Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mifuko ya tabaka ilivyo suluhisho vita dhidi ya upotevu wa mazao

Mariamu Simoni, mkulima wa Kijiji cha Milamate, Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi, akionesha mazao yake yaliyohifadhiwa katika mifuko ya tabaka, teknolojia inayosaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na kulinda ubora wake wakati wa uhifadhi.

Katavi. Kwa miaka mingi wakulima wadogo nchini wamekuwa wakitumia nguvu, muda na rasilimali nyingi katika kuzalisha mazao ya chakula ili kujihakikishia huduma hiyo na kuongeza kipato cha familia.

Hiyo ni kutokana na kukosa elimu, ubunifu na teknolojia, huku takwimu zikionesha kati ya asilimia 30-40 mazao ya chakula haswa nafaka jamii ya mikunde yanayovunwa hupotea kila mwaka kabla ya kumfikia mlaji.

Utafiti wa wataalamu wa kilimo wanaeleza sehemu kubwa ya hasara hiyo husababishwa na wadudu waharibifu, unyevunyevu, ukungu na sumu kuvu hali inayosababisha wakulima kukosa taarifa na maarifa sahihi ya kuhifadhi mazao hayo.

Matokeo yake, baadhi yao hulazimika kuuza mazao mara tu baada ya kuvuna kwa bei ya chini ili kuepuka hatari ya uharibifu kutokana na ukosefu wa teknolojia sahihi za uhifadhi.

Hata hivyo, matumaini mapya yanaanza kuonekana kupitia matumizi ya mifuko mipya ya tabaka isiyopitisha hewa ‘Hermetic Bags’ ambayo imeibuka kama suluhisho na kuleta matumaini kwa wakulima haswa mkoani Katavi.

Baadhi ya Mifuko ya tabaka ya PICS (Kinga Njaa) na SAFI iliyohifadhi mahindi, teknolojia inayowezesha wakulima kuhifadhi nafaka kwa usalama na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.

Teknolojia hiyo inahamasishwa kupitia Mradi wa Usimamizi wa Mazao baada ya Kuvuna kwa wakulima wadogo nchini unaolenga kuboresha usalama wa chakula, lishe na fursa za kiuchumi.

Lengo kuu ni kuongeza uelewa wa wakulima kuhusu matumizi ya teknolojia ya uhifadhi salama wa nafaka na kuboresha upatikanaji wa mifuko hiyo kwa kaya zaidi ya 100,000 kwa wakulima nchini.

Ushuhuda wa wakulima katika Mkoa wa Katavi waliokwisha kutumia mifuko ya tabaka wanasema teknolojia hiyo imeleta mabadiliko makubwa katika uhifadhi wa mazao yao.


Shuhuda za wakulima

Mkulima Nairat Kagozi kutoka wilayani Tanganyika mkoani Katavi, anasema kabla ya kutumia mifuko hiyo alikuwa akipoteza sehemu kubwa ya mavuno yake kutokana na mashambulizi ya wadudu waharibifu, hasa dumuzi.

“Tulikuwa tunauza mahindi haraka hata kama bei ilikuwa ndogo kwa sababu ya kuogopa mazao kuharibika, sasa tunayahifadhi kwenye mifuko ya tabaka na kusubiri wakati sahihi wa kuuza ili kupata faida zaidi,” anasema.

Nairat anaongeza mifuko hiyo imewawezesha wakulima kuhifadhi mazao kwa muda mrefu bila kutumia kemikali za kuhifadhia nafaka, akieleza kuwa teknolojia hiyo inalinda pia afya za walaji.

Hata hivyo, anasisitiza elimu ya matumizi sahihi ya teknolojia hiyo bado inahitajika kwa wakulima wengi ili kuondokana na changamoto za uhifadhi na usalama wa chakula kwa jamii.

“Mazao yanapaswa kukaushwa vizuri kabla ya kuhifadhiwa, mifuko ifungwe kwa umakini mkubwa na ihifadhiwe sehemu salama isiyo na unyevunyevu” anasema Nairath.

