Prime
Agizo la Mwigulu kuhusu mabasi kuingia stendi lagonga vichwa
Muktasari:
- Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alitangaza uamuzi huo bungeni Mei 7, 2026, akieleza ni sehemu ya mkakati wa Serikali kupunguza gharama za usafiri na kudhibiti ongezeko la nauli kwa wananchi.
Mwanza. Agizo la Serikali linaloruhusu mabasi kutopita katika vituo vya mabasi (stendi) vya mikoa mbalimbali iwapo hayana abiria wa kushusha au kupandisha, limepokelewa kwa sura tatu tofauti na wadau wa sekta ya usafirishaji.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alitangaza uamuzi huo bungeni Mei 7, 2026, akieleza kuwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kupunguza gharama za usafiri na kudhibiti ongezeko la nauli kwa wananchi.
Alisisitiza kuwa baadhi ya taratibu zilizokuwa zikifuatwa awali zilikuwa hazina ulazima na zilichangia kuongeza gharama zisizo za lazima kwa wenye mabasi.
Hatua hiyo imegonga vichwa vya wadau wa sekta ya usafiri wakieleza manufaa yake, lakini pia mamlaka za serikali za mitaa na baadhi ya wananchi wakieleza changamoto zake.
Kundi la kwanza lilizongumzia hatua hiyo ni watoa huduma za usafirishaji ambao wamepongeza hatua hiyo wakisema itapunguza gharama za uendeshaji na kuokoa muda; pili, ni halmashauri zikihofia kupoteza mapato yatokanayo na stendi hizo; na tatu ni abiria kukabiliwa na changamoto ya usafiri wanaposhusha maeneo yasiyo sahihi.
Furaha ya madereva
Madereva wanaeleza kuwa kabla ya agizo hilo, walilazimika kuingia katika kila stendi hata kama hawakuwa na abiria wa kushusha au kupakia, hali iliyokuwa inaongeza gharama za ushuru pamoja na kuchelewesha safari.
Mathalan, wamesema katika Manispaa ya Tabora, mabasi makubwa yanatozwa ushuru wa Sh4,000 kwa kila safari yanapoingia stendi huku mabasi madogo yakitozwa Sh3,000, gharama ambazo madereva wanasema zilikuwa zinaongeza mzigo wa uendeshaji.
Madereva wanasema agizo la Waziri Mkuu limekuwa mkombozi kwao hasa katika kupunguza matumizi kutokana na kupaa kwa bei ya mafuta, sambamba na kuokoa muda wa safari unaopotea.
Dereva wa basi mkoani Tabora, Saidi Mhoja amesema uamuzi huo umeondoa mzigo mkubwa waliokuwa wakikumbana nao njiani.
“Waziri Mkuu kaona mbali kwa sababu hii ilikuwa ni moja ya vitu vinavyotuumiza, uendeshaji wa huduma ya usafiri ulifanywa mgumu na gharama za kila stendi zinatofautiana,” amesema.
Katika Manispaa ya Moshi, dereva mmoja wa basi la masafa marefu aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, amesema agizo hilo limeleta nafuu kubwa kwao na kwa abiria kwa ujumla.
“Inaokoa muda kwanza kwa abiria kwa sababu ulikuwa lazima uingie stendi hata kama hushushi wala kupakia abiria, kwa maelekezo ya uongozi wa hapo. Usipoingia stendi ina maana unapigwa faini,” amesema dereva huyo.
Ameongeza kuwa kwa sasa mabasi yanafika mapema zaidi kuliko hapo awali, jambo linaloongeza ufanisi wa huduma na kupunguza uchovu kwa madereva.
Changamoto kwa abiria
Licha ya manufaa hayo, baadhi ya abiria wameanza kulalamikia namna madereva wanavyotekeleza agizo hilo, wakidai kuwa linatumika vibaya.
Mkoani Tabora, baadhi ya mabasi yanatuhumiwa kushusha abiria katika maeneo yasiyo rasmi, hali inayowalazimu abiria kutumia fedha zaidi kufika walikokusudia.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora, John Pima amethibitisha kuwepo kwa changamoto hiyo, akisema baadhi ya madereva wanatafsiri vibaya agizo hilo.
“Agizo hili la waziri mkuu wanalitafsiri tofauti kwani wanalitumia sasa kuwaumiza zaidi abiria wakati lengo la ni kumpunguzia gharama za usafiri mwananchi,” amesema.
Hata hivyo, amesema licha ya hali hiyo, mapato ya stendi hayajaathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na mabasi mengi kuendelea kuingia kwenye stendi hiyo.
