Rais Samia ataka kikosi kazi cha nishati safi ya kupikia

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi pamoja na Wananchi waliohudhuria kwenye Kongamano la Kitaifa kuhusu Nishati Safi ya Kupikia katika ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam Novemba 1, 2022.

Muktasari:

Rais Samia ameagiza kuundwa kwa kikosi kazi kitakachotoa mwelekeo wa Taifa kutumia nishati safi ya kupikia.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuanzishwa kwa kikosi kazi kitakachoshughulikia nishati safi ya kupikia, lengo likiwa kuanzisha safari ya kulitoa Taifa kwenye matumizi ya nishati isiyofaa.

Kikosi kazi hicho ambacho hakitakuwa cha Serikali pekee, kitahusisha pia sekta binafsi na wadau wa maendeleo kitakuwa na kazi ya kuchambua sera za Serikali na mapendekezo ya wadau.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ndiye atakayeongoza kikosi kazi hicho kwa ngazi ya mawaziri ambapo uratibu utafanyika chini ya Wizara ya Nishati.

Rais Samia ametoa maelekeo hayo leo Novemba Mosi wakati wa kongamano la kitaifa la nishati safi ya kupikia linalofanyika leo na kesho jijini Dar es Salaam.

Amesema kikosi kazi hicho kitakuja na mpango mkakati ambao utaiongoza Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kutafuta suluhu ya nishati safi na endelevu ya kupikia.

Takwimu zinaonyesha kuwa kaya zinazopikia kwa kutumia mitungi ya gesi ni asilimia 5, umeme asilimia 3 na nishati nyingine safi asilimia 2.2.

“Hii inaonyesha bado kuna kazi ya kuhamasisha matumizi ya nishati iliyo safi na salama. Tunapaswa kuwa na mkakati madhubuti wa kisera na kibajeti pamoja na kuweka mazingira wezeshi katika kutatua changamoto za upatikanaji wa nishati safi.

“Kwenye hili Serikali peke yetu hatuwezi tunapaswa kwenda sambamba na sekta binafsi, nashukuru baadhi yao wameanza kujitokeza tunakwenda nao sambamba lakini si kisera kwa sababu ni fursa ya biashara hivyo kuna haja ya kuwa na sera inayoshughulikia suala hili,” amesema Rais Samia.