Walima korosho wajipanga upya kuuza tani 2,000

Muktasari:

  • Mikakati hiyo iliwekwa juzi katika kikao kilichoandaliwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) na kuhudhuriwa na wakulima, wanunuzi na viongozi wa halmashauri zote za Tanga.

Tanga. Wadau wa korosho mkoani Tanga, wamejiwekea mikakati ya kufanyia kazi changamoto zinazokwaza uzalishaji na ununuzi wa zao hilo ili msimu ujao ununuzi ufikie tani 2,000 kutoka tani 734 mwaka 2017/18.

Mikakati hiyo iliwekwa juzi katika kikao kilichoandaliwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) na kuhudhuriwa na wakulima, wanunuzi na viongozi wa halmashauri zote za Tanga.

Miongoni mwa changamoto zilizotajwa ni kuchelewa kufunga minada ya ununuzi hivyo kutoa nafasi kwa walanguzi kununua nje ya mfumo rasmi kisha kuzitorosha nje ya nchi.

Kikao hicho kilichoongozwa na mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella kilielezwa tatizo la pembejeo kutowafikia wakulima kwa wakati na elimu duni ya utunzaji wake. Meneja wa CBT Kanda ya Kaskazini, Ugumba Kilasa alisema ili kuhakikisha uzalishaji unaongezeka mipango inafanyika ya kuwezesha miche na pembejeo zipatikane wilaya za Muheza, Pangani, Kilindi, Korogwe na Tanga tofauti na sasa zipo Mkinga tu.

Naye mkulima kutoka kijiji cha Gezani, Mbwana Mamboleo alisema hakuna njia ya mkato kwa wakulima kuongeza uzalishaji kama hawafuati kanuni za utunzaji wake ikiwamo kusafisha na kutoa vitawi kwa wakati.

“Kupata mavuno mazuri kunaanzia kusafishia mikorosho, kuipogolea na kutoa vikonyo. Kuweka dawa inafuatia” alisema.