Vivutio vyakuza uwekezaji Tanzania

Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Gilead Teri akimkabidhi Mwenyekiti wa ES Health Africa Pvt Limited ya India, Yash Shah cheti vya vivutio kwa mradi ya ubia wa uwekezaji kati ya taasisi hiyo na hospitali ya Tanzanite ya Mwanza. Kushoto ni Mwenyekiti wa Hospitali ya Tanzanite, Jared Awando.

Muktasari:

  • Kituo cha Uwekezaji (TIC) kimesisitiza uwekezaji wa ubia, ili kukuza biashara nchini.

Dar es Salaam. Wakati vivutio vya uwekezaji na mazingira mazuri ya biashara vikitajwa kuchangia ongezeko la uwekezaji kwa asilimia 61 kutoka Septemba hadi Desemba 2023, Kituo cha Uwekezaji (TIC) kimesisitiza uwekezaji wa ubia, ili kukuza biashara.

Hayo yameelezwa leo Aprili 12, 2024 na Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Gilead Teri alipokuwa akiwasilisha cheti cha vivutio kwa mradi wa ubia ya uwekezaji kati ya hospitali ya Tanzanite ya Mwanza na ES Health Africa Pvt Limited ya India iliyowekeza dola 5 milioni nchini.

Teri amesisitiza kwamba uwekezaji wa pamoja una nafasi muhimu katika kuboresha huduma mbalimbali ndani ya nchi.

"Tumeshuhudia maendeleo makubwa katika miradi ya uwekezaji wa pamoja iliyoanzishwa na Watanzania na wageni, ikionyesha dhamira ya serikali ya kuimarisha uwekezaji wa Kitanzania kwa kufanikisha ushirikiano na wawekezaji wa kigeni. Tunatoa pongezi zetu kwa hospitali hii kwa kutambua na kuchukua fursa hii

"Kituo hiki kinatoa fursa kwa ushirikiano wa maendeleo ya miradi au biashara za ndani, ufahamu unaokuwa ndani ya sekta ya afya unaonekana, na kwa sasa tunajadili na hospitali ya saratani huko Mauritius kufanya utafiti wa miradi ya pamoja na hospitali ya ndan," amesema Teri.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Hospitali ya Tanzanite, Jared Awando, amesema: "Hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan aliingiza utalii wa afya, hivyo tulipata mwaliko kutoka TIC kutembelea India. Kupitia ziara hiyo, tumepata ushirikiano utakaoimarisha huduma zetu za afya."

Ameendelea kueleza kwamba baada ya kusaini mikataba Januari mwaka huu, kundi la madaktari wataalamu wa tisa kutoka India wamefika nchini tangu Alhamisi wiki hii, hawa wataalamu watatoa huduma mbalimbali ambazo hapo awali zilikuwa zinapatikana nje ya nchi, na sasa zinapatikana kwa urahisi ndani ya nchi.

"Mshirika wetu amewekeza Dola milioni tano za Marekani na yuko tayari kushirikiana nasi. Kuanzia wiki ijayo, madaktari wataanza huduma zao. Ni vyema kutambua kwamba Watanzania mara nyingi hutumia pesa nyingi kutafuta matibabu nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na gharama za malazi. Kwa hivyo, tumekataa kuleta huduma hizi nchini kwetu, ili ziweze kupatikana kwa urahisi na bei nafuu," amesisitiza.

Wakati huo huo, mwenyekiti wa ES Health Africa Pvt Limited ya India, Yash Shah, amebainisha kuwa tayari wametumia nusu ya uwekezaji wao kununua vifaa vya matibabu na kutekeleza teknolojia.

Ameeleza nia yao ya kuwekeza zaidi nchini Tanzania, ili kuboresha ubora wa huduma za afya, kuondoa haja ya wananchi kusafiri nje ya nchi kwa matibabu.

"Kwa kutoa huduma kwa kiwango cha ndani, tunachangia katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Kuelekea mbele, tunazingatia kupanua huduma zetu katika mikoa mingine mwaka ujao na kuhamasisha zaidi ya uwekezaji nchini Tanzania," ameeleza.