Uwekezaji wapaa, nchi tatu zikiongoza

Muktasari:

  • Ripoti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) inaonyesha mtaji wa Sh1.807 trilioni uliwekezwa katika mwaka ulioishia Januari, 2024.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikishuhudia ukuaji wa uwekezaji wa zaidi ya mara tatu katika mwaka ulioishia Januari 2024 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, China, Mauritius na India ni nchi vinara kwa kuweka fedha nyingi kupitia uwekezaji wa moja kwa moja.

Ripoti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) inayoakisi uwezekaji uliofanywa Januari nchini, inaonyesha mtaji wa Sh1.807 trilioni uliwekezwa katika mwaka ulioishia Januari ikilinganishwa na Sh314.324 bilioni zilizowekezwa Januari 2023.

Kukua kwa ongezeko la mitaji kumechangiwa na ongezeko la miradi iliyowekezwa katika kipindi hicho iliyofikia 52 ikilinganishwa na 23 ya mwaka uliotangulia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 51.92 ya uwekezaji wote uliofanywa Januari 2024 ulikuwa wa moja kwa moja kutoka nje.

Hiyo ikiwa na maana Sh554.499 bilioni zilikuwa za uwekezaji wa nje, kati yake China, Mauritius na India ziliwekeza Sh319.477 bilioni, huku uwekezaji huo ukilenga zaidi sekta ya viwanda, kilimo na usafirishaji.

Sekta hizo tatu pekee zilibeba mtaji wa Sh396.77 bilioni uliotoka nje ya nchi, sekta nyingine zinazobakia zikiambulia kiwango kidogo.

Uwekezaji uliofanywa na nchi hizo tatu si mara ya kwanza, kwani hata kipindi kama hicho mwaka uliotangulia ndizo zilikuwa nchi vinara lakini tofauti ni kiwango kilichokuwa kimewekezwa kati ya nchi na nchi.

Akizungumzia kukua kwa ongezeko hilo la uwekezaji, mchambuzi wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Katoliki Mbeya, Dk Balozi Morwa amesema ni vyema kadri miradi ya uwekezaji inapoongezeka basi inaleta ahueni ya kodi kwa wananchi wa chini.

Hilo ni kutokana na alichoeleza kuwa, miradi hiyo huleta fedha nyingi za kigeni zinazoweza kuchochea ukuaji wa uchumi na kuifanya nchi kuwa na akiba ya kutosha.

“Sisi kiuchumi tunaambiwa kuwa jinsi vitega uchumi vinavyoongezeka ahueni ionekane hadi kwenye ajira, lakini hazionekani; kodi zinaendelea kuanzishwa wakati kampuni zinazokuja ni kubwa zinaweza kulipa kodi jambo litakalopunguza mzigo kwa wananchi,” amesema Dk Morwa.

Akisema hayo, ripoti  inaeleza ajira 7,220 zinatarajiwa kupatikana kupitia miradi 52 ikilinganishwa na ajira 1,937 za  mwaka uliotangulia.

Kati ya miradi iliyowekezwa Januari 2024, sekta ya usafirishaji ilibeba takribani nusu ya mtaji wote.

Hiyo ikiwa na maana kuwa zaidi ya Sh598.72 bilioni zitaenda kutekeleza miradi 16 katika sekta hiyo, inayotarajiwa kutengeneza ajira zaidi ya 2,379 itakapoanza kufanya kazi.

Sekta ya uzalishaji wa viwanda ilifuata kwa kuwa na mtaji wa Sh280.25 bilioni iliyoelekezwa katika miradi 25 itakayotengeneza ajira 3,584 itakapokamilika.

Hata hivyo, katika miradi 52 iliyosajiliwa Januari 2024, 30 inapatikana ndani ya Jiji la Dar es Salaam ambayo mtaji wake ni Sh687.9 bilioni.

Mbali na asilimia 51.92 ya miradi yote kuwa ya wageni, asilimia 32.69 ni ya wawekezaji wazawa na asilimia 15.38 ni ya ubia kati ya wawekezaji kutoka nje na wawekezaji wa ndani