Vale awachorea ramani vijana kuhusu kilimo
Muktasari:
- Baadhi ya vijana wanadhani kilimo ni kazi ya kuchosha, yenye kipato kidogo na isiyoweza kumwezesha kijana kufikia ndoto zake za mafanikio
Dar es Salaam. Kwa miaka mingi, vijana wengi wa Tanzania wameendelea kuamini kilimo ni shughuli ya watu waliokosa fursa nyingine za maisha.
Kwa baadhi yao, kilimo ni kazi ya kuchosha, yenye kipato kidogo na isiyoweza kumwezesha kijana kufikia ndoto zake za mafanikio.
Lakini mtazamo huo unaanza kubadilika taratibu kutokana na vijana wachache waliothubutu kuingia kwenye sekta hiyo na kuthibitisha kuwa, kilimo kinaweza kuwa njia ya kujenga maisha bora, biashara kubwa na hata kutimiza ndoto ambazo wengi hudhani haziwezekani.
Miongoni mwa vijana hao ni Valentine Gabriel Moi (25) maarufu mtandaoni kama Vale Nafaka, mfanyabiashara wa mazao, mkulima na mhamasishaji wa vijana ambaye amegeuza uzoefu wake katika masoko ya mazao kuwa darasa linalowasaidia mamia ya vijana kuona fursa zilizopo kwenye kilimo.
Vale anaongoza programu mbalimbali za mafunzo ya kilimo na biashara ya mazao kupitia kampuni yake ya Valen Nafaka Group. Lakini safari yake haikuanza na mtaji mkubwa wala urithi wa biashara.
Vale anasema changamoto kubwa inayowazuia vijana kuingia kwenye kilimo si ukosefu wa fursa, bali ukosefu wa taarifa sahihi na hofu.
Binti huyo aliyezaliwa Februari 14, 2002 huko Sombetini jijini Arusha anasema sekta ya kilimo bado ina nafasi kubwa kwa vijana kwa sababu ushindani wa rika lao ni mdogo ukilinganisha na sekta nyingine.
"Kama huna mtaji, huna ardhi au hata huna kazi, usifikiri umefikia mwisho wa safari. Kilimo kinaweza kuwa mwanzo mpya," anasema Vale ambaye ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia ya watoto watatu wa Gabriel Moi ambaye kiasili naye ni mkulima.
Anasema ingawa yeye alipata mwamko kutoka kwa familia ambayo ililima kilimo cha kienyeji, anasisitiza umuhimu wa vijana kutafuta maarifa, kujifunza kutoka kwa waliowatangulia na kuwa tayari kuanza na kidogo walichonacho.
Pia, anawatahadharisha vijana dhidi ya kujenga dhana kwamba mafanikio yanapatikana kwa njia za mkato.
"Kwenye kilimo hakuna ubishoo. Lazima ushuke chini, ujifunze, ufanye kazi na uwe tayari kuchafuka," anasema Vale akisisitiza kuwa hakuna sapoti aliyoipata kutoka kwa familia bali ailijituma kwa maarifa na nguvu zake.
Kwa mtazamo wake, anasema miaka ya ujana ndiyo muda sahihi wa kujenga msingi wa maisha.
"Kuanzia miaka ya ishirini hadi thelathini ndiyo kipindi muhimu cha kujenga ndoto zako. Ukikitumia vizuri unaweza kutengeneza msingi wa maisha yako yote."
Vale akiwa katika moja ya shamba la Mpunga lililopo mkoani Mbeya
Mwanzo wa safari akiwa na miaka 16
Vale anasema mapenzi yake kwa biashara ya mazao yalianza zaidi ya miaka minane iliyopita alipokuwa akisubiri kuanza masomo ya sekondari ya juu.
Badala ya kutumia likizo nyumbani, alipata nafasi ya kufanya kazi kwenye mazingira ya maghala ya mazao. Akiwa na umri wa miaka 16 pekee, alianza kujifunza namna biashara ya nafaka inavyoendeshwa.
"Nilikuwa nafanya kazi ofisini lakini kila siku nilikuwa najifunza namna biashara nzima inavyofanyika. Nilikuwa na uwezo wa kuelewa vitu haraka na baada ya muda nikaanza kuamini kwamba hiki ndicho kitu ninachotaka kufanya maisha yangu yote," anasema.
Baada ya kuhitimu kidato cha sita na kuhamia Dar es Salaam kwa ajili ya masomo ya chuo, hakukutana na mazingira mepesi.
Anasema hakukuwa na ndugu wala mlezi wa biashara wa kumshika mkono, alilazimika kuanza upya.
Anasema aliingia sokoni, akajifunza taratibu za biashara za jiji kubwa na kujenga mahusiano na wafanyabiashara waliokuwepo kabla yake.
Vale akiwa katika ghala la mazao, licha ya kufanya shughuli za kilimo pia amewekeza katika uhifadhi wa mazao
Gunia nne zilizobadili maisha
Wakati vijana wengi walikuwa wakisubiri ajira rasmi baada ya masomo, Vale alianza biashara yake kwa gunia nne tu za maharage.
Anasema biashara ya mazao si rahisi kwa mtu mwenye mtaji mdogo kwa sababu mnyororo wake ni mrefu kuanzia shambani, usafirishaji, uhifadhi hadi kufika sokoni.
"Faida inakuwa ndogo mwanzoni kwa sababu unapitia gharama zilezile kama mfanyabiashara mkubwa. Lakini nilikuwa tayari kuvumilia na kujifunza," anasema Vale.
