Zanzibar yageukia teknolojia ya SRI na uhifadhi shirikishi kunusuru misitu, kuongeza tija katika kilimo
Katibu Mkuu wa Wizara Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Saleh Mohamed Juma
Katika kile kinachoonekana kama mapinduzi ya kimyakimya kwenye sekta ya uzalishaji na hifadhi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, imetangaza mikakati mipya ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na uvamizi wa misitu.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Saleh Mohamed Juma amebainisha kuwa ongezeko la watu visiwani humo limeleta shindikizo kubwa kwenye rasilimali ardhi na misitu, hali inayohitaji mbinu mbadala za kisayansi na ushirikishwaji wa jamii.
Kutokana na maeneo mengi ya misitu kuvamiwa, wizara imeamua kutumia mbinu ya uhifadhi shirikishi kupitia kamati za jamii zinazojulikana kama Neta Kofma (Community Forest Management).
Katibu Mkuu anafafanua kuwa wananchi wa pembezoni mwa misitu sasa ndiyo walinzi wakuu wa rasilimali hizo.
“Asilimia kubwa ya waharibifu wa misitu hawatoki mbali na msitu ulipo. Tukifanikiwa kuwapata wananchi wenyewe wawe walinzi, kazi inakuwa rahisi kwa sababu wao ndiyo wako kule; mtu akipiga shoka au msumeno ni rahisi kwao kusikia kuliko kusubiri maafisa kutoka mjini,” anasema Saleh.
Lengo la Serikali ni kuifanya jamii ione faida ya misitu kwa vizazi vya sasa na vijavyo, huku ikihimiza miradi mbadala ya kiuchumi kama ufugaji wa nyuki na kilimo cha vanilla ndani ya misitu bila kuiharibu.
Teknolojia ya SRI: Jibu la ukame katika kilimo cha mpunga
Mabadiliko ya tabianchi yameleta joto kali na upungufu wa mvua, jambo linaloathiri kilimo cha mpunga ambacho kinahitaji maji mengi. Ili kukabiliana na hali hii, Zanzibar imeanza kutumia teknolojia ya SRI (System for Rice Intensification), ambayo inapunguza matumizi ya maji kwa kiasi kikubwa.
Tofauti na mfumo wa kizamani ambapo shamba la mpunga lilikuwa likijazwa maji muda wote, SRI inahusisha mzunguko wa kujaza maji na kukausha shamba. “Kile kipindi ambacho unalikausha shamba ndiyo mpunga unatoa machu (shina) zaidi na inasaidia kuokoa maji ya visima ambayo uzalishaji wake ni wa gharama kubwa,” anafafanua Katibu Mkuu.
Pamoja na teknolojia hiyo, Serikali imekuwa ikifanya majaribio ya mbegu mpy zinazostahimili ukame. Katibu Mkuu anatoa mfano wa mafanikio ambapo wakulima walivuna magunia mengi hata katika msimu wa vuli ambao ulikuwa na mvua chache sana.
Mmoja wa wakulima walionufaika na majaribio ya mbegu hizi mpya, Salum Salum Fatim kutoka eneo la Dunga, alionyesha kufurahishwa na matokeo ya mbegu hizo.
Mkulima huyo alieleza kuwa mbegu hizo si tu kwamba zinavumilia ukame, bali pia mchele wake una ladha nzuri na uzalishaji ni mkubwa ikilinganishwa na mbegu za asili.
Hata hivyo, mafanikio katika uzalishaji yameleta changamoto nyingine ya masoko. Katika msimu uliopita, uzalishaji wa mananasi ulikuwa mkubwa sana kiasi cha kushusha bei hadi kufikia fungu la mananasi matano kuuzwa kwa Sh 5,000.
“Kwa upande wa Serikali, haya ni mafanikio ya uzalishaji, lakini kwa mkulima ni maumivu kwa sababu anataka soko lenye faida. Tunajifunza kuwa tunapaswa kuunganisha uzalishaji na viwanda vya kuchakata mazao ili kuzuia uharibifu wakati wa mavuno mengi,” anasema Saleh.