Kwa upande wake, Ezekiel Ulimbu ambaye pia ni mtumiaji wa teknolojia hiyo, anasema siri ya mafanikio ya mifuko ya tabaka ni uwezo wake wa kuzuia hewa kuingia ndani ya mfuko.

“Mazao hubaki salama kwa muda mrefu bila kutumia kemikali lakini tofauti na nafaka zilizohifadhiwa kwa kutumia kemikali, mazao yaliyohifadhiwa kwa teknolojia ya hermetic hubaki salama kwa matumizi ya haraka bila kuhatarisha afya ya mlaji,” anasema.


Wafanyabiashara

Mfanyabiashara wa pembejeo mjini Mpanda, Juma Machimu, anasema mwaka 2024 aliuza mifuko 25 pekee lakini mwaka 2025 iliongezeka hadi mifuko 200 na matarajio mwaka huu ni kuuza zaidi ya mifuko 500.

Anasema ongezeko hilo limetokana na kampeni za elimu zinazotolewa na wadau wa kilimo, hususan Helvetas Tanzania, ambazo zimewafanya wakulima wengi kutambua faida za teknolojia hiyo.

“Wakulima wanapoona wenzao wamefanikiwa kuhifadhi mazao bila hasara nao huhamasika kutumia mifuko hiyo kwakuwa gharama bado ni kubwa licha ya mafanikio” anasema Machimu.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Mahindi mjini Mpanda, Ashely Nduru, anasema mfuko mmoja huuzwa kati ya Sh4,500 hadi Sh5,000, jambo linalowafanya baadhi ya wakulima kuiona ghali.

“Mfanyabiashara anayehitaji mifuko 300 analazimika kutumia zaidi ya Sh1.5 milioni kwa baadhi ya watu, kiasi hiki bado ni kikubwa, wakulima huamua kutumia kemikali kuhifadhi nafaka kukwepa gharama” anasema.


Wadau nao

Msimamizi wa Mradi wa Uhifadhi Nafaka Salama wa Helvetas katika mikoa ya Katavi na Rukwa, Zakaria Nyahende anasema zaidi ya wakulima 40,000 tayari wamefikiwa na elimu ya matumizi ya mifuko ya tabaka.

Anasema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa SAT, Helvetas Tanzania, SUA, na Chuo Kikuu cha Zurich ukiwa na lengo la kuboresha usalama wa chakula, lishe na kipato cha wakulima kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa za uhifadhi.

Mwalimu Ezekiel Ulimbu, mkulima wa Mpanda mkoani Katavi, akishirikiana na kijana wake kujaza mahindi kwenye mifuko ya tabaka kwa ajili ya kuhifadhi mazao baada ya mavuno.

Anabainisha kuwa matarajio ya mradi ni kuwafikia zaidi ya wakulima 100,000 na kuwezesha kaya za wakulima wadogo kupata mifuko hiyo kwa urahisi zaidi kupitia mifumo ya malipo ya baadaye.

“Takribani kaya 8 milioni za wakulima wadogo nchini zinaweza kunufaika endapo mifuko hiyo itapatikana kwa bei rafiki na sisi wadau tunazo hatua za kuifanya iwe nafuu kwa kuondoa au kupunguza tozo za kodi” anasema.

“Kadri matumizi ya mifuko ya tabaka yanavyozidi kuongezeka nchini, ndivyo matumaini ya kupunguza upotevu wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza kipato cha mkulima yanavyozidi kuimarika” anasema.


Mkakati wa Serikali

Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Katavi, Faridu Abdallah anasema Serikali kwa kushirikiana na mashirika, taasisi binafsi na wadau wa maendeleo imeendelea kuhamasisha matumizi ya mifuko ya tabaka ili kupunguza upotevu wa mazao.

Anasema katika miaka ya nyuma Mkoa wa Katavi ulikuwa ukipoteza zaidi ya asilimia 40 ya mazao yaliyovunwa kutokana na changamoto za uhifadhi, lakini hali hiyo inaanza kubadilika kutokana na matumizi ya teknolojia mpya.

“Tumekuwa tukipokea maoni kuhusu gharama za mifuko hii, lakini tunaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta njia za kupunguza gharama ili wakulima wengi zaidi waweze kumudu kuipata,” anasema.