiriamali zaidi ya 200, hatua inayochochea ukuaji wa biashara na kuongeza mapato ya Serikali.