Nishati ya kupikia kuibua fursa za ajira

Viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wakiwa kwenye Kongamano la Kitaifa kuhusu Nishati Safi ya Kupikia lililofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar Es Salaam.

Muktasari:

Wadau wa nishati mbadala wamewatoa hofu wananchi wakisema mabadiliko ya kwenda katika nishati safi ya kupikia hayataathiri ajira zao bali yataibua fursa mpya zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi.

Dar es Salaam. Wadau wa mbalimbali nishati mbadala wamesema mabadiliko ya matumizi ya nishati safi ya kupikia hayataathiri ajira za wananchi zilizotokana na kuni na mkaa, badala yake yataibua fursa mpya zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi na kuendesha maisha yao.

Hofu ya kupoteza ajira kwa wananchi wanajishughulisha na kuni na mkaa kuuza na hatua hiyo wakati Serikali ikiendeasha mjadala wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia unaolenga kufanya mapinduzi ya katika sekta hiyo.


Leo Jumanne Novemba 2, 2022 wakichangia mada kuhusu 'fursa,  ajira na ujuzi katika mabadiliko ya kutumia nishati safi ya kupikia' wadau hao wamesisitiza kuwa  kuibuka kwa fursa mpya kutokana na mabadiliko kutoka nishati chafu kwenda nishati safi.

Mkurugenzi Mkuu wa Solution Tag, Peter Kichogo amesema mabadiliko yoyote yanakuja na fursa na zitapatikana endapo wananchi watazifuata.

Amesema ubunifu na fikra chanya ndio silaha muhimu katika kufanikiwa kuzifikia fursa zitakazotokana na mabadiliko ya matumizi ya nishati.

"Kuna haja ya kuwekeza katika kulielewa soko na mahitaji yake, kisha unahitajika ubunifu kulingana na fursa zilizopo," amesema.

Amesisitiza mabadiliko kutoka katika nishati zinazotumika kwenda kwenye nishati safi za kupikia yatazamwe kama fursa na si vinginevyo.


Kwa upande wake Meneja wa Nishati Endelevu ya Tungamotaka na Mabadiliko ya Tabianchi (TaTEDO), Mary Swai amekiri nishati zinazotumika hivi sasa kuwa msingi wa ajira za wengi nchini.

Katika ufafanuzi wake, amesema takwimu za mwaka 2014 zinaonyesha dola za Marekani 1 bilioni zinaingia nchini kutokana na shughuli za nishati hizo.

"Hatua hii inaashiria uwepo wa idadi kubwa ya watu wanaonufaika na matumizi ya nishati za mkaa na kuni ili kuwahamisha kutoka walipo sasa zinahitajika juhudi za hatua kwa hatua, badala ya kuwalazimisha kuachana nazo ghafla," amesema Swai.

Kuhusu fursa, amesema mabadiliko ya nishati ya kupikia hubadilisha hata vifaa vitakavyotumika, hivyo wabunifu watanufaika na utengenezaji wa vifaa hivyo yakiwemo majiko banifu.Amesema pia uuzaji na usambazaji ni fursa nyingine katika mabadiliko ya nishati hiyo, hivyo anayejishughulisha na ukataji mkaa atahamia kusambaza nishati safi.


"Kama watu wataangalia namna ya kutengeneza mkaa safi, tutapata fursa kuna majiko yanayotumika na mkaa huo safi hayapo nchini hiyo ni fursa pia,tunahitaji kutoa uelewa wa kutosha, utafiti katika sekta hii na tutafute taarifa ya ajira ngapi zitapatikana kwenye hili," amesema Swai.

Naye Mkurugenzi wa Masoko, Kampuni ya Teknolojia ya Gesi ya Anric, Mhandisi Mercy Chilumba amesema matumizi ya gesi yataibua fursa lukuki ikiwemo uwakala wa uuzaji wa vifaa vya nishati hiyo.Alisema kila kampuni kubwa ya gesi huwa na vituo vya kusambazia maeneo ambayo yanaibuka fursa za ajira kwa wananchi.

Mratibu wa Miradi ya Nishati na Mazingira, Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO), Victor Akim, ametolea mfano nishati inayotokana na molasisi kutoka katika viwanda vya sukari.Amesema nishati hiyo inayoitwa Bioethanol ni salama kwa kupikia na kuzalishwa kwake kunaibua fursa nyingi."Kwa kadri itakavyojulikana wengi watahamasika kuizalisha na hata wawekezaji watawekeza humo hii itakuja na fursa nyingi," amesema.

Akitoa mapendekezo kwa kikosi kazi kitakachoundwa kushughulikia suala hilo, Mtaalamu wa Misitu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Profesa Romanus Ishengoma amesema maboresho ya sera ni muhimu kufanyika.

Ingawa sera hiyo imetaja mambo mengi mazuri, lakini mwanazuoni huyo amesema haikuelekeza namna ya kuhama kutoka nishati inayotumika sasa kwenda kwenye Ile inayohitajika.

"Nahisi sera ile ikiwezekana inaweza kupitiwa na isipowezekana ipate msaada, kwa kawaida sera inasaidiwa na sheria na kanuni, lakini ndani ya sera hakuna sheria inayoongoza matumizi ya kuni na mkaa," amesema

Amesema kuna haja ya maboresho ya sera hiyo, alisema inatokana na ukweli kwamba miaka saba tangu ilipotungwa haikufanikisha kuwahamisha wananchi kutoka matumizi ya nishati chafu kwenda safi.

Profesa Ishengoma amesema kuna pia haja ya kutafutwa mbinu za kuzibadili nishati inayoonekana kuwa chafu na kuongeza kuwa safi.amesema katika  maboresho ya sera ni vema kutoa muelekeo wa kipindi cha mpito ambacho hakitakuwa kifupi juu ya namna ya nishati inayopaswa kutumika.