Kilichomsaidia zaidi hakikuwa fedha bali uaminifu na uwezo wa kujenga uhusiano na watu.
"Mimi sikuanza na mtaji wa pesa. Mtaji wangu ulikuwa ni akili, uwajibikaji na kujitolea. Nilitumia muda mwingi kujifunza kuliko kutafuta faida."
Kadri alivyoendelea kujifunza, alitambua kuwa kilimo na biashara ya mazao vina fursa nyingi zaidi ya kununua na kuuza mazao.
Vale akiwa katika moja ya shamba la Mpunga lililopo mkoani Mbeya
Mitandao ya kijamii ilivyofungua milango
Mabadiliko makubwa yalikuja alipoanza kushirikisha safari yake kupitia mitandao ya kijamii, hususan Instagram.
Kupitia video, picha na mafunzo aliyokuwa akitoa, vijana wengi walivutiwa na kile alichokuwa akikifanya.
Alianza kutoa mafunzo ya bure kuhusu biashara ya mazao mwaka 2024. Wakati mwingine alikuwa akitumia siku nzima kuwafundisha vijana bila malipo yoyote.
"Ninapenda kufundisha. Niliona vijana wengi wanataka kuingia kwenye kilimo lakini hawajui waanzie wapi. Nikaanza kuwapa maarifa bure."
Anasema amefundisha zaidi ya watu 1,000 kupitia programu mbalimbali zikiwemo Vale Nafaka Masterclass, Masokoni Tour, Mashambani Tour, Kilimo Tour na Mavuno Tour.
Programu hizo zimekuwa daraja kwa vijana, wafanyakazi na wawekezaji wanaotaka kujifunza kilimo, biashara ya mazao au uhifadhi wa nafaka.
Kutoka maharagwe hadi mpunga
Ingawa alianza na biashara ya maharagwe ya njano, baadaye alijikuta akivutiwa zaidi na biashara ya mpunga na mchele.
Anasema maharagwe ya njano yana soko kubwa nchini kutokana na matumizi yake katika kaya nyingi na migahawa.
Baada ya kuelewa biashara hiyo vizuri, alihamia kwenye mnyororo wa thamani wa mpunga.
Hata hivyo, anasema kilimo cha mpunga kinahitaji muda mwingi wa kusimamia shughuli za shambani jambo ambalo lilikuwa changamoto kwake kutokana na kuwa na shughuli nyingi zinazomlazimu kusafiri mara kwa mara.
Badala ya kujikita zaidi kwenye uzalishaji, aliamua kuwekeza katika kununua mpunga wakati wa mavuno na kuuhifadhi kwa ajili ya kuuza baadaye.
"Hiyo ndiyo njia ambayo imekuwa bora zaidi kwangu kutokana na aina ya shughuli ninazofanya."
Vale akiwa katika moja ya shamba la Mpunga lililopo mkoani Mbeya
Mbegu bora zilivyobadilisha maisha ya wakulima
Vale anasema maendeleo ya utafiti wa mbegu za mpunga yameleta mapinduzi makubwa katika uzalishaji.
Anatoa mfano wa maeneo ambayo zamani mkulima alipata wastani wa magunia manane kwa ekari moja, lakini sasa kutokana na matumizi ya mbegu bora na teknolojia za kisasa, baadhi ya wakulima wanavuna kati ya magunia 35 hadi 40 kwa ekari.
Anasema ongezeko hilo la uzalishaji limevutia wawekezaji wengi katika maeneo ya uzalishaji wa mpunga.
Mbali na wakulima kunufaika, biashara nyingine kama usafirishaji, uhifadhi, usindikaji na uuzaji wa pembejeo zimeongezeka.
"Kilimo kina uwezo wa kukuza uchumi wa eneo zima. Watu wanapata ajira, biashara zinaongezeka na miji inakua kwa kasi."
Kwa mtazamo wake, taswira ya mkulima maskini inaendelea kupoteza nguvu.
"Matajiri wengi waliopo vijijini wamejengwa na kilimo. Tofauti ni kwamba wengi wao hawapendi kuonesha maisha yao kama ilivyo mijini."
Vale akiwa katika ghala la mazao, licha ya kufanya shughuli za kilimo pia amewekeza katika uhifadhi wa mazao
Ndoto bado inaendelea
Licha ya mafanikio aliyoyapata, Vale anasema bado hajafika anapotaka kufika.
Anasema mafanikio yake makubwa si kiasi cha fedha alichonacho bali uwezo wa kugusa maisha ya vijana wengi kupitia mafunzo na ushauri anaoutoa.
Kupitia shughuli zake za kilimo na biashara ya mazao, tayari amewekeza katika mashamba makubwa mkoani Manyara na anaendelea kupanua shughuli zake za uzalishaji.
Ndoto yake kubwa ni kuona vijana wengi zaidi wakiingia kwenye kilimo cha kisasa, kujenga biashara zao na kutumia sekta hiyo kama daraja la kufikia malengo yao.
"Kilimo si ndoto. Kilimo ni njia ya kufikia ndoto. Ukikipa nafasi, kinaweza kukufikisha mbali kuliko unavyofikiria."
Kwa kizazi kinachoendelea kutafuta fursa za ajira na kujitegemea, simulizi ya Vale ni ushahidi kwamba wakati wengine wanaona shamba kama eneo la jasho na uchovu, wengine wanaona mahali pa kujenga maisha, biashara na mustakabali wa Taifa.