Soko jipya la korosho lafunguliwa Marekani

Muktasari:

  • Wakati korosho zilizofungwa katika vifungashio vidogo zikianza kusafirishwa kwenda nchini Marekani kwa mara ya kwanza, hatua hiyo imetajwa italisaidia Taifa kufikia malengo ya kuzalisha tani 700,000 za korosho mwaka 2025/26.

Unguja. Wakati korosho zilizofungwa katika vifungashio vidogo zikianza kusafirishwa kwenda nchini Marekani kwa mara ya kwanza, hatua hiyo imetajwa italisaidia Taifa kufikia malengo ya kuzalisha tani 700,000 za korosho mwaka 2025/26.

 Kwa takwimu za mpaka mwaka jana, uzalishaji korosho nchini ni tani 240,000, wakati viwanda vilivyopo vina uwezo wa kubangua tani 64,000, huku mahitaji ya soko yakitajwa kuwa makubwa.

Hayo yalibainishwa na mkurugenzi mkuu wa bodi ya korosho Tanzania, Francis Alfred wakati wa kuzindua usafirishaji wa kontena la tani 750,000 za korosho zilizofungwa kwenye vifungashio vidogo kutoka Zanzibar kwenda Marekani. Korosho hizo zinasafirishwa na kampuni ya Ward Holding Tanzania (WHT). “Mahitaji ya korosho ulimwenguni ni makubwa, changamoto ambayo tumekuwa nayo tumekuwa tukibangua kiasi kidogo, kwa hiyo tukiwa na wabanguaji wengi tutapata wanunuzi wengi zaidi, kikubwa ni kuzalisha bidhaa zetu kwa viwango vya kimataifa na vinavyohitajika,” alisema.

Alisema Tanzania kuzindua kuuza korosho katika masoko ya rejareja ni hatua ambayo wamekuwa wakiwiwa kuifikia, hivyo itasaidia mpango wa kuzalisha tani hizo.

Alisema kupanua wigo wa kuuza korosho zilizofungashwa kwenye vikasha itaongeza mnyororo wa thamani, kuongeza pato la Taifa, wakulima na kuongeza ajira.

Hata hivyo, aliwataka wabanguaji wa korosho kushirikiana, ili Taifa lifikie malengo yake kuuza katika masoko ya nje, akisema bodi itatoa ushirikiano wote.

Kwa upande wake, Rais wa WHT, Godfrey Simbeye alisema pamoja na Tanzania kujaribu kwenda kwenye masoko mengi ya korosho, lakini haikuwahi kufanikiwa kulifikia soko la Marekani, hivyo hatua hiyo ni historia kwa Taifa na kufungua fursa mpya ya soko la korosho.

“Hata masoko tuliyokwenda ni kupeleka makasha makubwa maupe, si makasha madogo ya mlaji wa mwisho kama haya,” alisema.

Alisema kilo moja ya korosho hizo inauzwa dola 40 (Sh93,280) nchini Marekani.

Kuhusu korosho hizo kusafirishiwa Zanzibar licha ya kulimwa na kubanguliwa Mtwara, Simbeye alisema kiwanda pekee ambacho kimetengeneza vifungashio vya korosho hizo kimepatikana Zanzibar. Mkuu wa masoko wa kimataifa, Valentine Mugendi alisema maandalizi ya kupokea kontena hilo Marekani yanaendelea New Orleans na sherehe hizo chini ya kaulimbiu ya TanzaFest zitafanyika Novemba, mwaka huu.