TIC yasajili miradi 1, 200 ikiwemo ya kilimo

Pendo Gondwe Muwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) baada ya kutoa elimu ya uwekezaji kwa wananchi wa mkoa wa Simiyu. Picha na Samirah Yusuph.

Muktasari:

kwa kipindi cha miezi sita miradi 19 ya kilimo yenye thamani ya dola 134 milioni imesajiliwa ambayo inatarajiwa kutoa ajira 6,044  ikiwa ni baada ya kuboreshwa kwa sheria ya usajili wa miradi ambayo imepunguza kiwango cha mtaji kutoka dola 100,000 hadi dola 50,000.

Bariadi. Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) kimesajili miradi 1,200 kati ya hiyo 74 ikiwa ni ya kilimo ndani ya kipndi cha mwaka mmoja.

Hatua hiyo inatajwa ni kutokana na mwitikio mkubwa wa wawekezaji wazawa kuanzia kipindi cha Novemba 2022 hadi Juni 2023 mwaka huu.

Akitoa elimu kwa wakulima wa Mkoa wa Simiyu kuhusu umuhimu wa kusajili miradi, Ofisa Uhusiano kwa Umma wa Kanda wa TIC, Pendo Gondwe amesema wanapaswa kuongeza thamani ya mazao yao kwa kuanzisha viwanda vya usindikaji.

Mazao makuu ya mkoa huo ni pamba, alizeti, mahindi na mazao ya jamii ya mikunde hivyo ili kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara ni lazima viwepo viwanda vya usindikaji kumuwezesha mkulima apate tija ya kilimo kwa kuuza mazao yake kiwandani.

“Ili Mtanzania aweze kusajiliwa sio lazima awe na mtaji mkubwa kama awali kwa sasa wanaweza kuja kusajiliwa na mtaji wa dola 50,000 (Sh124.7 milioni)  tofauti na awali ilipokuwa dola 100,000 (249.4 milioni),” amesema Gondwe

Ameongeza kuwa tangu kupunguzwa kwa kiwango cha mtaji Novemba mwaka jana, kipindi cha miezi sita miradi 229 ya kilimo imesajiliwa ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 100 ikilinganishwa na mwaka 2020/21 ambapo kwa mwaka mzima miradi 250  pekee ilisajiliwa.

"Kwa sasa usajili wa miradi kielectronic umerahisisha wawekezaji wengi kujisajili na tunaelekea kuboresha na kuwa na kituo kimoja cha usajili ambapo kitamuwezesha muwekezaji kufanya usajili na kupata cheti cha kuthibitishwa kupitia mfumo jambo ambalo  litaondoa usumbufu kwa wawekezaji kuja ofsini na kuwavutia kusajiri miradi kwa njia ya mtandao,” amesema

Wakizungumza baada ya elimu iliyotolewa baadhi ya wafanyabiashara na wakulima wamesema kuwa kituo hicho kinatakiwa kutoa elimu ya kutosha kwa sababu wengi hawafahamu umuhimu kwa kupandisha thamani mazao.

Kingolo Nyanda Mkazi wa Bariadi, amesema "mfano leo ndio nimejua kuwa ukiwa na kiasi gani unaweza kusajili mradi, tunawaomba kituo hiki kuweza kuwatembelea wakulima wakubwa na kuwapa elimu.”

Mkazi mwingine wa Salunda, Anthony Nyese amesema iwapo elimu hii itatolewa hadi ngazi ya chini katika vijiji huenda ikapunguza adha ya wakulima kuuza mazao yao kwa bei ndogo kwani kutakuwa na viwanda vingi vinavyohitaji malighafi kwa ajili ya uzalishaji.