Rais Samia aagiza ukaguzi mto Ruvu

Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi pamoja na wananchi waliohudhuria kwenye kongamano la kitaifa kuhusu Nishati Safi ya Kupikia katika ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam Novemba 1, 2022.

Muktasari:

Rais Samia azungumzia hali ya maji Dar es Salaam na mipango ya kuhakikisha mkoa huo unakuwa na akiba ya maji ndani ya miaka mitano hadi sita kutoka sasa.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza wakuu wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kukagua maeneo yote yanayozunguka mto Ruvu na kuhakikisha vizuizi vyote zinavyozuia maji kuingia kwenye mto huo vimetolewa.

 Agizo hilo ambalo limewahusisha pia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) amelitoa leo Novemba Mosi 2022 wakati wa kongamano la kitaifa la nishati safi ya kupikia linalofanyika leo na kesho jijini Dar es Salaam.

Amesema licha ya ukame unaoendela nchini na kusababisha kupungua kwa maji katika mto huo, kuna uvamizi mkubwa wa shughuli za kibinadamu ambazo zinasababisha maji kupungua.

“Mgawo unaoendelea Dar es Salaam ni athari ya mabadiliko ya tabia nchi, kupungua maji katika mto Ruvu kwa kiasi kikubwa ni matendo yetu wenyewe binadamu. Watu wamevamia wanapeleka maji kwenye mashamba yao nendeni mkahakikishe mto uko salama.

“Pia miundombinu ya usambazaji maji Dar es Salama ni mikongwe, pengine mingine ilitengenezwa wakati kuna watu wachache leo kuna watu zaidi ya milioni tano. Dawasa na Wizara ya Maji waangalie namna ya kuiboresha ili maji yawafikie watu. Ukisoma kazi iliyofanywa mkoa huu unaweza kupata maji kwa asilimia 100 kuanzia mwakani,” amesema Rais Samia.

Kuhusu mkakati wa muda mrefu wa kukabiliana na changamoto ya maji katika Jiji hilo, Mkuu huyo wa nchi amesema tayari Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la Kidunda ambalo mkataba wake umesainiwa jana.

 “Mradi huu utachukua muda mrefu, ujenzi utamalizika baada ya miaka miwili na kujaa kwake ni kadiri mvua zitakavyokuwa zinanyesha hivyo tutegemee baada ya miaka mitano hadi sita mbele Dar es Salaam itakuwa na akiba kubwa ya maji,”.