Kilimo chatamba ongezeko miradi ya uwekezaji nchini

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo

Muktasari:

  • Wakati thamani ya fedha zinazowekezwa katika miradi mbalimbali ikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 mwezi Agosti ikilinganishwa na Julai, kilimo kimezidi kutamba kwa kubeba fedha nyingi zaidi.
     

Dar es Salaam. Wakati thamani ya fedha zinazowekezwa katika miradi mbalimbali ikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 mwezi Agosti ikilinganishwa na Julai, kilimo kimezidi kutamba kwa kubeba fedha nyingi zaidi.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ya Agosti mwaka huu, uwekaji katika miradi mbalimbali ulikuwa zaidi ya Sh2.33 trilioni, Agosti mwaka huu ikilinganishwa na Sh1.06 trilioni iliyokuwapo Julai mwaka huu.

Ongezeko la fedha hizo linabainishwa katika ongezeko la miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa nchini kutoka 40 Julai mwaka huu hadi miradi 58 Agosti 2023.

Wakati fedha zilizowekezwa zikiongezeka, thamani ya uwekezaji unaofanywa katika kilimo imeongezeka kwa zaidi ya Sh275.53 bilioni kwa Agosti, ikilinganishwa na kiwango kilichowekezwa Julai mwaka huu.

Ripoti hiyo iliyotolewa wiki iliyopita inaonyesha kuwa uwekezaji katika kilimo umeongezeka hadi Sh849.13 bilioni Agosti uliopita kutoka Sh571.10 bilioni mwezi uliotangulia.

Kukua kwa uwekezaji huo kunakwenda sambaamba na kuongezeka kwaidadi ya miradi inayosajiliwa katika kilimo.

Wakati miradi mitatu pekee ndiyo ilisajiliwa TIC Julai mwaka huu, kumekuwa na ongezeko la hadi miradi 10 Agosti mwaka huu, sawa na mara tatu.

Miradi hiyo ni kati ya miradi 58 iliyosajiliwa Agosti mwaka huu ambayo imebeba uwekezaji wa zaidi ya Sh2.331 trilioni ambayo inatarajia kutengeneza ajira 25,731.

Akizungumzia suala hilo, Profesa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abel Kinyondo alisema ongezeko la uwekezaji katika kilimo linatokana na Serikali ya sasa kuipa kipaumbele sekta hiyo.

"Sekta ya kilimo kwa sasa ndiyo lengo kuu (la Serikali) na bajeti yake imekuwa ikiongezeka katika miaka ya hivi karibuni," alisema Profesa Kinyondo.

Kwa mwaka 2022/23 Bajeti ya Wizara ya Kilimo imepanda kutoka Sh751.12 bilioni hadi Sh970.78 bilioni mwaka 2023/24, sawa na ongezeko la asilimia 29.24.

Kinyondo alisema uwekezaji huo unaenda sambamba na kampeni mbalimbali ikiwemo ile inayohamasisha usalama (uhakika) wa chakula ambazo zinaweza pia kuchangia kuongezeka kwa uwekezaji.

Wakati huohuo, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Haji Semboja alisema Tanzania inatambulika ulimwenguni kwa sababu ya uwezo mkubwa wa kufanya vyema katika sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuwa ardhi kubwa inayofaa kwa sekta hiyo kuliko nchi nyingine.

"Sekta ya kilimo ina sera, sheria na taratibu zinazowavutia wawekezaji," alisema Profesa Semboja.

Mbali na eneo la kilimo, ripoti inataja uwekezaji katika majengo ya biashara kuwa ndiyo ulifuata kwa kubeba fedha nyingi, ambapo zaidi ya Sh765.293 bilioni ziliwekezwa Agosti mwaka huu.

Usafirishaji pia ulibeba zaidi ya Sh302.616 bilioni huku sekta nyingine zikiwa ni utalii, viwanda, miundombinu ya kiuchumi na huduma zikifuatia.

Katika uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje, China inaongoza kwa kuwekeza fedha nyingi ikiwa na mtaji wa zaidi ya Sh1,055 trioni, ikifuatiwa na Mauritius iliyowekeza zaidi ya Sh60.023 bilioni.

Sekta ya majengo

Majengo ya biashara yametajwa na ripoti hiyo kuwa yalikuwa kipaumbele kwa kupewa fedha nyingi zaidi na wageni, yakifuatiwa na huduma na viwanda.

Kwa upande wa wawekezaji wazawa kipaumbe kilikuwa kwenye kilimo, usafirishaji na miundombinu ya kibiashara.

Hivi karibuni Waziri wa Uwekezaji na Mipango, Profesa Kitila Mkumbo aliwakaribisha wawekezaji kwa wingi akitaja eneo la uongezaji thamani ya mazao kuwa lina fursa ya uhakika.

"Wakati bidhaa za mafuta ya kula, ngano na sukari zikiingizwa zaidi kutoka nje, hapa nchini tuna malighafi na ardhi ya kufanya kilimo. Ni fursa ambayo inaweza kutumika vizuri na ya uhakika" alisema Profesa Mkumbo wakati akizungumza katika mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika 2023 (AGRF).

TIC sasa kidijitali

Ili kutoa urahisi katika uandikishaji wa miradi, TIC imeanzisha mfumo unaotoa huduma zake kwa wawekezaji kwa njia ya kielektroniki, ambao pia utaunganisha taasisi nyingine zinazohusika.

Mfumo huo katika awamu ya kwanza utajumuisha taasisi saba ikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara (Brela), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Wizara ya Ardhi, Kamishna wa kazi, Idara ya Uhamiaji.

Mkurugenzi wa Idara ya Uhamasishaji Uwekezaji TIC, John Mnali anasema lengo la kutengenezwa kwa mfumo huo ni kurahisisha utoaji wa vibali na leseni mbalimbali zinazohitajika na wawekezaji.

"Kabla ya kuunganika, kila taasisi ilikuwa na mfumo wake lakini katika maboresho haya taasisi hizi zimeunganisha mifumo y TIC ambayo inatumika katika kuwasajili wawekezaji na kutoa vibali na leseni mbalimbali wanazozihitaji," alisema Mnali.

Mnali alisema mfumo huo unamrahisishia mwekezaji na kumpunguzia muda wa kupata vibali na leseni mbalimbali.

"Kwa awamu ya kwanza kupitia mfumo huo mwekezaji atakuwa anaingia kwenye mfumo mmoja na atakapoanza usajili wa kampuni ataendelea kuomba vibali na leseni mbalimbali kupitia mfumo uleule mmoja"

"Zile taarifa za awali ambazo mwekezaji atakuwa amezitoa kuhusiana na jina au mmiliki wa kampuni pia zitapatikana na taasisi zingine zote za Serikali bila kulazimika kila wakati kutoa taarifa zilezile kama ilivyokuwa kabla ya mfumo huu," alisema.

Alisema hivi sasa baadhi ya wawekezaji wapo nje ya nchi, wanapohitaji huduma hizi za kuweza husaidiwa kupata vibali na leseni mbalimbali kwa kufanyiwa na kampuni za ndani, hivyo wataweza kusajili wenyewe wakiwa hukohuko.