Tucta yaja na suluhu Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje
Mkurugenzi wa ILO Afrika Mashariki Caroline Mugalla akizindua kituo cha kuwasaidia wafanyakazi wahamaji Tanzania, kulia ni Makamu wa Rais wa TUCTA, Shaban Ambindwile,
Muktasari:
- ILO imesema wafanyakazi wahamiaji bado wanakabiliwa na changamoto za mikataba isiyoeleweka, gharama kubwa za uhamiaji na ukosefu wa taarifa sahihi.
Dar es Salaam. Wakati Tucta ikizindua Kituo cha Msaada kwa Wafanyakazi Wahamiaji Tanzania (Tucta-MWRC), Shirika la Kazi Duniani (ILO) limeeleza wafanyakazi wahamiaji bado wanakabiliwa na changamoto za mikataba isiyoeleweka, gharama kubwa za uhamiaji na ukosefu wa taarifa sahihi.
Mkurugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki, Caroline Mugalla, amesema hayo leo Alhamisi Juni 11, 2026 wakati wa uzinduzi wa kituo hicho uliofanyika Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa kimeanzishwa kulinda haki na masilahi ya wafanyakazi wahamiaji kwa kuwapatia taarifa sahihi, ushauri na mwongozo.
Amesema huduma hizo zitatolewa kwa Watanzania wanaotafuta ajira nje ya nchi pamoja na wafanyakazi wa kigeni wanaokuja kufanya kazi nchini.
“Uhamiaji wa wafanyakazi unapofanyika kwa usalama na kwa kuzingatia haki za binadamu, unachangia ukuaji wa uchumi, kuongeza tija, kuhamasisha uhamishaji wa ujuzi na kuleta maendeleo.”
“Hata hivyo, wafanyakazi wahamiaji hukumbana na changamoto mbalimbali kutokana na kukosa taarifa sahihi kuhusu ajira wanazokwenda kufanya,” amesema Mugalla.
Amesema changamoto nyingine ni mikataba isiyoeleweka, gharama kubwa za uhamiaji na vitendo vya unyonyaji katika baadhi ya maeneo ya ajira.
Aidha, kituo hicho kitachangia kukuza uhamiaji salama unaozingatia sheria na viwango vya kazi vinavyotambulika kimataifa, sambamba na kusaidia juhudi za Serikali kulinda haki za wafanyakazi.
Mkurugenzi wa ILO Afrika Mashariki Caroline Mugalla akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kituo hicho Dar es Salaam
“Wafanyakazi wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi na wale wanaorejea nchini wataweza kupata taarifa sahihi na ushauri kuhusu masuala yote ya uhamiaji. Taarifa hizo zitawasaidia kufanya uamuzi sahihi na kujikinga dhidi ya udhalilishaji na aina mbalimbali za unyonyaji,” amesema.
Amewataka wafanyakazi wahamiaji kutumia kikamilifu huduma za kituo hicho, akisema taarifa sahihi ni msingi muhimu wa kuhakikisha uhamiaji una manufaa kwa mtu binafsi, familia na Taifa.
Takwimu za ILO zinaonyesha mwaka 2022 wafanyakazi wahamiaji walikuwa asilimia 4.7 ya wafanyakazi wote duniani. Kati ya milioni 167.7, wanaume walikuwa milioni 102 na wanawake milioni 64.9.
Makamu wa Rais wa Tucta, Shaban Ambindwile, amelishukuru ILO kwa kuendelea kushirikiana na shirikisho hilo katika ulinzi wa wafanyakazi na kuboresha mazingira ya kazi kwa Watanzania wanaotafuta ajira nje ya nchi.
Amesema kituo hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa wafanyakazi wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi kwa kuwapatia taarifa, ushauri na msaada wanapokumbana na changamoto mbalimbali.
“Lengo letu ni kuisaidia Serikali kuhakikisha wafanyakazi wetu wanakuwa salama na wanapata msaada wanapokumbana na changamoto mbalimbali wakiwa nje ya nchi,” amesema.
Amesema moja ya mikakati ya kituo hicho ni kushirikiana na mashirikisho ya wafanyakazi katika nchi mbalimbali, ili kurahisisha mawasiliano na utoaji wa msaada kwa Watanzania wanaofanya kazi nje ya mipaka ya nchi.
Ambindwile amesema wakati Serikali ikiendelea kutafuta fursa za ajira katika masoko ya kimataifa, kituo hicho kitakuwa na jukumu la kufuatilia mazingira ya kazi na ustawi wa Watanzania wanaopelekwa kufanya kazi nje ya nchi.
“Tutaendelea kushirikiana na ILO pamoja na balozi mbalimbali kuhakikisha wananchi wetu wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi wanafanya kazi katika mazingira salama na yenye kuheshimu haki zao,” amesema.
Ofisa Kazi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Oddo Hekela, amesema uzinduzi wa kituo hicho ni hatua muhimu katika kuimarisha usalama wa Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi.
Amesema kituo hicho kitakuwa daraja muhimu kati ya wafanyakazi, Serikali na wadau wengine kwa kutoa taarifa kuhusu ajira, vibali vya kazi na masuala mengine ya uhamiaji.