Waaswa kutumia nishati safi kupikia

Wajasiriamali wanaofanya biashara ya kuuza vyakula maarufu Mama Lishe, wakipata maelekezo ya namna ya kutumia moja ya majiko yanayotumia nishati safi.

Muktasari:

  • Wajasiriamali wanaofanya biashara ya kuuza vyakula maarufu Mama/Baba lishe wameaswa kutumia nishati safi kupikia ili kuokoa muda na kuongeza uzalishaji.

Dar es Salaam. Wajasiriamali wanaofanyabiashara ya kuuza vyakula maarufu mama/baba lishe, wameaswa kutumia nishati safi kupikia ili kuokoa muda na kuongeza uzalishaji.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Novemba 24, 2023 katika mafunzo yaliyotolewa kwa wajasiriamali hao kutoka maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, yakiwa na lengo la kuhamasisha kuachana na matumizi ya nishati isiyo safi ili kulinda afya za watumiaji, mazingira na kuinua uchumi.

Akieleza faida za matumizi ya nishati safi, Mhandisi wa Nishati Jadidifu na Mshauri kutoka Interfini Consultancy Limited, inayojihusisha na masuala ya biashara na miradi, Wilson Shoo amesema wengi hupenda kutumia nishati zisizo safi kwa kuogopa gharama bila kujua kwamba huko ndiko kuna gharama zaidi.

"Wengi wanaangalia hela tu, hawaangalii muda ambao ni muhimu zaidi kwenye uzalishaji. Unaweza kuwa unatumia hela kidogo lakini muda mwingi na pia afya inaathirika, tayari hapo umetumia gharama kubwa zaidi," amesema

Pia, Shoo amesema kuna hatari ya kupata madhara kiafya kutokana na matumizi ya nishati isiyo safi ambayo husababisha magonjwa na vifo vingi.

"Kwa Tanzania kila mwaka watu 33,000 hupoteza maisha kutokana na athari za matumizi ya nishati zisizo safi kupikia wakati duniani ni watu milioni 4 hupoteza maisha," amesema Shoo

Amesema matumizi ya nishati isiyo safi hutumia muda mrefu kupikia hivyo kumnyima muda mtumiaji muda wa ziada kufanya shughuli nyingine.

Aidha, Meneja Miradi kutoka shirika hilo, Pamela Mushi amesema mafunzo hayo ni hatua za kuunga mkono jitihada za Serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi kupikia kwa Watanzania.

"Mafunzo haya ni kwa ajili ya kutoa uelewa juu ya matumizi ya nishati safi kwa Watanzania, kujua ni wapi inapatikana lakini pia kufahamu changamoto zao," amesema Pamela.

Amesema waliamua kuwatumia mama/baba lishe kwani hutumia muda mwingi kwenye shughuli za upishi na kwamba ndio waathirika wa kwanza wa nishati isiyo safi kupikia.

Kwa upande wake, Asha Rajabu ambaye ni mama lishe eneo la Mwenge, amehudhuria mafunzo hayo ambaye pia hutumia kuni na mkaa katika shughuli zake amesema amejifunza umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

"Nashukuru kupitia mafunzo hayo, nimefahamu kwamba ziko nishati nyingine mbadala ambazo naweza kuzitumia katika shughuli zangu bila kuathiri afya yangu, mazingira na kutumia kiasi kidogo cha hela," amesema Aisha

Amesema kila siku hutumia mkaa wa kawaida wa Sh10, 000 ambayo ni gharama kubwa kuliko mkaa salama ambao akiutumia ataweza kutumia kiasi kidogo cha hela kuliko kile anachotumia sasa.

"Ningetamani kutumia umeme lakini eneo nilipo hakuna nishati hiyo maana nimefahamu kwamba si gharama kubwa tofauti na ambavyo watu wengi wamekuwa wakifikiri," amesema.

Pia, wadau mbalimbali wakiwemo wauzaji wa majiko ya nishati safi ya kupikia walipata fursa ya kuonyesha bidhaa zao na kutoa mafunzo ya namna ya kutumia majiko hayo na umuhimu wake.

Ripoti ya utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na viashiria vya Malaria (THDS) ya mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha ni asilimia 7 pekee ya Watanzania wanaotumia nishati safi.

Hata hivyo, Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi kupikia ifikapo mwaka 2033.