Mbegu ya ufuta ‘Lindi White’ mkombozi kwa wakulima Lindi, Mtwara
Athanas Minja, mtafiti wa zao la ufuta kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), akionesha ufuta uliokaushwa baada ya kuvunwa shambani.
Muktasari:
- Wakulima wa ufuta washauriwa kutumia mbegu ya ‘Lindi White’ ili kupata mavuno mengi zaidi kwani mbegu hiyo inakabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi
Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wameendea kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo kupitia utafiti wa zao la ufuta, moja ya mazao muhimu ya biashara nchini.
Kupitia Kituo cha Utafiti wa Kilimo Naliendele kilichopo mkoani Lindi, watafiti wamefanikiwa kugundua na kuendeleza mbegu bora ya ufuta iitwayo Lindi 2002 au Lindi White zinazowezesha wakulima kupata mavuno mengi zaidi huku zikikabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu mafanikio hayo, mtafiti wa zao la ufuta kutoka TARI Athanas Minja, amesema taasisi hiyo ndiyo msimamizi wa uratibu wa utafiti wa zao la ufuta kitaifa na imefanikiwa kuzalisha aina mbalimbali za mbegu bora zikiwemo Lindi 2002, Ziada 94 na Mtondo 2013.
Ufuta ukikaushwa baada ya kutoka shambani.
Kwa mujibu wa Minja, mbegu ya Lindi 2022 ambayo wakulima wengi huifahamu kwa jina la “Lindi White” kutokana na rangi yake nyeupe. Imeonyesha uwezo mkubwa wa kuzalisha hadi kilo 1,500 kwa hekta moja chini ya usimamizi mzuri wa kilimo.
Mbegu hiyo pia hukomaa mapema ndani ya siku 100 hadi 110, jambo linaloiwezesha kustahimili mabadiliko ya tabianchi.
“Mbegu hii imekubalika sana sokoni kutokana na ubora wake na rangi yake nyeupe inayohitajika katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Pia ina uwezo wa kuvumilia baadhi ya magonjwa kama ugonjwa wa madoa ya majani,” amesema.
Amesema zao la ufuta lina mchango mkubwa katika uchumi wa mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Mbali na kutumika kama chakula, ufuta ni zao la biashara linalouzwa katika masoko mbalimbali duniani ikiwemo China, Japan na nchi nyingine duniani.
“Kupitia mauzo ya ufuta nje ya nchi, Tanzania hupata fedha za kigeni zinazochangia maendeleo ya uchumi wa taifa. Hali hiyo imeifanya TARI na COPRA kuendelea kuwahamasisha wakulima kutumia mbegu bora ili kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao yao,”amesema
Amesema mbali na kuwa zao la biashara, ufuta una matumizi mengi katika lishe na viwanda. Mbegu za ufuta zina mafuta kati ya asilimia 50 hadi 60, na wastani wa kilo mbili hadi tatu za ufuta zinaweza kutoa lita moja ya mafuta.
Wa kwanza kulia ni Safina Abdurahman, mtoto aliyeshindwa kujiunga na chuo kutokana na changamoto za kifedha, akiwa pamoja na familia yake. Wa pili kulia ni baba yake, Abdurahman, akifuatiwa na mama yake, Asumini Ismail, pamoja na kaka zake Safina.
“Ufuta hutumika katika utengenezaji wa mikate, biskuti, siagi ya ufuta na vyakula vingine vya lishe. Baada ya mafuta kukamuliwa, mabaki yanayojulikana kama mashudu hutumika kama chakula cha mifugo, hivyo kufanya zao hili kuwa na thamani kubwa katika kila hatua ya uzalishaji wake.,”amesema
Amesisitiza kuwa mafanikio ya mbegu bora yanategemea pia kufuata kanuni sahihi za kilimo. Mkulima anatakiwa kupanda kwa wakati, kutumia nafasi sahihi za upandaji, kufanya upunguzaji wa mimea mapema na kuvuna kwa wakati ili kupunguza upotevu wa mazao.
“Kwa mfano, nafasi inayopendekezwa ni sentimita 50 kati ya mstari na mstari. Huku mimea ikiachwa kwa umbali wa sentimita 10 baada ya kupunguza miche. Utekelezaji wa kanuni hizi huwezesha mkulima kufikia mavuno yaliyokusudiwa”amesema.
Katika kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora kwa wakati, TARI imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo COPRA na wengineo.
“Kupitia ushirikiano huo, zaidi ya tani 10 za mbegu bora za ufuta zimesambazwa kwa wakulima katika maeneo mbalimbali hususan mikoa ya Lindi na Mtwara. Lengo ni kuongeza uzalishaji, kuinua kipato cha wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa,”amesema Minja
Anasisitiza kuwa mafanikio yote yanayotokana na mbegu bora za ufuta ni matokeo ya uwekezaji katika utafiti wa kilimo. Kupitia tafiti hizo, wataalamu wameweza kuzalisha mbegu zinazokidhi mahitaji ya soko la dunia, kustahimili mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uzalishaji kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko mbegu za asili.
Kwasababu hiyo, TARI inaendelea kuwahamasisha wakulima kutumia mbegu bora zilizofanyiwa utafiti na kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo ili kuongeza tija, kipato na ushindani wa zao la ufuta katika masoko ya kimataifa.