Tanzania yaweka wazi mafanikio sita sekta ya kazi ILO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, akizungunza Juni 5, 2026 Mjini Geneva, Uswisi katika Mkutano Mkuu wa 114 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Muktasari:
- Tanzania imeeleza mafanikio sita katika sekta ya kazi kwenye Mkutano wa 114 wa ILO Geneva, yakiwemo ulinzi wa haki za wafanyakazi, hifadhi ya jamii, mfumo wa e-Utatuzi na mageuzi ya mishahara, huku ikisisitiza matumizi ya AI na ushirikiano wa wadau wa utatu kuimarisha ajira zenye staha.
Geneva, Uswisi. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu ameeleza mafanikio sita ambayo Tanzania imeendelea kuyatekeleza katika kuimarisha sekta ya kazi, ajira na ustawi wa wafanyakazi, hatua anazosema zinaifanya nchi kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia duniani.
Akizungumza juzi katika Mkutano wa 114 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) unaofanyika Geneva, Uswisi, Sangu alisema mkutano huo unawakutanisha waajiri na wafanyakazi kutoka nchi wanachama 187 kujadili na kuweka mikakati ya kuboresha sekta ya kazi duniani.
Sangu alitaja mojawapo ya mafanikio hayo kuwa ni dhamira ya Tanzania kuhakikisha mabadiliko ya kiteknolojia yanakuza ajira zenye staha, tija, ubunifu na haki ya kijamii kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, akizungunza Juni 5, 2026 Mjini Geneva, Uswisi katika Mkutano Mkuu wa 114 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Aidha, alisema Serikali imeendelea kulinda haki za wafanyakazi katika mazingira ya kidijitali kupitia Mpango wa Taifa wa Kazi Zenye Staha (NDWCP III), sambamba na kuimarisha usalama na afya mahali pa kazi kupitia mpango wa Vision Zero.
Sangu amebainisha kuwa mafanikio mengine ni kuimarishwa kwa mifumo ya hifadhi ya jamii kupitia Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2023, ambapo zaidi ya wanachama 560,000 wa sekta isiyo rasmi na wanaojiajiri wamefikiwa kupitia usajili wa kidijitali hadi Machi 2026.
Katika hatua nyingine, Sangu alisema Serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa e-Utatuzi unaosimamiwa na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), uliorahisisha upatikanaji wa huduma za utatuzi wa migogoro ya kazi kwa njia ya mtandao kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Aliongeza kuwa Tanzania pia imeimarisha mazungumzo ya kijamii ya pande tatu kati ya Serikali, waajiri na wafanyakazi, hatua iliyowezesha kuanzishwa kwa kiwango kipya cha chini cha mishahara kwa sekta binafsi kuanzia Januari 1, 2026, pamoja na marekebisho ya sheria za kazi yaliyofanyika mwaka 2025.
Sangu alisema eneo jingine ni ushirikiano kati ya Tanzania na ILO katika kuhakikisha matumizi ya Teknolojia ya Akili Bandia (AI) yanachochea maendeleo endelevu na kuboresha mazingira ya kazi.
Aidha, alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na kimataifa kuhakikisha teknolojia inatumika kuongeza tija, kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha ustawi wa wafanyakazi.
Kwa upande wao, wawakilishi wa waajiri na wafanyakazi walieleza kuridhishwa na juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuimarisha ushirikiano wa wadau wa utatu (tripartite), wakisema umechochea mshikamano na majadiliano ya pamoja kuhusu ajira, haki za wafanyakazi na ustawi wa waajiri.
Baadhi ya washiriki katika Mkutano Mkuu wa 114 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), uliofanyuka Juni 5, 2026 Mjini Geneva, Uswisi
Mkutano huo wa 114 wa ILO unajadili mustakabali wa kazi duniani, ukiangazia matumizi ya Akili Bandia (AI) katika kukuza ajira zenye staha, kuongeza tija na kuimarisha ukuaji jumuishi wa uchumi.
Pia, washiriki wanajadili masuala mbalimbali yakiwemo utekelezaji wa Mikataba ya ILO, ushirikishwaji wa wadau wa utatu katika majadiliano, kazi zenye staha katika majukwaa ya kidijitali, mageuzi ya usawa wa kijinsia mahali pa kazi, pamoja na utekelezaji wa Mkataba wa Viwango vya Kazi kwa maeneo yasiyo ya mijini (ILO Convention No. 83) unaolenga kulinda haki za wafanyakazi katika maeneo ya pembezoni.
Tanzania imekuwa mwanachama wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) tangu mwaka 1962 na imeendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kimataifa za kulinda haki za wafanyakazi na kukuza ajira zenye staha.
Pia, Tanzania ni mjumbe wa Bodi ya Magavana ya ILO (Governing Body), ikiwakilisha nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki ambapo kupitia nafasi hii imekuwa ikichangia kwa dhati katika maamuzi ya kimataifa yanayohusu Sera za ajira, Haki za Wafanyakazi na Maendeleo ya kijamii, hivyo kuimarisha taswira yake kama mshirika muhimu katika kukuza kazi za staha na usawa katika sekta ya kazi ulimwenguni.
Kupitia Shirika hilo la ILO, kila mwaka imekuwa ikifanyika mikutano ambayo huwakutanisha wawakilishi wa Serikali, Waajiri na Wafanyakazi kutoka katika nchi wanachama 187 kwa lengo la kupanga na kuweka mikakati inayolenga kuboresha na kukuza ustawi wa Sekta ya Kazi Duniani.