Ukuaji matumizi simu janja ulivyoongeza matumizi ya 'data'
Dar es Salaam. Wakati matumizi ya simu janja yakitajwa kunufaisha Watanzania katika shughuli zao za kiuchumi, pia ukuaji wake unatajwa kuongeza matumizi ya intaneti.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Basiimire Novemba 7, 2024 akisoma Taarifa ya Fedha kwa Robo inayoishia Septemba 30, 2024.
Taarifa hiyo inasema Vodacom imerekodi ongezeko la asilimia 23.6 la watumiaji wa simu janja huku ongezeko hilo likihusianishwa na ongezeko la matumizi ya data ya intaneti kwa asilimia 50.
Akizungumzia mafanikio hayo, Basiimire amesema: "Mafanikio haya ni sehemu ya dhamira yetu ya kuunganisha jamii kwa mustakabali bora, kwa kuhakikisha tunaondoa mgawanyo wa kidijitali (digital divide) baina ya wananchi."
Katika kuhakikisha mgawanyo huo unaosababisha athari hasi katika ukuaji wa teknolojia unamalizika, Basiimire amesema Sh127.7 bilioni zimetumika katika kuimarisha uwekezaji ambao unalenga kupanua huduma ya 4G.
"Mbali na ukuaji wa teknolojia tu Uwekezaji uwekezaji huu unalenga pia kuongeza ufanisi wa nishati safi na kupunguza utoaji wa hewa ukaa, kwa kuendana na mikakati.
"Ambapo dira ya kampuni yetu inajikita katika uendelevu wa mazingira na uwezeshaji wa jamii, katika hilo mpaka Sasa Vodacom imepanda miti 50,000," amesema na kuongeza Basiimire.
Kwenye upande wa kifedha, taarifa hiyo imesema Vodacom imeendelea kuimarika, huku mapato ya huduma yakipanda kwa asilimia 19.1 hadi Sh718.2 bilioni pia faida halisi iliongezeka kwa asilimia 42.4 na kufikia Sh42.2 bilioni ikilinganishwa na kipindi kama hiki kilichopita
Pia, idadi ya wateja imekua kwa asilimia 13.2 na sasa imefikia milioni 20.9 huku mikopo yenye thamani ya Sh1 trilioni ikitolewa kwa watumiaji milioni 6 wa huduma za kifedha za mtandao huo.
Akimalizia kusoma ripoti hiyo, Basiimire alionyesha matumaini ya kuendelea kupata ukuaji endelevu wa mapato pamoja na dhamira ya kudumu ya ushirikishwaji wa kifedha na ufikiaji wa teknolojia kwa Watanzania wote.