Wakulima wa vanila wapata wakala soko la nje

Zao la vanila likiwa shambani kabla ya kuvunwa. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Wakulima wa vanila nchini wameeleza kufurahia kupata wakala wa kusafirisha mazao yao kwenda sokoni, wakisema hatua hiyo itaongeza tija na thamani ya kilimo hicho.

Dar es Salaam. Wakulima wa zao la vanila nchini wamesema hatua ya kupatikana kwa wakala wa kusafirisha zao hilo kwenda nje ya nchi ni mageuzi mkubwa katika jitihada za kuwafikia wateja wao walioko mataifa makubwa.

Wakulima hao kwa sasa wamepata kampuni ya vifaa vya Kijerumani (DHL) itakayokuwa wakala kwa kutoa huduma kwa mfumo wa mtandao ili kuwafikia wakulima walioko mikoani wanaolima bidhaa hiyo na kuwapelekea sokoni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Dar es Salaam leo Januari 17, 2023  baada ya kumalizika kikao kilichoandaliwa na DHL kwa kuwakutanisha wakulima wa zao hilo nchini, wakulima hao wamesema licha ya kuongezeka kwa mwamko wa kulima zao hilo, bado walikuwa na changamoto kulifikia soko la uhakika.

“Tunachangamoto kubwa ya soko la uhakika kwa sababu kuna wakati soko lililopo linapanda na kushuka inakuwa shida kwetu na ni kwa sababu hatuna wanunuzi.

“Sasa DHL amekuja tunaamini itakuwa chachu ya kuongeza uzalishaji wa zao hili,” amesema Abdi Seweid mkulima kutoka Zanzibar.

Amesema bei ya vanila kwa kilomoja ni Sh1milioni lakini ilishuka hadi Sh250, 000 na kwa sasa inauzwa kwa kilo hadi Sh300,000.

“Sasa bei hiyo ni tatizo na tunaamini wakala huyo atatufanya kulifikia soko la dunia.”

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Masoko kutoka DHL, Caritas Ntaganda amesema kikao hicho kiliwakutanisha wakulima, wanunuaji na wasafirishaji kutoka mataifa mbalimbali na malengo yalikuwa kuwaelimisha wakulima kufanya biashara yao kwa njia mtandao.

“Tutakuwa tunawasaidia biashara yao kwa njia mtandao na wataweza kuongeza thamani ya bidhaa zao kuweza kuwafikia wahitaji moja kwa moja, kwahiyo DHL tumekutana na wakulima kutoka Njombe, Zanzibar, Mbeya na Kagera,” amesema.

 “Vanila inayozalishwa Tanzania ni bora na inasoko kubwa dunia kwa sababu hawatumii dawa nyingi na mbolea katika kuihudumia hivyo wanaweza kufikia uchumi mkubwa iwapo watageukia kilimo hicho kinachokuwa kwa kasi,” amesema.

Naye Meneja wa DHL nchini, Humphrey Pule amesema kampuni hiyo imejitosa baada ya kuona wakulima hao wanapata shida kwenye kulifikia soko huku akieleza kupitia mkutano huo wametoa elimu ya kutoa tumaini jipya kwa wazalishaji.