Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kuanza kuhifadhi sukari


Muktasari:

  • Ili kusaidia nchi kutoingia katika uhaba wa sukari kama ilivyokuwa mwaka 2023, Serikali imependekeza kufanyika kwa marekebisho kwenye Sheria ya Sukari, Namba 6 kama ili kuiwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua sukari na kuhifadhi

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imependekeza kufanyika kwa marekebisho kwenye Sheria ya Sukari, Namba 6 kama ili kuiwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuwa na uwezo wa kununua kuratibu na kuhifadhi pengo la sukari kwenye hifadhi ya chakula ya Taifa.

Lengo la hatua hii ni kuwezesha upatikanaji wa sukari nchini na kuondoa uhodhi kwa baadhi ya wenye viwanda bila kuathiri dhamira ya Serikali ya kulinda viwanda vya ndani.

Mapendekezo hayo yametolewa leo Alhamisi, Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati wa uwasilishaji wa Bajeti ya Serikali mwaka 2024/2025 iliyokuwa ikisomwa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.

Hatua hii inafikia ikiwa ni siku chache tangu Tanzania kujinasua katika uhaba wa sukari uliokuwa unaishumbua nchi jambo ambalo lilikuwa likitajwa kuchangiwa na mvua kubwa iliyoathiri uzalishaji.

Hali hiyo ilifanya bei ya sukari kupaa hadi kufikia Sh5,000 katika baadhi ya maeneo huku baadhi ya wafanyabiashara wakilazimika kuacha kuuza sukari kwa muda.

Kufuatia uwepo wa hali hiyo, Serikali kupitia Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) ilitangaza bei elekezi ambapo kilogramu moja ya sukari kwa wanunuzi wa rejareja ilitakiwa kuuzwa kati ya Sh2,700 hadi Sh3,200.

Akisoma mapendekezo hayo Bungeni jijini Dodoma, Dk Mwigulu amesema jambo hilo pia linalenga kufanya marekebisho kwenye kanuni ya NFRA kwa kuijumuisha sukari kuwa sehemu ya usalama wa chakula.

“Kutoza napendekeza kutoza Sh50 kwa kilo ya mabaki yanayotakana na uzalishaji wa sukari. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato yatakayoiwezesha Bodi ya Sukari kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuendeleza mafunzo na kukuza ujuzi katika sekta ya sukari,” amesema Dk Mwigulu na kuongeza

“Pia itaiwezesha bodi hiyo kusimamia uzalishaji wa sukari nchini kupitia upanuzi wa viwanda vilivyopo na kuhamasisha uwekezaji mpya,” amesema.