Unataka kuwekeza Tanzania? Hizi hapa fursa

Muktasari:

  • Unataka kuwekeza Tanzania? Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) kimetaja fursa na unafuu wa kodi kwa yeyote atakayejitokeza kuwekeza Tanzania ikiwamo Wilaya ya Pangani maeneo ya uchumi wa buluu, kilimo biashara na utalii.

Dar es Salaam. Unataka kuwekeza Tanzania? Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimetaja fursa na unafuu wa kodi kwa yeyote atakayejitokeza kuwekeza Tanzania ikiwamo Wilaya ya Pangani maeneo ya uchumi wa buluu, kilimo biashara na utalii.

TIC imesema fursa zote zimeainishwa katika makundi matatu ya mitaji ya uwekezaji: mtaji wa kawaida(mdogo), mtaji wa uwekezaji wa umahili(kati) na mtaji wa uwekezaji wa umahili maalumu(mkubwa) chini ya Sheria ya Uwekezaji Tanzania wa Mwaka 2022.

Akizungumza usiku wa kuamkia leo Jumapili Oktoba 8, 2023 wakati wa Jukwaa la Uwekezaji katika Wilaya ya Pangani (PIF) jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, John Mnali amesema;

“Kwa mwekezaji atakayejitokeza kuwekeza eneo la shughuli za uchumi bahari  uvuvi, kiimo cha biashara na kuuza nje bidhaa zao kwa asilimia 80, watafutiwa kodi ya mapato asilimia 30, ushuru wa halmashauri kwa miaka kumi,”amesema akifafanua:

“Kwa wale watakaowekeza katika utalii watasajiliwa na TIC, hawa watapata unafuu kutokana na aina ya mitaji yao ya uwekezaji katika makundi hayo matatu.”

Kisheria, mtaji wa kima cha chini unaanzia dola 50,000 na wageni dola 500,000 wakati mtaji wa kima cha kati wazawa ni dola milioni 20 na wageni dola milioni 50. Kwa uwekezaji mkubwa ni kuanzia dola milioni 300 kwa wazawa na wageni.

Amesema kundi la kati na mubwa lina fursa ya kuchagua vivutio vya nyongeza ili kutoa nafasi kwa mwekezaji asibanwe na vivutio vinavyotlewa na Serikali.

“Kwa mtaji wa kima cha chini watasamehewa ushuru wa forodha wanapoingiza bidhaa, msamaha maalumu wa Kodi ya Ongezeko la Thamani(VAT) kwa asilimia 75 katika vifaa visivyokuwa mahususi vya mtaji.Kundi la Pili wanapata vivutio vyote wanavyopata kundi la kwanza.”

Mnali ametoa mwelekeo huo mbele ya wanajukwaa wa tukio hilo lililokuwa sehemu ya onyesho la saba la Utalii la Kimataifa la Swahili kwa mwaka 2023 litakalofungw leo jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri Mkuu Doto Biteko aliyezindua jukwaa hilo ameagiza kila wilaya nchini kuwa na ubunifu wa vyanzo vya uwekezaji kwa lengo la kusaidia malengo ya kitafa.

“Kama wilaya zote zingekuwa zinafanya ubunifu wa kukuza uwekezaji, tungepunguza mzigo kwa rais wetu(Rais Samia Suluhu Hassan), itapunguza mzigo kwa wizara katika kuhudumia wananchi,”amesema Biteko akifafanu:

“Utalii hauwezi kukua kwa juhudi za rais peke yake, leo Pangani wanasaidia kutangaza vivutio vya uwekezaji, natamani kuona kila wilaya ikifanya ubunifu wa fursa ilizonazo.”

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu aliunga mkono hoja hiyo huku wizara na taasisi zikieleza namna zinazorahisisha mazingira ya uwekezaji Pangani.

“Wizara inaendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, usafiri wa reli na bandari. Taifa lina bandari 693 hazijarasimishwa, bandari zilizorasimishwa ni 86 tu,”amesema Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile akiongeza:

“Tumeanza uwekezaji bandari ya Dar es Salaam kuanzia gati namba 1-11 , tunakwenda ya Bagamoyo, Pangani kuna bandari tatu, Pangani imehudumia tani 16,00, Kipumbwi(21) na Mkwaja tani 7,494 zikiwamo 33 za mifugo, wizara itaboresha bandari hii ili iwe fursa ya kusafirisha nyama nje.”


Kuhusu Pangani

Kwa mujibu wa wilaya hiyo iliyoanzishwa mwaka 1958 chini ya mkuu wa wilaya wa kwanza ambaye ni rais mstaafu Jakaya Kikwete, sasa ina wakazi 75, 642 huku wastani wa pato la kila mkazi likiwa Sh1.4milioni kila mwaka.

Pato hilo linatokana na asilimia 60 ya kaya zilizojiajiri kwenye kilimo na uvuvi ambapo mwaka 2022/23 asilimia 30 ya mapato ya Sh1.6bilioni za wilaya zilizokusanywa kupitia ajira 8.000 za uvuvi. 

Pia, ina wafanyabiashara wadogo 750, makundi 45 ya wazalishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo huku ikiwa na umeme katika vijiji vyote 33 vya wilaya.

Mkuu wa wa wilaya hiyo, Zainab Abdallah amewakaribisha wawekezaji wa ndani nan je kwenda kuwekeza maeneo sita yenye ushawishi wa kurejesha mtaji na faida

Kwanza ,wilaya hiyo imetenga eneo la kilometa za mraba 40.2 za ufukwe wa bahari kwa ajili ya uwekezaji wa hoteli za kitalii, maeneo ya starehe na kisiwa cha Maziwe kilometa nane kutoka Pangani mjini.

Pili, mji huo wenye mandhari ya kale umetenga pia ekari 16,000 za ardhi ya kilimo cha biashara kwa mazao ya mkonge, korosho, karanga, nazi na mbongambonga katika vijiji vya Mseko, Mbulizaga, Mtonga na Mtango.

Msingi wa jukwaa hilo kutangaza vivutio vya uwekezaji ili kukuza mchango wake wa GDP, kuondoa umaskini wa wakazi wake na kuimarisha huduma za kijamii. 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula amesema jukwaa hilo ni sehemu ya malengo ya wizara kuchechemua ukuaji wa sekta ya utalii ili kukuza mchango wake kitaifa. 

“Tunatamani mchango wa fedha za kigeni uongezeke kutoka asilimia 25 ya sasa na asilimia 17 ya Pato la Taifa(DGP), tunataka ifikapo mwaka 2025 tufikia watalii milioni tano na fedha za kigeni dola milioni sita,”amesema Kitandula.