Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilimo cha michikichi na ufuta chafungua fursa kwa wananchi Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge

Muktasari:

  • Serikali ya Mkoa wa Pwani imeanzisha kilimo cha pamoja cha michikichi katika wilaya za Kisarawe na Rufiji kwenye ekari 78,000 na kutenga ekari 500 kwa kilimo cha ufuta, hatua inayolenga kuongeza ajira, kuinua kipato cha wananchi na kukuza uchumi wa mkoa.

Kibaha. Wananchi wa Mkoa wa Pwani wanatarajiwa kunufaika na fursa za ajira, ongezeko la kipato na ukuaji wa shughuli za kiuchumi kufuatia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kilimo cha michikichi na ufuta inayotekelezwa na Serikali katika wilaya za Kisarawe na Rufiji.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa  Juni 5,2026 mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030 kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026 katika kikao kazi kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinishee Mlao.

Kunenge amesema Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa kilimo cha michikichi katika jumla ya ekari 78,000, ambapo ekari 38,000 zipo Wilaya ya Kisarawe na ekari 40,000 zipo Wilaya ya Rufiji.

Amesema pamoja na mradi huo, Serikali imetenga ekari 500 kwa ajili ya kilimo cha ufuta, huku ekari 300 zikiwa tayari zimegawiwa kwa vijana 150 wa Wilaya ya Kisarawe ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali.

"Lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata fursa za kiuchumi kupitia sekta ya kilimo, kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara na kuimarisha kipato cha kaya," alisema Kunenge.

Almeongeza kuwa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kukuza uchumi wa wananchi na kupanua wigo wa ajira, hasa kwa vijana.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinishee Mlao, aliwataka wakurugenzi wa halmashauri na wananchi wa mkoa huo kuwa waangalifu katika matumizi ya ardhi na kuepuka kuuza maeneo yao bila kuzingatia maslahi ya baadaye.

"Ardhi ni rasilimali muhimu na urithi wa vizazi vijavyo. Tusipokuwa makini tunaweza kujikuta tumepoteza msingi mkubwa wa maendeleo yetu. Wananchi waithamini na waitumie kwa manufaa ya kiuchumi," alisema Mlao.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Pwani, Catherine Katele, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za kijamii hususan upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali ya mkoa.


"Serikali imefanya kazi kubwa ya kusogeza huduma za maji karibu na wananchi. Jukumu letu sasa ni kulinda miundombinu hiyo ili iendelee kuhudumia wananchi kwa muda mrefu," alisema Katele.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibiti, Juma Ndaruge, alisema mafanikio ya maendeleo yanayopatikana mkoani humo yanapaswa kutumiwa kama chachu ya kuongeza uzalishaji na kuimarisha shughuli za kiuchumi.

"Wananchi wanapaswa kuzitumia fursa hizi kwa tija ili maendeleo yanayoletwa na Serikali yaweze kuwanufaisha zaidi katika maisha yao ya kila siku," alisema.

Katibu wa CCM Wilaya ya Kibaha Vijijini naye alisema utekelezaji wa Ilani ya CCM umeendelea kuleta mafanikio katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.

"Maendeleo yanayoonekana katika maeneo mbalimbali ni uthibitisho wa utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwa wananchi na Serikali inaendelea kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo yao," alisema.

Kikao hicho kilijadili utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa robo ya kwanza ya mwaka 2026 na kupokea taarifa za maendeleo kutoka sekta mbalimbali za Mkoa wa Pwani.