Viwanda vya kubangua korosho mbioni kujengwa Tanzania

What you need to know:

Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe amewatangazia neema wakulima wa korosho mkoani Mtwara wakati akieleza kuhusu mpango wa Serikali wa kuongeza thamani ya zao hilo kabla ya kusafirishwa.



Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe amewatangazia neema wakulima wa korosho mkoani Mtwara wakati akieleza kuhusu mpango wa Serikali wa kuongeza thamani ya zao hilo kabla ya kusafirishwa.

Bashe ambaye yupo katika ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani humo amesema Serikali iko mbioni kujenga viwanda vya kubangua korosho.

Amesema lengo la ujenzi wa viwanda hivyo ni kuhakikisha korosho zote zinazolimwa ndani ya mkoa huo zinabanguliwa kabla ya kusafirishwa

Akizungumza katika kijiji cha Nanguruwe ambapo msafara wa Rais ulisimama kuwasalimia wananchi, Bashe amesema tayari eneo la ujenzi wa viwanda hivyo limeshapatikana katika kijiji cha Maranje.

“Kufikia 2025/2026 korosho yote itabanguliwa Mtwara na eneo la ubanguaji litakuwa kijiji cha Maranje, Serikali imeshaanza kulipa fidia eneo la ukubwa wa ekari 1500 na linaanzwa kusafishwa Novemba  mwaka huu ili ujenzi wa viwanda.

Kwahiyo Oktoba 2025 tutakapoanza kuvuna korosho za msimu wa mwaka huo, tani laki moja za kwanza zitaanza kubanguliwa Maranje na tutaanza kukamua mafuta ya korosho na bei itaimalika na soko litakuwa la uhakika na sio kusubiri kudra za Mungu au wale watu kutoka Vietnam wanaotupangia bei.

Mbali na hilo Bashe amesema Serikali imeweka mikakati ya kuyapa kipaumbele mazao ya mbaazi na ufuta, katika msimu ujao wa kilimo Bodi ya Korosho itahusika pia kusimamia mazao hayo.

“Msimu ujao tunabadilisha kanuni za bodi ya korosho ili kumpa mamlaka mkurugenzi wa bodi ya kusimamia mazao ya mbaazi na ufuta kwa kuwa nayo ni ya mazao ya biashara.

“Hii ina maana kwamba kama ambavyo tunagawa miche ya korosho bure kwa wakulima tutagawa pia mbegu za mbaazi na ufuta ili mazao haya yapate thamani na kuleta tija kwa mkulima,” amesema Bashe.