Uwekazaji wa CRDB kwa wajasilimali watambuliwa

Dar es Salaam. Uwezeshaji wa Sekta ya biashara ndogo na ya kati (SME) nchini unaifanya Benki ya CRDB kuwa miongoni mwa benki tano Afrika zilizotunukiwa Tuzo ya Benki Bora ya SME 2023 chini ya utendaji kazi unaoanzia Aprili 1, 2021 hadi Machi 31, mwaka jana.  

Washindi wa tuzo hizo chini ya Jarida la Kimataifa la masuala ya Fedha, Global Finance, walichaguliwa kutoka Afrika, Asia-Pacific, Karibiani, Ulaya ya Kati na Mashariki, Amerika ya Kusini, Mashariki ya Kati, Amerika Kaskazini na Ulaya Magharibi. Benki ya CRDB ndiyo benki pekee kutoka Afrika Mashariki na Kati.

Taarifa ya jana ya CRDB inasema utambuzi huo uliofanyika jijini London, Uingereza hivi karibuni unachagizwa na dhamira iliyopo katika uwezeshaji wenye tija kwa kila mfanyabiashara wa daraja hilo kwa kupata usaidizi wa mahitaji ya kila siku ya benki.

"Ni heshima kubwa kupokea tuzo hii maalum,  uthibitisho kuhusu msaada wetu wa kudumu kwa wajasiriamali wadogo na wa kati nchini. Utendaji wetu katika sekta ya SME unatokana na ushirikiano imara wa kimkakati,” alisema Bonaventure Paul, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo wa Benki ya CRDB.

Hivi karibuni, Benki hiyo ilipokea mkopo wa euro 150 milioni(Sh370bilioni) kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya(EIB), utaimarisha upatikanaji wa fedha kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini, na kujumuisha ufadhili wa kujitolea kwa biashara za wanawake na biashara za uchumi wa bluu.

Uwekezaji huo wa EIB utasaidia ukuaji wa biashara, kuchangia usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na kuwezesha kampuni za uchumi wa bluu kuwekeza katika siku zijazo bora.