Kuhusu malalamiko hayo, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Aridhini (Latra) mkoani Tabora, Nelson Mmary amesema madereva na wamiliki wa mabasi wanapaswa kuzingatia sheria zote za usafirishaji na hawatosita kuchukua hatua kwa dereva atakayekiuka utaratibu.
Amesema ni lazima basi liingie kituo kikubwa cha mabasi bila kujali lina abiria wa kushusha au wa kupandisha, lakini kwenye vituo vilivyopo wilayani si lazima kuingia steni, labda liwe na abiria wa kushusha au kupandisha au kupata huduma za kijamii kwa abiria.
“Wazingatie sharia, hatutofumbia macho dereva au mmiliki wa mabasi atakayekwenda kinyume na utaratibu...kuna baadhi ya mabasi wanatii agizo la kutoingia vituoni lakini gharama za usafiri na usafirishaji bado ni aghali na pia wanawashusha abiria maeneo yasiyo salama, jambo ambali si sahihi,” amesema.
Hali ni tofauti Moshi
Katika Manispaa ya Moshi, picha ni tofauti kidogo ambapo Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mwajuma Nasombe amesema agizo hilo halijaathiri mapato ya halmashauri kwa sababu ya shughuli kubwa za kiuchumi zinazofanyika katika stendi hiyo.
“Kwa upande wangu hapa Moshi, kufuatia maelekezo ya waziri mkuu, hakuna sehemu yoyote ambayo tumeathirika. Sisi hatuna magari ambayo hayashushi wala hayapakii abiria. Moshi ni kituo cha biashara, kwa hiyo magari mengi yakitoka Arusha au yakienda Dar es Salaam ni lazima yawe na abiria wanaoingia hapa Moshi na hivyo ni lazima yataingia stendi,” amesema.
Hata hivyo, amebainisha changamoto nyingine ambayo si ya moja kwa moja kutokana na agizo hilo, ya uwepo wa vituo binafsi vya mabasi nje ya stendi kuu.
“Kimtazamo, kitendo hiki kwa namna moja au nyingine kinapunguza mapato yetu ya halmashauri kwa sababu gari ikiingia stendi kuu lazima ichangie,” amesema.
Amesema Serikali inaendelea kujenga stendi mpya yenye uwezo mkubwa, hatua ambayo inatarajiwa kuondoa changamoto ya vituo vidogo na kuongeza mapato ya halmashauri.
Hali ilivyo Kanda ya Ziwa
Mkoani Mwanza, utekelezaji wa agizo hilo unaonekana kuwa wa wastani, ambapo madereva huingia stendi pale tu wanapokuwa na abiria wa kushusha au kupakia.
“Tukiingia stendi ni bure lakini kutoka tunalipa ushuru wa Sh2, 000. Mara chache tunaingia kama tuna abiria wa kushusha au kupakia, kama hakuna tunaendelea na safari,” amesema Mrisho Abel, dereva wa basi, njia ya Mwanza – Shinyanga.
Katika mkoa huo, kuna stendi kuu mbili; Nyegezi na Nyamhongolo ambapo mabasi hutozwa ushuru huku vituo vidogo vya wilayani vikitekeleza utaratibu huo mpya kwa kiasi kikubwa.
Katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, athari za agizo hilo zimeanza kudhihirika wazi kiuchumi.
Watendaji wa halmashauri hiyo wamesema idadi ya mabasi yanayoingia stendi imepungua, hali iliyosababisha kushuka kwa mapato yatokanayo na ushuru.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Iddi Ndabhona amesema halmashauri inaendelea kufanya tathmini ya kina kubaini ukubwa wa athari hizo.
Hata hivyo, agizo hilo ni kicheko kwa madereva ambao wanasema wamepunguziwa mzigo wa gharama za uendeshaji.
“Muda wa safari unapungua na mafuta tunayatumia kidogo tofauti na zamani tulipokuwa tunaingia kila stendi,” amesema dereva wa basi, Derick Josephat.
Wakati huohuo, wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao ndani ya stendi hiyo wameathirika zaidi kwa kukosa wateja ambao ni abiria.
Mfanyabiashara Joyce John amesema kwa sasa hafanyi biashara yake vizuri kwani kipindi mabasi hayo yalipokuwa yakiingia stendi, aliuza bidhaa zake kwa wingi tofauti na sasa.
Imeandikwa na Saada Amir (Mwanza), Hawa Kimwaga (Tabora), Yese Tunuka (Moshi) na Samwel Mwanga (Simiyu).