Wizara pia imepiga hatua katika matumizi ya mashine. Kwa sasa, wakulima wanapatiwa huduma za matayarisho ya mashamba, machipukizi, kuburuga, kuchamba, kuboroga, kuchavanga, kupanda, kupandikiza na kuvuna kwa kutumia mashine, jambo linalopunguza mahitaji ya nguvu kazi ya watu.
Katibu Mkuu huyo anabainisha kuwa wako katika mchakato wa kuanzisha mashine za kupandikiza (transplanters) na za kuvunia.
“Mashine ya kuvunia inaweza kumaliza eka moja ndani ya dakika 50, kazi ambayo ingechukua timu nzima ya mpira siku nzima kuimaliza,” anasema.
Katibu Mkuu huyo anasema, mwelekeo wa sasa wa Zanzibar katika kuboresha kilimo na kuhifadhi misitu hauishii tu kwenye uzalishaji wa chakula, bali unagusana moja kwa moja na harakati za kimataifa za kusimama na sayansi katika kulinda afya.
Kupitia mfumo wa 'Afya Moja' sayansi inatufundisha kuwa afya ya binadamu, wanyama, na mazingira imeshikamana kwa karibu.
Inakadiriwa kuwa kati ya asilimia 60 hadi 70 ya milipuko ya magonjwa ya kuambukiza inatokana na mwingiliano kati ya binadamu, wanyama na uharibifu wa mazingira.
Hivyo, juhudi za Serikali ni kulinda na kuhifadhi rasilimali za misitu Zanzibar si tu za kiuchumi, bali ni kinga ya afya ya jamii dhidi ya magonjwa yanayoibuka.
Wito kwa uwekezaji katika ubunifu na utafiti
Mafanikio yoyote ya kisayansi, yawe kwenye mbegu mpya za mpunga zinazostahimili ukame au kwenye chanjo za magonjwa, hayana maana kama hayatamfikia mlaji wa mwisho kwa wakati.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linahimiza Serikali kuongeza uwekezaji wa ndani katika sayansi na ubunifu ili kujenga mifumo thabiti ya ulinzi wa afya na uchumi.
Katibu Mkuu amebainisha kuwa Zanzibar ina uwezo mkubwa wa kupiga hatua zaidi ikiwa itajikita katika kuingiza ushahidi wa kitafiti moja kwa moja kwenye mifumo yake ya utendaji.
Hii ni fursa kwa taasisi kama Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kushirikiana na wadau wa Zanzibar katika kuendeleza tafiti zinazojibu changamoto za mahali husika.
Mustakabali upo mikononi mwa sayansi na jamii
Kaulimbiu ya “Pamoja kwa Afya; Simama na Sayansi” inatukumbusha kuwa kila mmoja wetu ana jukumu la kufanya. Kuanzia kwa mkulima anayejaribu mbegu mpya za mpunga visiwani Zanzibar, hadi kwa kijana anayetafuta fursa katika kutoa huduma za mashine za kisasa za kilimo, wote wanachangia katika ujenzi wa Taifa lenye usalama wa chakula na afya thabiti.
Kama alivyosisitiza Katibu Mkuu, siri ya mafanikio ipo katika kuacha kuwatetea wahujumu wa rasilimali na kuanza kukumbatia mbinu za kisasa zinazolinda mazingira na kukuza tija.
Ni wakati wa Zanzibar kuandika ukurasa mpya ambapo sayansi si tu nadharia, bali ni nyenzo ya kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha ya kila mwananchi.
Aidha, Katibu Mkuu ametoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa za kilimo na kutoa huduma za mashine (kama 'boda boda' za mashine za kilimo) ili kujiajiri. Pia amewataka wananchi na viongozi kuacha kuwatetea wahujumu wa mazingira ili kulinda mustakabali wa visiwa vya Zanzibar.